Sunday, April 18, 2010

Afrika ya weusi haiwezi kutumia ‘boom’?

‘Afrika haiwezi kutumia vyema kupanda kwa bei katika soko la ulimwengu (boom) wala kujihami na majanga yanayoathiri uchumi wake’ Hi ni sehemu ya taarifa ya ripoti ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) kuhusu muenendo wa biashara na uchumi katika Afrika miaka 90.
Tumeona ni vyema kuanza na maneno hayo katika makala haya ili kujenga tafakari pana ya Afrika ya weusi na majaaliwa yake. ADB inaona hali hii na inaona jinsi bara hili linavyoshindwa kufanya vyema hata kama likawa na ziada kutoka mazao ya mashamba yake.
Afrika ya weusi haina ukame wala neema kila siku ni vilio, ni hali ya muda mrefu lakini lenye kuti uchungu ni kuona hali hii ikionekana kukomaa kama ni stahiki kwa bara hili. Isionekana kama tumekata tamaa la hasha ila tunajaribu kutafuta nji ya kutokea.
Mavuno yakiwa mazuri Afrika bado kuna watu watakufa njaa na wakulima watapata hasara kwa kukosa kuuza mazao kwa bei nzuri na hata kuharika. Hali hii inaonesha Afrika inahitaji zaidi ‘breki’ kuliko ‘kasi’ inayoenda nayo.
Ripoti moja ya UNDP inaelezea Tanzania kupoteza zaidi ya asimilia 60 ya matunda yake kuoza huku bado nchi ikiwa muagizaji mkubwa wa juisi za Maaza, toka Falme za Kiarabu, na Ceres (Hili ni jina la Mungu wa dini za kale za Kigiriki, Mungu wa uzao wa Ardhi) toka Afrika Kusini na Del Monte toka Kenya.
Bidhaa hizi zikifurika katika soko la ndani huku wakulima wa matunda katika mikoa ya Tanzaga, Iringa na Morogoro wakiingia katika lindi la umasikini. Hii ni hali ya kawaida hasa katika Afrika ya weusi.
Hivi karibuni kuna taarifa inaoashiria hayo ya ADB kuwa bado yanaendela katika Tanzania. Naibu Waziri wa Kilimo na Ushirika Dokta Mathayo amekaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa wakulima wa nafaka wa Rukwa walio na kitisho cha kuharibikiwa zaidi ya tani 1.2 za mahindi kwa kukoka soko serikali iko mbioni kupata takwimu za ukweli. Taarifa hii ya kitisho cha kuharibika kwa nafasi Rukwa zilitolewa na Serikali ya Mkoa!
Hili likitokea kuna taarifa za kitafiti kuwa watanzania zaidi ya milioni 8 huwa wanashinda njaa kila siku. Hii ndiyo hali ya kutoweza kutumia ‘boom’ umevuna unashindwa kuuza, huku kuna wanaohitaji nao wakiwa hawajui watapata wapi!Sababu kubwa za hali hii imekwisha elezewa sana nalo ni miundo mbinu leo halina nafasi hapa.
Ni wazi kuwa mzunguko huu hauna mwisho mwema, na umasikini utaendelea kutuzunguka wakulima wa mahindi pia wale wanaoakadiriwa na kitisho cha njaa wataendelea kukiona cha moto huku kuna wenzao nafaka zinaoza. Hali ya mambo inaonesha kupanda kwa mfumuko wa bei, na hili katika tafsiri rahisi ni kuwa bei ya vyakula imepanda na hasa vyakula vikuu na hapa tunazungumzia mahindi, sasa iweje tena kuna watu wanakosa soko!Kuna dosari mahali.
Hivi karibuni Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameruhusu wakulima wenye shehena za mpunga kuuza nje ya Tanzania. Hatua hii ni mwanzo mwema kuelekea kuwaunganisha wakulima wetu na masoko ya nchi jirani.
Ila wasiwasi wetu ni namna ya kuratibu zoezi hili. Isieleweke kuwa wakulima hawawezi kuuza katika soko la ndani na wala kwamba soko la ndani limeweza kupata inachohitaji isipokuwa ni wakwamba muenendo wa soko umeshindwa kuwaunganisha wakulima hawa.
Tatizo ni wakulima wetu kuunganishwa katika soko la ndani. Ni sisi tunaouza mchele huu nje punde tu tutaenda Thailand na Vietnam kuhitaji kununua mchele. Sasa kwanini tusiwaunganishe wakulima hawa na soko la ndani?Kwa nini tusinunue na kuhifadhi nafaka hii? Strategic Grain Reserve I wapi?
Hapa tena tunashindwa kutumia ‘boom’. Nilishatahadharisha katika makala iliyopita katika siku za nyuma kuwa bei ya mchele Duniani haionekani kupungua na hili linasababishwa na India na Philippines ambao ni walaji na wauzaji wakubwa wa mchele pia kwenda sokoni kuhaha kutaka kununua mchele. Unapomuona muuza mkubwa kaingia sokoini kununua ujue kuna jambo, India yupo sokoni.
Ingawa Philippines alipandisha dau la bei ya mchele lakini hakupata tani alizokuwa anahitaji.India yupo sokoni kwa vile anakabiliwa na hali mbaya ya hewa iliyokuwa kitisho kwa zaidi ya tani 650,000. Hivyo kuamua kupiga marufuku kuuza mchele nje ya nchi.
Tanzania si mmlaji wa mchele kama chakula kikuu ila tunaenda Asia kama kimbilio la njaa. Hali ya mambo ya bei ya mchele duniani inaonesha wazi kuwa hata ule mchele daraja la mwisho toka Vietnam uliovunjika kwa zadi ya asilimia 25 umepata soko katika Afrika nchi kama Mali, Senegal na Nigeria ambayo huagiza zaidi ya asilimia 60 ya mchele.
Hali hii inaonesha sisi hapa tunachezea ‘boom’ kwa kujifariji kuwa ni bora wauze katika masoko ya nchi jirani kwa hoja kuwa tumeshindwa kununua. Lakini hatari i yaja. Kwani bei ya nafaka na hasa mchele haitapungua zaidi ya dola 600, huku Thailand muuzaji mkubwa wa mchele duniani akisusa akingoje walau ipande.Ipande mpaka wapi hakuna anayejua, ni soko limeachiwa liamue.
Pia shirika la OECD, linabainisha wazi kuwa mchele hautashuka zaidi ya dola 600 kwa tani tena huu ni wa dajara la chini (25% broken) kwa vile Ulimwengu umeweka nguvu katika kutumia mahindi kutengeneza nishati ya mafuta (bio fuel) , hali ambayo inafanya mchele ugeuzwe kama chakula cha mifugo katika Uchina, Marekani na Ulaya!
Katika miaka ya karibuni China imebadili uuzaji wa mchele nje huku ulaji wa nyama ukipanda kwa zaidi ya alimia 40 hali inayoelezewa inatokana na kutumika kwa mchele kama chakula cha mifugo. Na Japani moja ya watoaji wa misaada ya mchele kwa Afrika iliyokatika hatari ya kuharibika na hasa kama wanasafisha maghala inatoza kodi wakulima wake wanaotumia ardhi kulima mpunga huku ikiwapa motisha wale wanaolima matunda na mboga mboga ‘tozo’ toka katika wakulima wa mpunga. Hali hii inafanya mchele kupungua duniani.
Pamoja na hayo Afrika ulaji wa mchele unaongezeka hali inayochangiwa na kukuwa kwa daraja la kati katika nchi nyingi za kusini mwa jangwa la Sahara, Tanzania ikiwemo.
Muenendo huu wa soko la nafaka duniani unaashiria kuwa sisi tunacheza na ‘boom’ tena katika nchi ambayo zaidi ya watu milioni 8 wanashinda njaa! Ni vyema tukaipa uwezo Strategic Grain Reserve wa kununua na kuhifadhi nafaka hizi kuliko kupigia chapuo uamauzi wa kuuza nje.
Na isitoshe utaratibu huu wa kuuza nje unapaswa kuratibiwa vyema kwani ni wazi kuwa soko la kimatiafa linasumbua na kama watu wetu hawakujipanga vyema tutaishia kuwa watengeza ajira kwa wenzetu. Kuna mashine za kukoboa nafaka, basi tusiuze nafaka ghafi ni bora tukawauzia mchele ulioongwezwa thamani.