Sunday, July 27, 2008

Kufurika kwa viatu kutoka Asia ni kitanzi


“BAHILI hapendezi! Wanavaa! Elfu moja mia tano! Mpende mkeo! Mpende mwanao…!”

Ni maneno ya wapiga debe, wachuuzi wa viatu kuanzia vya watoto na watu wazima.

Wapiga debe wamejaa katika maeneo mbalimbali ya masoko maarufu ya Mchikichini, Tandika, vituo vya daladala vya Ubungo na Buguruni hasa nyakati za jioni. Mchana hawaonekani wanaogopa mgambo wa jiji.

Viatu vinavyouzwa kwa sh 1,500 ni vipya, vinatoka katika nchi za Asia, hasa China, Thailand na Indonesia. Bei yake huwa haipungui, kwani ni bei ya debe.

Viatu hivi vinauzwa vikiwa vimemwagwa chini. Mteja huwa anachagua anachokitaka.

Kuna vya bei zaidi ya hii, kuanzia sh 1,500. Hakika kila Mtanzania wa kundi la chini, kati na juu katika jamii wamachinga wako tayari kumpatia kiatu na mtindo anaohitaji.

Hakuna ubishi ya kwamba kwa sasa watu wa Asia wanatuvika kwa kila kitu. Na wengi wetu tu nadhifu kwa gharama ndogo sana.

Nia ya serikali ni kuona kila Mtanzania anavaa viatu vya bei rahisi, imefanikiwa kwa kiasi fulani nchini na hasa katika siku za karibuni viatu hivi vipya vimekuwa ni vya gharama nafuu kuliko hata mitumba toka Ulaya na Amerika.

Lakini lengo hili linakinzana na jitihada za kufufua viwanda vya ngozi na viatu vya ndani. Takwimu zinaonyesha zaidi ya asilimia 80 ya viatu na bidhaa zingine za ngozi ama halisi au feki, huagizwa kutoka Asia.

Hii ni hatari kwa ukuaji wa viwanda vya viatu kwani soko la ndani tayari limechukuliwa na Waasia.

Soko la Tanzania sasa limejawa na bidhaa za viatu kutoka Asia kuanzia maeneo ya mijini hadi mashambani.

Kwa watu wengi kutembea bila viatu labda kama umeamua. Swali la kujiuliza, ni je, kufurika huku kwa viatu kutoka Asia na hasa China ni ukombozi au kitanzi kwa viwanda vyetu vya ngozi na viata?

Bidhaa zetu mara zote zimeshindwa kuingia katika masoko ya nje kwa kigingi cha kukosa ubora.

Lakini sisi tumeendelea kupokea viatu hivi kutoka Asia na wala si kwamba vina ubora wa hali ya juu kuliko vya nyumbani, hapana.

Matukio ya kuvunjika visigino na kubanduka kwa soli ni jambo la kawaida kwa viatu kutoka Asia. Kina Dada wengi ni mashahidi wa kadhia hii. Lakini hakuna anayeweza kuzuia viatu hivi kuwa na ubora wa chini.

Makala hii itajaribu kutupia jicho ujio huu wa viatu na mkakati wa sasa wa serikali wa kutaka kuona sekta ya mifugo inachangia vilivyo katika pato la taifa na hatimaye kuwezesha kuchangia katika kupunguza umasikini nchini.

Viatu hivi vilivyofurika kwa sasa katika soko la Tanzania ni vya nusu plastiki na nusu ngozi. Hivyo basi kufanya visiwe vinatumia kabisa rasilimali ya ngozi.

Tanzania ni nchi ya kwanza kwa idadi kubwa ya mifugo katika nchi za SADC na ni ya tatu katika Afrika.

Mara baada ya uhuru kulikuwa na viwanda viwili vikubwa vilivyokuwa vikitengeza viatu navyo ni BORA na MORO Shoes Company vilivyokuwa chini ya Serikali.

Viwanda hivi kwa sababu mbalimbali vilishindwa kujiendesha.

Kufuatia mabadiliko ya uchumi yaliyotokea miaka ya 1985, ilisababisha miaka ya 1990 sekta ndogo ya viwanda vya viatu kupata msukumo mpya uliosababisha kubinafsishwa kwa viwanda hivyo viwili na kuanzishwa kwa viwanda vingine vipya kama vile Lexman cha Arusha, Nyanza Shoes cha Mwanza, Shah cha Moshi, Liberty, Chelsea, Italshoes, Ok Plastics, Ladha Industries na Noble Industries vya Dar es Salaam.

Pia viwanda vya kuzalisha ngozi kwa ajili ya kutengenezea viatu vilichipua nchini. Na inakadiriwa kuwa viwanda vidogo vya kati na vikubwa vipatavyo 30, vilifunguliwa, vikiwa na uwezo wa kuzalisha futi za eneo milioni 30.

Vingi ya viwanda hivi vya ngozi na viatu leo hii vimefungwa. Si kama hakuna malighafi la hasha! Ngozi ipo nchini na inaendelea kusafirishwa kupelekwa katika masoko ya nje na hasa India.

Wale waliokuwa wamefungua viwanda vya viatu sasa wamegeuka kuwa waagizaji wa viatu toka China.

Si kama wamependa, hapana ila ni hali ya soko ndiyo inawafanya wao watafute pa kujishika ili kujipatia riziki.

Kilio kimekuwa katika kodi na sera mbovu za soko huria zinazokumbatiwa na serikali yetu kwa kuwafurahisha watawala wa Washington na Downing Street.

Mafundi wadogo wadogo wa viatu wanaoendesha biashara zao katika baraza za nyumba na ofisi zingine ndogo, ndio wanaoendelea kuzalisha viatu.

Hawa nao wanachechemea wanasubiri tu muda na wakati ukifika wajiondokee.

Kinachowafanya wabaki ni kwa vile wanaweza kujibadili kwa kufanya kazi za kukarabati vile vilivyo chakaa na kung’arisha.

Lakini hali ya soko haipendelei wao wawepo hata kidogo.

Utafiti fulani uliofanywa na Profesa Joseph Kuzilwa na Dk. Andrew Mbwambo mwaka 2004, unaonyesha mafundi wadogo wanaojishughulisha na kutengeneza viatu kwa sasa huagiza ngozi kutoka Kenya na Zambia. Haya yote yanatokea katika nchi ambayo inaongoza kwa idadi kubwa ya mifugo.

Takwimu haziko wazi kuweza kujua ni Watanzania wangapi wameingia katika umasikini kutokana na kufungwa kwa viwanda hivi vya uzalishaji wa ngozi na viatu.

Lakini katika zoezi rahisi unaweza kuhisi kuwa kufurika huku kwa viatu kutoka Asia si ukombozi ila kitanzi kwa uchumi wa Tanzania na Watanzania kwa ujumla.

Ili Tanzania iweze kwenda sambamba na lengo lake la kutaka kuona sekta ya mifugo inachangia vilivyo katika pato la taifa ni lazima ihakikishe inalinda viwanda vya ndani vinavyozalisha ngozi na pia vile vinavyotengeneza viatu.

Soko la ndani lazima lilindwe kwa maslahi ya viwanda hivi na nchi kwa ujumla.

Serikali lazima ifanye kwa vitendo suala la kuwapunguzia gharama za uzalishaji hasa umeme na kodi ili kuwajengea uwezo na huku tukiweka kodi kubwa kwa viatu toka nje.

Nia ikiwa kuvijengea uwezo viwanda vyetu vya ndani. Kama tunaweza kusamehe kodi kwa wawekezaji wakubwa wa migodi kwa zaidi ya miaka 25, nini kinatufanya tushindwe kuwapa hawa wa viwanda vya viatu likizo ya kodi!

Mazao ya sekta ya mifugo ni nyama, maziwa, ngozi na samadi. Kwa sasa nchini kuna juhudi za kuboresha machinjio ili kupata ngozi bora na ujenzi wa majosho.

Uhimizaji wa ufugaji wa kisasa miongoni mwa jamii za wafugaji. Lengo likiwa kupata mazao bora. Hakika juhudi hizi si za kubezwa hata kidogo.

Ili mazao haya yawe na manufaa kwa wafugaji wa Tanzania ni lazima viwanda vinavyosindika malighafi hizi vilindwe katika kutumia soko la ndani.

La sivyo tutakuwa watu wakupokea misaada kila siku kutoka kwa wahisani. Shime watawala tungeni sera zenye kulinda viwanda vyetu hasa katika kufaidi soko la ndani.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa barua pepe: fagdas1980@yahoo.कॉम
माकला हया क्वा हिसनी या फ्री मीडिया वामिलिकी गजेती ला म्तान्ज़निया डैम

No comments: