Sunday, November 29, 2009

Kampuni za Tanzania zinahitaji kurudisha sehemu ya faida kwa miradi endelevu

Biashara ulimwenguni kote imekuwa ikipitia katika vipindi tofauti vya kinadharia juu ya masilahi ya wateja. Katika nchi za Magharibi kuna changamoto ya ulinganisho wa faida na manufaa wanayopata jamii husika toka kwa kampuni zinazofanya biashara katika eneo husika.
Wateja hawataki tena kampuni ambazo ni ‘mumiani’ kampuni zinazovuna faida tu bila kujali masilahi ya jamii husika. Tanzania wateja hawana nguvu kama nchi za Ulaya na Marekani ambako kuna vyama imara vya kutetea masilahi ya walaji. Na hili ndilo linafanya kampuni zetu kubweteka.
Hili linafanya kampuni za kitanzania zione ‘wadau’ na hasa walaji ni watu wa kukamuliwa tu, na wala wasiohitaji marejesho ya faida ya kampuni. Ingawa suala la marejesho ya faida kwa jamii ni lenye kuhitjai zaidi muongozo wa bodi ya kurugenzi ya kamapuni husika.Lakini kwa Tanzania kuna matukio yanatufanya tujiulize hivi hizi kampuni zetu zinaamini kweli katika kile inachokisema au ni masihara?
Kuna kampuni ambazo zinajigamba kuwa zinarejesha faida iliyopata kwa wateja na hasa kupita maofisa matukio wao. Na hili limekuwa likitokea hasa wakati wa kutoa zawadi kwa washindi wa ‘kamali’. Sasa hivi katika Tanzania kila kampuni kubwa imejikita katika kuchezesha ‘kamali’ kwa kivuli cha ‘promotion’ za kujishindia zawadi.
Na ndiko huko wanakojificha wakijidai wanarudisha faida kwa jamii! Si kweli kwani kimsingi wachezaji wamechangia wao wenyewe na kampuni nyingi zinakuwa zimejinyakulia faida nono kabla ya ‘draw’ na kama haijavutia wachezaji tumeshuhudia zikisogezwa mbele.Kama kweli ‘promotion’ kwa nini wasogeze mbele draw?
Kuna kampuni moja ya simu ambayo ilichezesha ‘kamali’ yake baada ya kujikusanyia milioni 100 ya faida! Huku wateja wakiambuali vijizawadi vya muda wa maongezi wa kwa mtindo wa kuchangiana wao wenyewe.
Hii si ‘promotion’ kama vile wao wanavyotaka tuamini, kwani sales promotion ni faida kwa mteja kwa kupata huduma au bidhaa kwa bure au chini ya bei ya soko kwa kipindi maalumu.
Isieleweke kuwa hakuna kampuni ambazo hazifanyi na wala hazina juhudi lakini kwa faida zinazochuma mara zote imekuwa hailingani na kile wanachotoa na zimekuwa zile zile kila mara kuna kampuni zingine zinastaajabisha kabisa. Ukizialika katika michango ya ujenzi wa shule utawaona wanatoa mifuko ya sementi tani moja. Huku taarifa za TRA zinasema kampuni imepata faida ya zaidi ya bilioni 20 tena baada ya kulipa kodi!
Ila mara nyingi kampuni zetu zimejikita katika miradi ambayo si yakudumu, na wala haina faida ya muda mrefu kwa jamii husika. Mara nyingi imejikita kufuturisha watanzania wakati wa ramadhani, huku kampuni hizo zikijipatia faida kubwa na wakatia mwingine kutoa zawadi wakati wa Krismasi katika vituo vya kulelea yatima kwa magunia ya mchele na mafuta ya kupikia.
iliandaa harambeee hii miaka miwieli
Kimsingi kamapuni zetu zinahitaji kwenda zaidi ya hapo.Tanzania ya leo inamatatizo mengi na tukiunganisha nguvu zetu tunaweza kufika mbali na si kufanya mambo kwa staili ya ‘kiini’ macho.
Wakati fulani iliwahi kuripotiwa na vyombo vya habari kuwa Waziri Mkuu aliyejiuzuru Mheshimiwa Edward Lowasa aliwahi kukataa michango ya kampuni fulani katika harambee ya kuchangia bweni la wasichana wa Chuo Kikuu Mzumbe. Mzumbe inahitaji kufikia lengo la asilimia hamsini kwa hamsini ya udahili wa wanawake na wanaume.
Hivyo iliandaa harambee hii miaka miwili iliyopita Jijini Dar-Es-Salaaam ,kichekesho ni kwamba kampuni inapata faida ya bilioni 26 baada ya kulipa kodi inatoa machango wa milioni tano kwa mradi wa kuwezesha wanawake wengi kupata elimu ya juu!
Hii ndio hali ya kampuni za Tanzania ni kupenda kutumia nguvu kazi pasi hata kurejesha wala kutolea jasho. Nyingi ya hizi kampuni ndizo waajiri wakubwa lakini hawaweki nguvu hata kidogo katika kuboresha hali ya elimu nchini.
Hii haimaanishi hakuna kampuni ambazo hazijielekezi katika kuboresha hali za watanzania katika miradi ‘endelevu’ zipo kama vile Zain ambayo hutoa ufadhili kwa wanafunzi wa shahada ya kwanza katika fani mbalimbali nchini. Lakini juhudi hizi ni kwa kampuni chache huku zingine wakiwa kama watazamaji au hawajui matatizo ya watanzania. Ila katika kudhamini ‘matamasha’ huko utawaona!
Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mzee Benjamin William Mkapa akiwa Uganda katika mahafali ya Chuo Kikuu Makerere ambako alitunukiwa PhD ya heshima ya Sheria amenukuriwa na na vyombo vya habari akiweka bayana kuwa nchi za Ulaya haziweki nguvu katika kufadhili elimu ya juu badala yake zipo katika elimu ya msingi, na hakuna taifa linatakalo ondokana na umasikini kwa kuwa na watu wenye elimu ya msingi bila wa na wataalamu wa elimu ya juu.
Hii ni wazi, upungufu wa udhamini wa elimu ya juu nchini unaweza kupunguzwa na udhamini wa kampuni za ndani kama tukijipanga.
Yatupasa kuweka nguvu katika miradi endelevu kama elimu ya juu kwa kutoa ‘udhamini ‘ kwa wahadhiri pia. Hili linawezekana hebu tuangalie kwa Uchache tuone namana kampuni zetu zinavyotumia pesa katika matangazo.
Mwaka 1997 kampuni za Tanzania zilikuwa zinatumia 1.1 asilimia ya pato la Taifa kwa ajili ya matangazo. Kampuni kumi bora za Tanzania katika matumizi kwa ajili ya matangazo zilitumia bilioni 14.2(2005), 18.9 (2006) na 25.2(2007) ( Advertising Age, Desemba 8, 2007).
Matumizi kwa matangazo ni kwa kampuni zile tu ambazo zimeruhusiwa kufanya matangazo katika Televisheni na Radio acha kampuni kubwa kama TCC watengenezaji wa sigara ambao sheria inawabana kutumia rediao na TV wao wanatumia mabango na udhamini wa matamasha.
Matumizi haya kwa ajili ya matangazo kwa makampuni kumi ni wazi kuwa kampuni zetu zinapata faida kubwa, lakini hazirejeshi hata chembe ndogo kwa jamii ya kitanzania kwa uwiano unaolingana na hasa miradi endelevu.
Ulinganisho haupo katika kurudisha faida kwa miradi ya jamii, na badala yake wakitoa mchele utaona jinsi wanavyojitangaza katika redio na televisheni! Si sawa kwani matangazo hayafanani na faida wanayopata au kurusha kipindi maalum.
Kama nchi tumekosa cha kuzifanya kampuni hizi na ndiyo maana zinapata faida kubwa bila hata kujali sehemu ya jamii. Tuangalie mfano mdogo tu ambao unaonesha jinsi kampuni zetu zilivyolala katika kupeleka faida kwa jamii husika.
Ukipita katika barabara ya Alli Hassan Mwinyi utaona abiria wapo juani pembeni kuna Ofisi za kampuni kubwa na zenye kuheshimika kwa jamii ya kitanzania. Hiki ni kituoa cha daladala kampuni zimeshindwa walau kuweka kibanda cha abiria kujisitiri kwa jua na mvua.
Sasa hivi Krismas inakuja utaoana kampuni zetu ndogo na kubwa zinavyoshindana kutoa zawadi za mbuzi na mchele kwa mafuta ya kupikia. Kimsingi hatupingi zawadi hizi, lakini matatizo ya watoto hawa si kula ya siku moja au pilau, wengi wao wanahitaji elimu jitokezeni mulipie karo za watoto hawa na si kuvizia ‘picha’ Mifano ipo mingi kampuni kubwa na zenye kuheshimika mbele ya ofisi zao abiria wanakaa juani na wananyeshewa mvua wakati wa masika bila hata kujali sehemu hii ya jamii na wakati mwingine hawa na wateja wao.
Hii ni mifano midogo lakini inaonesha jinsi kampuni zetu zinavyoona kurudisha chumo lake kwa jamii ni ngumu.
Tanzania ina kabiliwa na changamoto ya kukosa fedha kwa ajili ya tafiti za kitaalamu kwa maendeleo ya nchi. Serikali ndiyo inasema labda itajaribu kuweka fedha zake kwa walau asilimia 0.1 ya bajaeti kwa ajili ya tafiti kwa miaka ijayo ni suala la kusubiri na kuona .
Ila hili ni eneo lingine kampuni zetu zimekaa kimya wala haziinui mkono wala ‘mdomo’ ili kuonesha njia lakini ‘show’ za urembo wanamwaga fedha huku wakishindana kutoa zawadi. Matamasha ya ‘bongo fleva’ wanapigana vikumbo ili waonekane kuwa ndiyo vinara.
Wanashindana kuleta wanamuziki wa magharibi, ni wazi kuwa burudani ni muhimu kwa jamii lakini tutanachekesha kwani mbio zetu kwa mambo ya kupita ni za kasi mno kuliko mambo ya msingi ambayo tumeyapa kisogo.Kampuni inatumia bilioni 5.1 kwa matangazo kwa mwaka ni wazi kuwa inaweza hata kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kutoa fedha kwa ajili ya tafiti za kitaalamu zitakazoweza kuinua taifa na kampauni husika pia.
Hakuna taifa lilillopiga hatua duniani bila tafiti na kikubwa ni kwamba hzio tafiti chanzo chake ufadhili kikiwa ni cha ‘ndani’. Na tafiti hizi zikifanywa kwa mazingira ya Tanzania ni wazi kuwa zitapelekea mafanikio kwa kampuni zetu za ndani katika kutumia tafiti hizi kwa urahisi. Lakini hakuna kitu kama hicho badala yake ni miradi ya muda mfupi ndiyo inayopendwa na kushabikiwa na kampuni zetu.
Tafiti zinazofanywa na vyuo vya Magharibi nyingi zinagharimiwa na kampuni zao kwa kuweka pesa katika vyuo na wao wananufaika na matokeo ya tafiti. Huku ndiyo kurudisha ‘chumo’ kwa jamii na si kuchezesha ‘kamali’ alafu munajigamba kuwa munarudisha chumo kwa jamii.
Kampuni zetu zinapata faida ‘nono’ lakini mgao kwa jamii bado ni mdogo yatupasa kubadilika, kwani biashara ni kujali jamii husika kwa miradi endelevu na ‘ujanja ujanja’ na maneno mengi yasiyo na tija na kuhimiza ‘press coverage’ ili muonekane munatoa.
Yatupasa kama nchi kufahamu kuwa tunahitaji kwenda hatua za mbele zaidi ili kutatua matatizo yetu na faida inayochumwa na kamapuni zetu ikitumika vizuri inaweza kuleta mabadilko kwa maisha wa watanzania walio wengi, na si kufadhili ‘burudani’ tu.

No comments: