Friday, May 1, 2009

Anguko la Uchumi la Ulimwengu na majaaliwa ya MBA

Anguko la Uchumi wa Ulimwengu limeleta madhara makubwa lakini lililowazi ni juu ya UBORA na UMAKINI kwa ujuzi unaotolewa katika elimu ya biashara DUNIANI.
MBA imekuwa ni elimu pendwa kwa sasa, kunamadai hasa nchini Marekani juu ya ubora wa ELIMU ya MB kunakoibuliwa na kushindwa kwa wasomi wake kutoa muelekeo wa wazi na kulinda uchumi wa DUNIA.
Kampuni kubwa za kimerakani zilizoanguka zinaongozwa na wataalamu wa biashara kutoka vyuo bora kama vile Havard. Sasa nini kimefanya washindwe kutoa hali halisi ya mambo?Fuatilia makala hii.

Tudhibiti mabango makubwa ya sigara

‘Hakuna anayeweza kukwepa ushawishi wa matangazo katika Ulimwengu wa leo’, ni maneno ya Papa Paulo wa VI , kama alivyonukuliwa katika kitabu cha Ethics in Advertising.

Nimehisi ni vyema kuanza na nukuu hiyo hapo juu kuweka wazi juu ya ukweli kwamba matanzago yana nguvu kubwa sana kijamii,kisiasa,kiuchumi na kiutamaduni. Hakuna anayeweza kupinga uhitaji wa matangazo katika jamii yetu ya leo. Ulimwemgu wa biashara umeweza kwenda na kufikia mafanikio hayo iliyo yapata kutokan na mchngo mkubwa wa matangazo yamechukua.

Matangazo yamefanya vyema kazi ya ‘kuziba pengo’ kati ya mzalishaji na mlaji. Fikiria jinsi bidhaa zinazozalishwa Uchina zinavyoweza kupenya kiurahisi katika soko la kijiji cha Kitangali, Newala Mkoani Mtwara. Ni kilometa elfu ngapi kati ya Uchina na Kitangali, lakini kwa vile matangazo yameweza kutolewa walaji wameikubali na kuifahamu bidhaa husika.

Kisiasa matangazo yameonekana jinsi yalivyo na nguvu katika kampeni za Uraisi wa Marekani ambapo Rais Mwafrika wa kwanza mwenye asili ya Kenya, Barack Hussein Obama ameweza kuingia Ikulu ya nchi hiyo maarufu kama ‘White House’

Matangazo hapa yalitumika vizuri katika kushawishi umma wa Wamarekani kumpigia kura bwana Obama. Lakini si wakati wote matangazo yanakuwa na taswira nzuri kwa wanajamii.

Ulimwengu unakumbuka mauji ya kimbari ya Rwanda yaliyotokea mwaka 1994-1998 na kuuwa zaidi ya watu 500,000 wengi wao wakiwa Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa kadiri. Matangazo ya radio, magazeti na televisheni yalichochea kwa kiasi kikubwa mauji haya mabaya ya kimbari kuwahi kutokea katika historia ya bara hili.

Niwazi kuwa nukuu ya maneno ya papa yana ukweli kwani hakuna leo hii ambaye hajaweza kujikuta amefanya jambo lenye manufaa au lisilo na manufaa kwake au jamii yake pasi na kusukumwa na matangazo ama ya televisheni,radio ,magazeti,mabango,au ya ‘kitekinohama’.

Kimsingi matangazo yana faida na hasara na usipoyatumia vizuri huleta hasara zaidi ya faida. Wapinzani wa nadharia za taaluma masoko mara nyingi wamekuwa wakitumia ‘uoza’ unaotokea katika jamii unaosababishwa na matangazo ambayo kwa kiasi kikubwa ni kazi ya wana taaluma wa masoko.

Kwa kutambua ukweli kwamba madhara yake ni mabaya hasa kukitokea taarifa yenye harufu ya uwongo wa kukusudia, ni muhimu tukidhibiti matangazo.Tunaposema kudhibiti matangazo tunamaanisha mfumo mzima wa utayarishaji na utoaji wa matangazo lazima udhibitiwe.
Tunataka tuangalie kampuni zinazo andaa matangazao haya ya kibiashara nchini zinawatu wenye taaluma ya biashara. Je sheria zipo zinazodhibiti matangazo?Sheria lazima nazo zianishe wazi udhibiti huu ni katika nini?

Udhibiti wetu wa sasa hivi ni wa ‘kitraditional’ zaidi. Kwa mfano unadhibiti kampuni ya sigara isifanye matangazo yake katika redio na televisheni. Lakini unampa nafasi ya kuweka mabango katika makutano ya barabara kubwa! Hiki kichekesho.

Lazima udhibiti uende hadi maeneo ya kuweka mabango katika barabara.Katika nchi ambayo asilimia 10 ya watu wake wana umeme, ni sawa na watu 4,000,000 ( Taarifa za karibuni za Bwnki ya Dunia inaonyesha Tanzania ina watu milioni 40).

Tukadirie tu kwamba watu hawa milioni nne ndiyo wenye TV, ni wazi kuwa kundi hili ni dogo, hivyo sheria yetu imejikita kulinda watu wachache ikawaacha watu wengi. Si maanishi kwamba kundi hili halikupaswa kulindwa lakini kimsingi watu wenye kuathirika na matangazo ya sigara niwatu wa vijijini ambao hawana umeme na hili ,linajidhihirisha na idadi ya vijana wa vijijini wanao anza kuvuta sigara. Takwinmu za Tanzania sasa zinaonesha kuwa ni miaka 8, na wengi wao wapo vijijini.

Iweje kijana wa miaka 8 aanze kuvuta sigara wakati hana hata televisheni, hili limechangiwa zaidi na kuachia kampuni za sigara kutumia maeneo yanayopitwa na watu wengi huku wao wakiwa na mabango makubwa ya matangazo.

Tangazo la TCC lilikuwa linasomeka hivi ‘Haya ndiyo maisha’ likiwa na vijana wakiwa katika boti wakivuta Sweet Menthol(SM), hii haitoshi sasa hivi wanabango kubwa la sigara ya Iceberg linalouliza ‘umeshaijaribu’.

Mabango haya yapo katika vituo vya daladala(Bus Terminal) ambavyo watoto wetu wanapoenda shule wanavitumia. Sasa hapa tumelinda nini? Huku barabarani wako peke yao, hawana mtu wa kuwashauri wanakutana na bango la ‘Haya ndiyo maisha’. Hapo ndipo unapowapata watoto wenye umri wa miaka 8, wanavuta sigara.

Inakadiriwa kuwa asilimia 35 ya watanzania leo hii ni wanavutaji wa sigara. Hii ni zaidi ya asilimia 10 ya wetu wenye umeme ambao tunaweza kujiridhisha kuwa wanamiliki TV. Na idaidi inakadiriwa kuongezeka.

Thomas Lauria mdau wa taasisi moja inayojishughulisha na tumbaku nchini Marekani aliwahi kunukuliwa akisema’Sisi tuko na nguvu kwasababu tumeajiri watu 700,000 na watu milioni 50 wamechagua kununua bidhaa hii, hii ni zaidi ya kura kwa Bill Clinton’

Huu ndiyo umekuwa ushawishi wa tumbaku kila mara wanapoambiwa kuwa tumbaku si rafiki wa binadamu, wao wanajificha katika chumo ‘hasi’ la kiuchumi.Kwa mfano katika Marekani pekee ambako tumbaku ilianza kabla ya kusambaa maeneo mengine ya Ulimwengu, mwaka 1994 kampuni za sigara zilijikusanyia dola bilioni 47.1, lakini serikali ilitumia dola bilioni 50 kutibu magonjwa yanayotokana na kansa kwa watu 153,000.
Tanzania kansa inatibika bure, lakini tuna uwezo huo wa kiuchumi?Ya nini kununua kifo , kwa fedha uliyoitafuta kwa jasho!

Hapa ni tiba tu, hatujakadiria madhara ya kimazingira yanayotokana na tumbaku ambayo sisi tumeifanya kuwa ndiyo mama na baba yetu!Kwani tumekubali kuacha mabango yakiwekwa hovyo hovyo tu.Tena tumewaruhusu kutumia maeneo ambayo ni ya kiushindi(Strategic Areas) kuliko hata redio au televisheni.Bango kubwa la tangazo la sigara linawekwa katika makutano ya barabara na vituo vya basi. Hii
ni hatari.Tanzania ni ya tatu kwa kuzalisha tumbaku Duniani imeipiku Afrika kusini!Hii maana yake nini?

Tuondoke katika udhibiti wa ‘kimamlaka’ na tuende katika kuwa na sheria ya wazi inayodhibiti matangazo. Sasa hivi kuna TCRA na TFDA, wale walio chini ya malaka hizi kibiashara wanajaribiwa kudhibitiwa, lakini bado tatizo ni kubwa zaidi kwani hapa ni malaka ndoyi imepewa uwezo wa kisheria, na siyo jamii nzima.

Sheria za kimamlaka zinabebesha mzigo watu wachache ambao kimsingi hawana uwezo wa kiutendaji katika kudhibiti hata lile tulilowakabidhi. Kwa mfano sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi ya Mwaka 2003 inaonesha wazi kuwa TFDA ndiyo yenye uwezo wa kuidhinisha tangazo litoke ama la, ambalo wao wanahusika nalo.

Sina uhakika kama matangazo ya sigara ni yao, lakini itakapo kuja dawa ya kansa kuonekana tangazo lake limetia ‘chumvi’ sana wao wanatakiwa kuwajibika.Tatizo hapa tunaweza tukajikuta tunadhibiti matokeo badala ya kiini kilicholeta matokeo.

Gazeti la Daily News (Tanzania) la tarehe 6,Machi,2006 linahabarisha umma kuwa wenye kampuni za matangazo mara zote wameshindwa kwenda TFDA kupata kibali cha kurusha matangazo yao kama sheria inavyowahitaji kufanya. ‘Mara nyingi tumeshindwa kufuata sheria hii kwa sababu ya haraka ya wateja na msukumo wa kujipatia faida’lilinukuu Daily News.

Kiu ya kupata faida imefanya kampuni zetu zivunje sheria za nchi, na hili linatufanya tuhoji watu walio katika biashara hii kweli wanauelewa wa biashara, na kama wapo waliosoma, huko waliko pata vyeti vyao walipata msasa juu ya ‘maadili ya biashara’?

Matangazo yetu yanayotoka mtu yoyote akiyaona, kusikia, au kusoma atabaini kuwa watu wengi wamefanya taaluma ya biashara kama ‘kichaka’ cha kuficha na hasa taaluma ya masoko.

Uzembe huu unahimiza uwepo wa chombo cha kuratibu taaluma ya biashara la sivyo, matangazo hatari yatakuwa yanaibuka kila leo. Mtu aliyesoma taaluma ya masoko hata kwa ngazi ya cheti atakuwa amewahi kusikia kitu maadili ya biashara na umuhimu wake katika ukuaji wa kampuni husika.Hivyo hawezi kuingia katika mtego kama huu wa kuhitaji faida bila kuzingatia maadili. Isieleweke kuwa hawapo ila yatupasa sasa kuchambua yupi amefuata faida na yupi ana dhati ya kweli katika kufanya biashara inayolinda nchi yake pia.
Bila chombo cha kuratibu na kupiga msasa wataalamu wa biashara nchini kama vile watu Uhasibu(CPA) au Ugavi(NBMM), taaluma ya masoko itaendelea kuwa kichaka na matangazo hatari hayatadhibitika kiurahisi.Tukijipanga inawezekana, chukua nafasi yako.