Saturday, November 21, 2009

Biashara bila ushirikiano ni bure

Biashara ni mzunguko wa Vita na Amani( War and Peace) lakini yenye kuhitaji kushirikiana na adui yako, Waingereza wanaiita nadharia hii kama (Coopetition), ni muunganiko wa maneno mawili ya Kiingereza Cooperation and Competition. Sina neno zuri la Kiswahili kwa tafrisi ya Coopetition, lakini nitalitumia kama lilivyo.

Coopetition kama nadharia iliibuliwa na Ray Nadal Mkurugenzi wa Novel na kuletwa katika Ulimwengu wa elimu ya biashara na kwa tafiti za Adam M. Brandenburger na Barry J Nalebuff ambao waliandika kitabu kilichoitwa ‘Co-opetition’ na kufanikiwa kuwa miongoni mwa vitabu vilivyouzwa sana duniani katika miaka ya 1997.

Coopetition ni muungano ambao mara nyingi si wa kudumu kati ya kampuni ambazo zipo katika ushindani . Mfano mzuri ni jinsi kampuni za mifumo ya kompyuta zilivyoweza kupeleka sokoni ubunifu wa JAVA uliofanywa na Sun Microsystems, kampuni za IBM, Apple na Netscape ziliungana kwa pamoja.Wapinzani wa nadharia hii huiita 'cartel' lakini katika elimu ya mbinu biashara(Business Strategy) hii ni mbinu bora kwa kueneza ubunifu wenye kukuza ushindani.

Duniani kote nadharia hii inashamiri, katika Tanzania kuna maeneo yanayotia moyo lakini kwa ujumla hali si shwari miongoni mwa wajasiriamali. Kinachonifanya niandike makala haya ni habari za hivi karibuni zinazoonesha wafanyabiashara wa Tanzania kukosa kuuza zabuni katika ‘kampuni’ kubwa ya Barrick Gold Mining ya Shinyanga.

Barrick ni kampuni kubwa inayohitaji kila aina ya bidhaaa huku ikitumia zaidi ya dola milioni 200 za kimarekani kwa mwaka, na hii ni nafasi ya wajasiriamali wetu kuweza kunufaika na uwekezaji wandani. Lakini taarifa za kampuni hii zinasema kuwa hata wale walio karibu na Barick hawanufaiki, na kampuni hii kibiashara.

Hili linachangiwa na wao kutoweza kutumia mawasiliano ya mtandao wa kompyuta wa kampuni hii kuweza kuuza bidhaa na kupata zabuni mbalimbali zinazotangazwa.Hali hii haipo kwa Barick au wafanyabishara wa Shinyanga tu, ni Tanzania nzima.

Wakati fulani iliwahi kuripotiwa kuwa kuna mjasiriamali aliyeshindwa kutimiza masharti ya mteja wake aliyekuwa anahitaji tani 'mia moja' za korosho zilizobanguliwa, hivyo akakosa kutimiza mahitaji ya mteja wake kwa vile alishindwa kushirikiana na wajasiriamali wenzake katika kuishambulia 'tenda'.Ni wazi kuwa mteja aliyevunjwa moyo hawezi kurudi tena!

Hili halikutokea kwa sababu nyingine isipokuwa ni kukosa ufahanmu wa namna ya kuweza 'kushirikiana na kushindana'.
Biashara ni ushindani na ndiyo maana tunasema ni 'vita', lakini hili halifanyi kuwa mfanyabiashara mwenzako awe adui la hasha. Maana yake ni kwamba utabuni na utajaribu kujifunza nini mwenzako anafanya huku mukishirikiana kuleta hali nzuri kwa wateja.

Ni muhimu wafanyabiashara wetu waungane ili kuhakikisha wanawafikia wadau wao kwa ukaribu zaidi na kwa ufanisi. Kuna mifano kama vile muungano wa Vodacom na Zantel, kampuni ya Zantel inatumia minara ya Vodacom, hii haimaanishi kuwa Voda watakosa wateja hapana isipokuwa itaongeza kavereji ya zantel kwa gharama nafuu kwa kampuni zote mbili katika kuhudumia minara yao.
Pia mfano mwingine ni UMOJA ATM za banki DCB, ACCESS BANK, BOA BANK, AKIBA COMMERCIAL na AZANIA BANK.Kwa ktumia msine hizi wameweza kufikisha huduma kwa wateja wao huku 'wakishindana'.
Kuna watanzania wengi waliokuwa wakiipigia chapuo nadharia hii kuingia katika biashara ya Tanzania, kama Vile Mzee Reginald Mengi alipokuwa akihimiza kampuni za simu kutumia minara ya pamoja au warusha matangazo ya Redio na Televisheni. Hili halikufanikiwa sana, kwa sababu ya 'umimi' miongoni mwa wafanyabiashara wa Tanzania.

Wajasiriamali wanashindwa kujitangaza au kufikika kwa vile hawana namna bora za kisasa ambazo mteja au msambazaji anaweza kuwafikia na kufahamu wapi kunahitajika nini?. Hili linaweza kutatuliwa kama wajasiriamali wakiwa na tovuti ya pamoja.

Tovuti ni kitu ambacho kinaweza kutumika na wajasiriamali wadogo, wakati na wakubwa kwa pamoja kwa kuweka bidhaa zao katika tovuti hiyo moja huku wakitumia gharama nafuu kuiendesha pia mteja akifahamu wapi walipo kwa kutembelea tovuti husika.

Mfano mzuri ni Google na eBay ambazo kimsingi zote wakati zinaanza zilikuwa na lengo moja tu kuwa ‘search engine’ huku kampuni zinazofanya biashara zikijiweka mbele kuwa zinakuwa zakwazwa kuonekana mara baada ya 'mtumia mtandao' kutafuta taarifa fulani kama vile ya bidhaa.

Kampuni hizi zilipoungana, sasa hivi miongoni mwa wateja inajulikana kama unataka ‘kuuza’ basi uza na eBay na kama unataka kuongeza wateja’traffic’ katika tovuti yako jiweke na Google. Lakini lililowazi ni kwamba eBay anatumia Google kuongeza traffic, huku 12 asilimia ya wateja wanapitia Google kwanza ili kufika eBay.

Si kama hawana biashara zinazofanana la hasha, eBay ana Skype,Google,ana Gmail/Talk hizi ni kampuni za mawasiliano ya simu kwa kutumia ‘Internet’. eBay ana Paypal, Google ana Forhtcomming.

Taarifa za karibuni zinaonesha wote kunufaika na mapato yao yakiimarika mara baada ya 'kushirikiana' huku 'wakishindana'.
Ukweli ni kwamba ubunifu wa ‘Google’ ni faraja ya eBay, pia ubunifu wa eBay katika biashara yake ni faraja ya Google.

Ndipo tunasema biashara ni Vita na Amani, ….Vita tena Amani ….. ni mzunguko.Coopetition ni kukubali ubunifu wa mwenzako huku nawe ukiboresha kazi yake kwa faida ya wadau. Tupia jicho pia wanamuziki wa ‘Kikongo’ ikiwa Ndombolo, kila mwanamuziki ataitumia hiyo 'staili', bila kujali nani aliianzisha,huku akiweka ‘nakshi’(ubunifu) tofauti na wakwanza, 'Kiwazenza' wote 'kiwazenza'.

Tanzania hali ni tofauti kabisa, Kapteni John Komba amekuja na ‘Achimenengule’ ngoma ya wayao wa Masasi ni mwanamuziki mmoja tu amejaribu kuitumia!

Ni muhimu wafanyabiashara wetu wakajitahidi kufikiria kuungana na kushindana kuliko kukalia ushindani bila ‘kushirikiana’. Ni wazi kuwa ushirikiano ni nyumba ya ubunifu.

Hakuna 'adui' wa 'kudumu' wala 'rafiki' wa kudumu katika biashara, ila cha msingi ni kuimarisha ushirikiano kwa faida ya wadau wote. Na si kuikalia 'tenda' ambayo unajua hauwezi kuitekeleza bila ushirikiano. Wajasiriamali yawapasa kushirikiana ili kusonga mbele, ushindani si vita tu, bali amani pia kwa maana ya kwamba utaweza kunufaika na ubunifu wa adui yako pia.

1 comment:

Unknown said...

kaka umenena kweli,but vp ushirikiano wa wafanyabishara wetu na wafanyabishara wa kenya na uganda kwenye hii common market iliyopitshwa juzi juzi mbona haujazungumzia?"maana mie naona bado wafanyabishara wetu wengi ni wachanga so kuwasukumia kwenye fee marketnaona kama tunawadidimiza vile,niweke sawa kaka kwa points zilizoshiba za kimarket