Thursday, October 8, 2009

Mwangwi wa ushindi wa zabuni kwa Jeetu Patel na hatima ya 'maadili ya biashara' nchini

Vyombo vya habari tena vimekuja na taarifa inayostua masikio na kutia 'simanzi' ukifikiria kwa undani. Lakini ni wazi kuwa hilo linalozunguzwa na kuandikwa ndilo hasa lililotokea. Nalo ni kwamba Jeetu Patel kupitia kampuni yake ya Escort Tanzania ikiwa kampuni mama ipo India, kashinda zabuni ya kusambaza matrekta ya KILIMO KWANZA kwa JKT,zabuni yenye thamani ya bilioni 50 fedha za kitanzania.
Waziri mwenye dhamana amekiri kuwa hakuna shaka yoyote kuhusu kuwepo kwa harufu ya rushwa na zabuni imetolewa katika misingi ya uwazi na uwajibikaji kwa kampuni husika.
Habari hii katika gazeti la Mtanzania Daima iliibuliwa kama vile mfanyabiashara maarufu nchini Yusuffali Mehbub 'Manji' kuwa hakuridhika na 'mchakato' wa ushindi wa Patel. Gazeti hili lilidai kuwa Manji anaona kuna harufu ya 'Takrima' hadi kufanya Jeetu awa mzabuni bora.
Gazeti la serikali la kiswahili 'Habari Leo'lilikuja na kanusho la taarifa za Mtanzania Daima, likinadi wazi kuwa Manji moyo wake mweupe na hana kinyongo na maneno ya Mtanzania Daima hayana hata chembe ya 'ukweli'.Lililowazi ni kwamba Patel kaibuka kidedea katika zabuni ya serikali inayomshitaki!Nasema ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni.
Makala haya haijadili ushindi wa Jeetu Patel kupitia kampuni yake ulikuwa wa halali au la, hiyo ni kazi ya kipolisi,IGP wakili Said Mwema na vijana wake na upande mwingine Kamanda Dr. Edward Hosea na vijana wake wa TAKUKURU, ndiyo wanaweza kutoa majibu sahihi ya nini kilitokea hadi Manji kakosa Patel akaonekana lulu.
Bali siye tutajaribu kutupia macho ushindi huu wa 'mtuhumiwa' wa kesi ya Uhujumu Uchumi,wa fedha za EPA J Patel una maana gani katika elimu ya maadili ya biashara(Business Ehtics).
Nikisoma maoni ya mtanzania fulani katika mtandao wa gazeti la serikali 'Habari Leo' chini ya habari 'Manji akiri kukosa 'dili' la kilimo kwanza' alionesha wazi kuwa ushindi huu wa zabuni kwa Jeetu Patel umeleta 'ukakasi', kwa kuzingatia kuwa J.Patel ni mtuhumiwa wa EPA!
Hapa kuna mambo mawili tunaweza kuyaangalia mosi sheria zetu na pili ni hili la elimu ya maadili kwa wasomi wa vyuo vikuu. Ambao ninaamini ndiyo waliunda jopo la kupitisha zabuni kwa Jeetu na kampuni yake ya Escort ya India.
Katika sheria inaonekana wazi kuwa hatuna sheria inayodhibiti mtu aliyefikishwa mahakamani kwa kosa kama la 'UHUJUMU UCHUMI' kuendelea kushiriki zabuni tena za serikali nayo ndiyo inayomshitaki!
Katika hili lazima tuangalia sheria zetu kwani zinaonekana wazi kuwa zimezeeka. Kwani kama tumeweza kushikilia pasi yake ya kusafiria, iweje tunashindwa kuweka kipengele kama hiki ili kulinda nidhamu ya mahakama!
Lazima ieleweke kuwa msingi mkuu wa sheria ni kuwatumikia jamii ya watu husika, sasa kama nilivyoonesha hapo juu kuwa watanzania wamepatwa na 'ukakasi' juu ya ushindi wa mfanyabiashara huyu mkubwa nchini, ambaye watu fulani waliweka wazi kuwa yupo katika kila 'utafunaji' mkubwa wa pesa nchini usiao halali.Ni wazi kuwa tunahitaji sheria katika hili, ili kulinda siyo tu heshima ya mahakama, la bali pia kuweka urari uliosawa kwamba mfanyakazi akishitakiwa na kuwepo mahakamani kwa zaidi ya miezi sita basi kuna haki zake zinasimama pia mshahara unaanza kutoka nusu,mfanyabiashara naye hapaswi kufaidi tu huku yu katika kizimba.Hii ni nchi ya wafanyakazi na wakulima,SIYO!
Pili lazima sasa tuanze kufundisha somo la maadili ya bishara(Business Ethics) vyuoni kwa wasomi wetu ama la itakuwa kichekesho kila siku. Maadili ya bishara si sheria, isipokuwa ni uwezo wa kutafsiri nakuamua lipi jema na lipi baya kulingana na hali ya watu wa jamii husika, kwa faida ya jamii hiyo katika tendo husika.
Tanzania vyuo vingi vinafundisha 'Business Ethics and Law', si sawa hata kidogo.Ni IFM(Institute of Finance and Management) pekee ndiyo wana kozi ya Business Ethics kwa wanafunzi wa MBA International Business wanayoendesha na Taasisi ya Biashara ya Nje ya India.Kwani katika kozi ya Business and Law ambayo vyuo vingi vya elimu ya juu wanaendesha wameweka nguvu nyingi katika kufahamu 'vifungu' vya sheria na si maadili ya biashara mara zote hiki kinasahaulika!Kiukweli maadili ndiyo biashara ya Ulimwengu wa leo na hasa ushindi katika soko la Ulaya upo katika kampuni zenye maadili.
Na hili ndiyo hayo matunda ya kumpa zabuni Jeetu, kwani kama sheria haipo wale wahusika katika huu mchakato wangejiuliza tafsiri ya kumpa Jeetu zabuni kwa wakati huu ni nini?Hapa wangeweza kumuondoa mapema katika mchakato. Linawezekana hata kama fedha zenyewe asili yake ni India.
Hebu tuone mifano michache ya maadili ya biashara ili tuone sheria na watawala wanavyoweza kuepukwa na badala yake maadili kufuatwa kwa faida ya jamii na ukuaji wa biashara kwa ujumla.Charles Cadbury wakati majeshi ya Uingereza yanakwenda kupigana Afrika Kusini katika 'Anglo Boer War' alitakiwa kuwauzia biskuti,lakini kwa vile yeye hakuunga mkono ile vita 'kimtizamo' aliuza bila faida! Na hili alilifanya kama uoga kwa utawala wa kifalme lakini alikuwa tayari wafanye wengine ila alilazimishwa.
Vivyo hivyo wakati fulani kampuni zile zote zilizokuwa zikifanya maandalizi ya tamasha la mwanamuzi Robert Kelly maaruku kama R.Kelly na Shawn Carter maarufu kama 'JAY-Z' kwa ajili ya uzinduzi wa albam ya 'Greatest of the both world' zilijitoa pale Kelly alipofikishwa mahakamani kwa madai yakujihusisha na mshichana aliye chini ya miaka 81 kimapenzi.
Si kama walimtenga Kelly wakati wa shida la hasha walimamisha uzinduzi kwa vile ingekuwa ni kama 'kuunga' mkono kitendo alichokuwa 'akituhumiwa' kukifanya kuwa ni cha heri. Na wala siyo kuwa nao pia waliungana 'kumsulubu' Kelly hapana isipokuwa ni kuheshimu maadili ya biashara na kulinda heshima ya mhimili mmoja wapo wa utawala MAHAKAMA.
Ingawa Kelly alishinda tuhuma zile na mahakama huru kumuona hana hatia, lakini lililowazi ni kwamba huwazi kufanya jambo na mtu ambaye yu kizimbani tena ambalo linaleta faida ya kibiashara, hata kama mtu huyo ushahidi unaonesha kuwa yu hana hatia. Na huu ndiyo msingi mkuu wa maadili ya biashara kulinda 'masilahi' ya wengine, vivyo hivyo zabuni ile hakupaswa kupewa Patel ili kulinda masilahi ya Jamhuri ambayo inamshitaki.
Kwa hili hatupaswi kumlaumu Patel, ila kama nilivyosema, huu ni wakati sasa wa kungalia elimu yetu ya biashara na kuingiza somo hili la maadili biashara(Business Ethics) pia kuangalia sheria zetu katika kuhakikisha hatui wachekeshaji katika nchi yetu wenyewe.
Katika nchi za Ulaya na Marekani kampuni zinazozingatia maadili ya biashara ndizo zinazofanya vizuri sokoni na walaji wana muamko katika kuhakikisha bidhaa wanazotumia si za kiyonyaji, hazitumikishi watoto katika kuzalisha bidhaa zake, zinalinda mazingira, hazitoi hongo ndani na nje ya nchi, zinatoa bei nzuri kwa wakulima wa nchi masikini ( Fair Trade na Body Shop). Haya ni maeneo machche tu.

No comments: