Wednesday, October 14, 2009

Mifumo yetu ya elimu na heka heka za ufadhili wa kimasomo

Waatalamu wa maendeleo na wachumi kwa pamoja wanaungama kwamba kukosekana kwa 'nafasi sawa'(Lack of Opportunities) mara zote ni sababu kubwa inayopelekea kuongezeka kwa umasikini barani Afrika na hasa Kusini mwa jangwa la Sahara.
Mara zote nafasi inapotokea ama iwe inachelewa kuwafikia walengwa, au hata walengwa kukosa taarifa sahihi wapi waanze na wapi waishie ili kufaidi nafasi husika. Kudoda kwa mapesa ya mabilioni kwa mabilioni katika taasisi za kifenda kwa ajili ya mikopo ya wajasiriamali, kushindwa kujitokeza kwa watu wenye sifa katika nafasi mbalimbali za fadhili za kimasomo nakadhalika nimaeneo machache tu yanayoweza kuorodheshwa.
Changamoto kubwa ipo katika mifumo yetu hasa inapokuwa 'hasi' katika kuhakikisha tunafaidi nafasi hizi za ufadhili zinapotokea. Makala haya itatupia jicho mifumo yetu ya elimu nchini Tanzania na jinsi inavyoviza fadhili mbalimbali kwa watanzania nje au ndani ya nchi kwa ajili ya masomo.
Madai ya kuwa watanzania tumeshindwa kutumia nafasi tena wakati mwingine zinakuja kwa anwani ya kwamba mwanafunzi awe wa Tanzania yamesikika mara nyingi. Na lililowazi ni kwamba nafasi hizi ni adimu na zinatokea katika nchi ambayo si kwamba watu wake wanakipato cha kutosha bado tupo katika dola 270 kwa mwaka. Kwa kuzingatia hili nafasi za ufadhili wa kimasomo ni muhimu kwetu, kwani bado idadi ya walio na sifa kushindwa kuendelea na masomo ni kubwa na lenye kuhuzunisha ni kwamba wakati wote pesa imekuwa ndiyo kikwazo.
Swali ni kwani nini tunashindwa kutumia nafasi hizi?Taasisi za elimu ya juu nchini Tanzania mara zote zimekuwa vigingi katika kuelekea kufaidi nafasi hizi za ufadhili. Hili limetokana na jinsi tunavyofanya kazi ama la kuwa 'kizamani' au 'kuamini' kuwa lazima vikao vikaliwe ndiyo jambo fulani liweze kupitishwa.
Mathalani suala la vyeti na taarifa ya maendeleo ya mwanafunzi (transcript) imekuwa kero hasa kwa wahitimu. Maeneo mengine hati hii inahitaji kusaniwa na DVC! Mifumo hii mara zote inaleta 'uzubavu' katika kutumia nafasi. Hatuna tatizo kwa DVC kusaini, lakini kimtizamo naona DVC wakati wote amekuwa na kazi nyingi, na kimsingi yeye hawezi kuwa anamfahamu mwanafunzi zaidi ya watu wa Idara au Mkuu wa fakati husika ya mwanafunzi.
Kuna vyuo hii nikazi ya Mlezi wa fakati na si kazi ya DVC, katika hili utaona ambavyo mambo hayalegi, matokeo yakitoka idarani mwanafunzi anayathitisha yanaenda kwa Dean hati ya matokeo inasainiwa, kijana anapata 'transcript' anaendelea kusubiri cheti huku heka heka za maisha baada ya chuo zikiendelea.Chuo kinachotumia utaratibu huu ni Mzumbe na mara zote wanafunzi wamekuwa wakijiuliza kwa nini vyuo vingine hati zinachelewa pamoja na vyeti lakini si kwa Mzumbe!
Katika ulimwengu wa leo elimu ni 'biashara' chuo kinacho kuwa makini katika kutoa matokeo na kufanikisha kudahili kwa wakati kinapata wanafunzi wengi tena kwa wakati na wale wanaoweza kujilipia pia wanakuwa wanafanya hivyo.
Tanzania ni nchi ambayo kama niliyotangulia kusema mifumo ya elimu inadumaza kutumia nafasi za ufadhili. Nafasi kede kede zinaendelea bila kupata mtu wa kuzitumia, kisa taarifa ya udahili, oooh kikakao cha seneti bado. Elimu ni biashara narudia tena, lazima iendane na matakwa ya wateja.
Hebu tuangalie mifano michahe kuonesha jinsi tulivyokuwa na mifumo mibovu inayotunyima kutumia nafasi za ufadhili katika nchi yetu za kimasomo. BTC (Belgium Techniocal Cooperation)huwa inatangaza nafasi za ufadhili kwa wanafunzi waliopata udahili kwa vyuo vya ndani na ndani ya Afrika Mashariki. Ufadhili huu unakuwa katika ngazi ya shahada ya Uzamili(Masters) na Uzamivu(PhD).
Matangazo haya mara nyingi huwa yanatoka kati ya mwezi wa nne hadi wa tano kwa mwaka husika. Kipindi hiki vyuo vyetu bado havijatangaza kupokea maombi ya udahili kwa mwaka husika. Bado hata vikao vya udahili havijulikani vitakaa lini na tangazo litatoka katika gazeti gani. Mara zote kuanzia mwezi wa sita hadi nane na mwezi wa tisa heka heka za matangazo na udahili zinakuwazimeanza.
Matokeo kutoka ili kufahamu umepata au umekosa ni mwezi wa tiasa hasa.Na ule udhamini unaotolewa na BTC unakuwa unamwisho wa kutuma maombi mara nyingi tarehe zao zinakuwa ni chini ya kuanza kwa kutuma maombi chuoni. Hii inaonesha wazi mifumo 'iliyozeeka' isivyoweza kuwapa nafasi watanzania kutumia neema ya ufadhili katika kujiendeleza kimasomo katika nchi yao wenyewe!
Shirika jingine la Osienala (Friends of Lake Victoria) lenye makao yake Kenya hutoa udhamini kwa wanafunzi wa Afrika Mashariki kusoma katika vyuo vya nchi hizo kwa shahada ya uzamili katika fani za mazingira, maendeleo, biashara nakadhalika, hutoa nafasi hadi mwezi wa tano tarehe 30. Bado kilio kile kile nafasi hii kwa wasomi wa Tanzania hawawezi kuitumia kwani muda wa udahili na vikao vya seneti bado nchini!
Njia hii ya ukale wa kutuma maombi kwa vyuo vyetu ni wazi kuwa inatutoa katika soko la ushindani wa kielimu. Hivi karibuni nimepata fununu kuwa The Open University of Tanzania watakuwa wanapokea maombi kwa mwaka mzima hii ni hatua ya kupongezwa. Na lililowazi sasa yatupasa kutambua kuwa mfumo wa vikao vya seneti umepitwa na wakati katika kuuza elimu.
Njia sahihi ni kuacha idara iangalie wanafunzi inaowahitaji kwani ndiyo walimu na wao wapeleke majina kwa Idara ya Elimu ya Juu (Directorate of Postigraduate Studies) kwa taarifa na kuandikwa kwa barua kwa mwanafunzi husika.Hili haliitaji seneti kwani 'member' wa seneti siyo wote watakao mfundisha mwanafunzi na wala hawana hata utalaamu wa shahada husika, sasa kwanini wao ndiyo wawe na nguvu katika hili?
Katika nchi za Ulaya na Marekani utumaji wa maombi huwa mwaka mzima na mwanafunzi anapaswa ataje anaingia majira gani ya mwaka, na hili linafanya wanafunzi wawe katika nafasi nzuri ya kutafuta wafadhili.Pia maombi hutumwa kwanza katika idara yako. Tanzania inakuwa kinyume chake,nacho hudumaza heka heka za kutafuta ufadhili.
Vyuo vya elimu ya juu lamiza vibadilike, ili kuhakikisha vinauza elimu na si kuendelea kuwa kigingi katika kuwezesha watanzania kufaidi nafasi za ufadhili. Katika zama za mawasiliano ya kompyuta hili linawezekana.
Yatupasa kutumia nafasi hizi kwa kubadili mifumo yetu, simaanishi kuwa hawapo ambao hawajanufaika na BTC lakini wengi wao waliomba na mara zote ni wale wanaojuana na wahusika ndiyo walipata barua za Partial Admission wakisubiri vikao vya seneti , barua hizi ziliwasaidia kupata ufadhili. Sasa hili ndilo linaloleta umasikini kwani nafasi sasa inakuwa si 'sawa kwa wote' ila wale wanaojua kutupa karata tu.
Vikwazo vya kusubiri hati ya maendeleo ya kitaaluma hadi isainiwe na DVC imepitwa na wakati hii ni kazi ya Dean wa Idara husika. Na hasa katika kipindi hiki cha kuuza elimu ambacho mteja anapaswa kukimbizana na muda kwani muda ni pesa na kuchelewa kwake ndiyo hatari yake ya kupata ufadhili na kukosa kwake ni kukosa kwako (CHUO) kuuza elimu.
Huu ni mzunguko hauja mkomoa mwanafunzi hata chuo nacho kipo katika kukosa mapato pia, na hasa inapokuwa huyo mwanafunzi ana sifa stahili za kupata ufadhili. Shime wasomi wakati umefika wa kuondoa vikwazo katika kuuza elimu na hasa katika kuhakikisha tunakwenda sambamba na matakwa ya wateja hasa wafadhili wa kimasomo, na hili ni kuendana na muda wao tu. Tuanze kudahili kwa wakati na jukumu hili liwe la idara husika, pia tuwe na udahili wa mwaka mzima kupitia mtandao.Ili tuweze kuongeza kipato na kupambana na ukata unaosababishwa na bajeti finyu ya serikali.

No comments: