Friday, November 6, 2009

Stakabadhi ghalani inahitaji ubunifu zaidi na si kusambaza 'woga'(SEHEMU YA PILI)

Soko la mazao la Tanzania tangu kuingia kwa kwa dhana ya soko huria vilio vya wakulima vimesikika kila kona. Hili halina nafasi katika makala haya kwani tunaamini mengi yamezungumzwa. Ila lililowazi ni kwamba tumeonesha jinsi wanunuzi wa korosho walivyokaidi agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika sehemu ya kwanza ya makala haya.
Tulishaonesha msimamo wetu katika makala yetu kuwa hatukubaliani na mawazo ya waheshimiwa wabunge kufuta stakabadhi ghalani pamoja na changamoto za sasa zilizopo katika zao la korosho.
Hebu tutupie jicho kidogo katika hoja zao mbili ambazo, mosi ni kuwa stakabadhi ghalani ni mfumo wakinyoyaji na pili unawatenaa wakulima wadogo.
Tuanze kwa kubainisha wazi kuwa si kweli kuwa mfumo wa stakabadhi ghalani ni kuwa wakinyonyaji. Isipokuwa ni mfumo ambao kinadharia unaleta uhuru wa kweli kwa wakulima wa nchi hii. Wakulima wa korosho wameshuhudia kulipwa katika mikupuo miwili na maeneo mengine mikupuo mitatu zaidi ya bei ya soko.
Wale waliouza korosho katika msimu wa mwaka jana kuna waliouza kwa kilo 650/= walichukua malipo yao na baadaye walilipwa mafao yao ya nyongeza ambayo baada ya kuuza korosho ilifikia kilo shilingi 800. Hivyo kufanya nyongeza ya zaidi ya shilingi mia kwa kilo.
Katika hali kama hii mkulima amenyonywa nini! Na liliwalowazi wale waliouza katika mtindo wa stakabadi ghalani walipata nafasi ya kujiwekea akiba kwa ajili ya pembejeo, lazima ieleweke watanzania walio wengi na hasa walio vijijini hawafaidi huduma za kibenki, hivyo kupitia stakabadhi ghalani wakulima wanaanza kuhifadhi kipato chao, kama vile mwenye akaunti, kwani hii ni ‘negotiable instrument’ inaweza kuthaminishwa. Hapa tunahitaji ubunifu katika sheria madhubuti katika kuhakikisha benki inapokea stakabadhi kama ‘inventory credit’.
Mfumo huu umeleta neema si katika korsho tu, hata katika kahawa , katika tafiti ya Gideon E. Onumah na Fedelis Temu ya mwaka 2005 katika kahawa na pamba iliyoitwa ‘Reducing Marketing Constraints and Enhancing Producer Income Through Warehouse System’ ilibaini kunufaika kwa wakulima wa Tarakea, Moshi kwa kipato kizuri kwa wanachama wa ushirika wa Tarakea ambao waliuza kahawa kwa kilo 1800/= tofauti na wenzao waliouza kwa mfumo wa soko huria wa kwa kilo 1250/=.
Ushirika hauchagui hivyo hoja ya kuwa mfumo huu unamtenga mkulima mdogo si sahihi. Ila ili mfumo huu usonge mbele unahitaji ushirika imara ambao umeundwa na wakulima wenyewe kwa ridhaa yao.
Mifano inaewza kuwa mingi kama vile IFAD inavyoshuhudia wakulima wa mahindi katika Karatu wanavyonufaika na mpango huu, huku wakiimarisha maisha yao. Mahindi yanauzwa 13,000/= kwa gunia wakati wa mavuno, lakini sasa wakulima wanaweka ghalani, wanuza hadi gunia la kilo mia 26,000/=.
Na lililowazi ni kwamba wengi wa kulima hawa ni wadogo walioungana kupitia ushirika wao kwa hiyari. Na wala hakuna tishio la kumnyonya mkulima mdogo. Sasa hili la kuwa stakabadhi ghalani ni tishio linatoka wapi?
Wataalmu wa biashara ya mazao wanabainisha kuwa mara zote adui mkubwa wa stakabadhi ghalani ni kilimo cha mikataba (Contract farming). Tanzania ina kampuni chache zinazofanya kilimo cha mikataba, kama vile Starbuck tena wapo katika kahawa wilayani Mbinga.
Inawezekana katika nchi yetu kilimo hiki kisiwe tishio kwa sasa ila yatupasa kuangalia namna yakufanya vyote viende kwa pamoja kwani vinamanufaa kwa wakulima wan nchi hii.
Pili upinzani wa stakabadhi ghalani unasababishwa na ‘bush buyers’ na kampuni za kinyonyaji zisizotaka kumuona mkulima anainuka. Hili ndilo lipo sana Tanzania.
Walanguzi wa korosho wapo wengi sana, wanakaa mjini msimu( Mwezi wa Kumi) ukifika kila mmoja na gunia la dagaa wa Mwanza au wa kigoma, chumvi na nguo za kichina au mitumba hujifanya wanauza kwa kubadirisha kwa korosho.
Hawa wananunua kwa kubadilishana ‘barter trade’. Ubaya wa biashara hii hutumia ‘kangomba’ (Ni kopo lenye kuingia kilo mbili na nusu) kubadilisha na mtumba au dagaa wa Mwanza wengi wame neemeka kupitia njia hii siyo rasimi.
Sasa hawa kwa vile ni watu waliokatiwa utamu bila jasho wanaona mwishowao unahatarishwa kwani sasa wakulima wamekombolewa, ndiyo wanaleta vitisho vya kuhamasiha kunyima kura wabunge na vurugu zote zile tulizo ziona katika makala haya sehemu ya kwanza chanzo ni hawa wanununzi wa ‘kangomba’.
Pia kampuni hizi za kihindi za ‘mfukoni’ zinamkono katika kuhimiza kuonekana kwa stakabadhi ghalani si mali kitu. Hizi kampuni zinafanya kazi kwa ‘ujanja ujanja’ Wengi wao kiukweli hawana mtaji, ila kinachotokea ni kwamba wao wanakubali kwenda vijijini na kujifanya wananunuzi kwa walau tofauti ya shilingi 20-100, ambayo wao huchukua kama cha juu. Hii biashara ya udalali imewanufaisha wengi hasa Mtwara Mjini.
Merehemu Profesa Seith Chachage anawaita makuadi wa soko huria. Na hawa nao hufanya kazi kupita mtindo huu wa soko huria kwa kusambaza vitisho.
Makuwadi hawa wanavyofanya ni unyonyaji ambao hauuvumiliki kama unaipenda nchi yako, kuna rafiki zangu walifanya kazi katika kampuni za korosho simulizi zao ni kwamba mkulima anapofika kuna madalali ambao wao wanijifanya ‘kumjua’ tajiri na bila wao ‘hauuzi’, sasa kwa vile mkulima ametoka Kitangari au Nambali hamjui tajiri wa kihindi anamkabidhi huyo ‘dalali’ kazi ya kufuatilia mauzo ya korosho zake.
Anazunguka anakuja na vijana ambao’ wanapiga’ bambo kutathimini ubora wa korosho kisha hudai kuwa ubora uko chini, hivyo hawawezi kununua.Hiki ni kitisho cha wazi. Mkulima amekodi gari na mjini siyo kwao, ataanza ‘kuweweseka’ tayari amekiwsha!
Wanauza korosho kwa bei kubwa na watachukua wao cha juu, kisha mkulima ataambulia maumivu, hawana huruma hata kidogo. Stakabadhi ghalani imewaondoa ndiyo hao ‘wanaugulia’ maumivu kwa kuleta hoja chakavu na hawa nao wananguvu ya kisiasa kwani wengi wao ni wapigaji wa ‘mdomo’ hasa vijiweni, basi wabunge wanajifanya kuleta hoja kuwa mfumo mbovu kumbe kutaka masilahi ‘uchwara’ yasiyo na tija, kwa walio wengi.
Changamoto ya kutolipa kwa wakati tumeshaona jitihada za serikali ilivyofuta madeni ya vyama vya ushirika ili viweze kukopesheka.Hili lilifanyika kwa baadhi ya vyama vya ushirika katika mkoa wa Mtwara na viliweza kupata mikopo kutoka benki ya CRDB. Ni wazi kuwa huu ni uamuzi mgumu na wa hali ya juu, ila yatupasa kwenda zaidi ya hapa.
Yatupasa kuhakikisha vyama vinakuwa na wataalmu wa kutosha, kwani katika ripoti ya mwaka 1967 ya Ushirika (Presidential Inquiry on Cooperative) mkoa wa Mtwara ulioneka kukosa wataalamu wa ushirika na masuala ya fedha. Ingawa muda ni mrefu lakini inawezekana kuwa tatizo hili mpaka leo lipo.
Lakini hili haliwezi kutufanya turudi nyuma. Wabunge lazima wabuni mbinu bora za kuhahakisha viongozi wanapata elimu ya kuweza kuendeleza ushirika katika maeneo yao
Pamoja na faida zake zote stakabadhi ghalani na hasa kwa Tanzania ina changamoto ambazo kimsingi tunapaswa kuzitafutia dawa na kitu kikubwa ni ubunifu.
Changamoto kubwa ni uhifadhi wa mazao, hapa tunazungumzia maghala yetu?Je yana bima? Ikitokea ghala limeshika moto, hatima ya mkulima wetu ikoje?
Kuhifadhi (Storage) ni taaluma, je tunawataalamu na mbinu za kutosha katika uhifadhi wa kisasa?
Nguvu ya stakabadhi tunayo mpatia mkulima wetu inakubalika katika taasisi zetu za kifedha kama ‘negotiable instruments’? Kama hapana tunaboreshaje?Kama ndiyo je uhalali wake ukoje kifedha?Sheria zetu zinasemaje kuhusu inventory credit?
Hatari nyingine ni kughushi (fraud) mara zote stakabadhi ghalani inaambatana na tatizo hili.
Ripoti moja ya Shirika la Umoja la Mataifa linaloshughulika na Chakula (FAO) inasema kama kilimo kinahitaji kuinua maisha na maendeleo kwa walio wengi basi mfumo imara wa mikopo unahitajika, na stakabadhi ghalani ni suluhu ya kudumu kwa wakulima kupata mikopo.
Tukijipanga na kuongeza ubunifu tunaweza.

No comments: