Sunday, February 14, 2010

Elimu ya biashara na anguko la uchumi wa Ulimwengu

Anguko la Uchumi wa Ulimwengu limeleta madhara makubwa lakini lililowazi ni juu ya UBORA na UMAKINI kwa ujuzi unaotolewa katika shule za biashara DUNIANI.Katika Marekani swali lilikuwa juu ya majaaliwa ya elimu ya MBA (Masters of Business Administration). Katika Afrika Kusini kuna waliojiuliza kwa nini waafrika waende kusoma katika nchi ambazo zimeshindwa kuzalisha wasomi walioweza kulinda ‘msusuko’ huu.Yaani katika vyuo vya Marekani na Ulaya.
Pamoja na madai hayo bado MBA imekuwa ni elimu pendwa kwa sasa, hasa nchini Marekani kwani inakadiriwa watu wengi waliokosa kazi walirudi madarasani na wengi walirudi kusoma hizo elimu za biashara.Kampuni kubwa za kimarekani zilizoanguka zinaongozwa na wataalamu wa biashara kutoka vyuo bora kama vile Harvard, Stanford, MIT na kadhalika.
Makala haya haina nia ya kujaribu kusimulia nini kilichosababisha ‘msukosuko’ huu mkubwa wa kiuchumi duniani ulioanzia Marekani mwishoni mmwa 2007, ila tutajaribu kuangalia majaaliwa ya sekta ya Elimu ya Biashara katika Tanzania na nini tunaweza kujifunza.
Rais Barack Obama alipoingia madarakani aliendeleza mpango wa kunusuru taasisi za fedha na bima mpango ambao uliasisiwa na rais aliyemtangulia George Walker Bush Jr. Lakini mpango huu uligubikwa na utata wa matumizi yasiyorasmi ya malipo ya posho za maofisa wa ngazi za juu.
AIG (American Insurances Group), ilitumia dola milioni 165 kulipa posho ya maofisa wake. Hali hii ilifanya White House kuingilia kati na kuweka wazi kuwa haipo tayari kuona ‘bailout’ ikitumika kujilipa posho na malipo mengine manono ya maofisa wakuu wa benki na hasa katika kipindi hiki cha kupambana na anguko la Uchumi wa Ulimwengu.
Hili linaashiria kutokuwepo kwa umakini wa hali ya juu ambao unalalamikiwa na watu wengi duniani miongoni mwa watendaji wa sekta za fedha.Na hasa lililowazi ni hili la kukosekana kwa maadili, watu wachache wajilipe wakale ‘starehe’ ufukweni au kidogo kilichopo kitumike kwa ajili ya kulinda masilahi ya wengi!
Katika Marekani kuna walioenda mbali zaidi kwa kuikebehi elimu ya MBA kama ‘Masters of Disaster’. Ni wazi kuwa anguko la uchumi wa ulimwengu ni changamoto kwa elimu ya MBA na hasa shule za biashara duniani.
Kwa mwaka nchini Marekani pekee wahitimu wanaokadiriwa kufikia 100,000 uhitimu katika ’specialization’ mbalimbali za elimu ya MBA, huku asilimia 40 wakiajiriwa katika sekta ya fedha. Na sekta hii inasadikiwa ndiyo ‘chokochoko’ ya mdororo wa Uchumi ulikoanzia, pale maofisa walipokuwa wakikimbizana kutoa mikopo ili kupata ‘bonuses’ bila kujali uwezo wa mlipaji. Mikopo iliwafikia, NINJA (No Investment, No Job, No Asset) Hapo ndipo mtafutano ulipoanza, huku wakiwa na lundo kubwa la kadi wakitumia kwa mtindo wa ‘credit card’, hili lilipelekea ‘mkusanyiko’ mwingine wa madeni usiolipika kutoka sekta nyingine.
Pia kurunzi lilimulika ule utamaduni maarufu wa kuandaa mameneja, unaotambulika kama ‘Harvard Culture’. Msusuko huu wa uchumi unafanya kutimia kwa ubashiri wa Profesa Henry Mintzberg, mwanazuoni wa Masomo ya Uongozi, katika Chuo Kikuu cha McGill, Canada.
Profesa Mintzberg alipinga ‘utamaduni wa Harvard’ wa kumuandaa menejea darasani na aliweka wazi msimamo wake kuwa meneja siyo MBA, na kimsingi meneja bora anapaswa kunolewa huku akiwa anajifunza toka kwa waliomtangulia na situ kukabidhiwa wadhifa kwa msingi wa cheti.
Pamoja na yote hayo Ulimwengu umeendelea kushuhudia shule za Biashara na hasa elimu ya MBA ikipata wanafunzi wengi kuliko nafasi za udahili kama nilivyokwisha sema hapo awali. Ni wazi kuwa MBA inapendwa, na sokoni bado ipo juu.
Msususko huu wa kiuchumi umeshuhudia wasomi wa Harvard wakija na nadharia ya kuweka kiapo (oath) kwa wasomi wa MBA kuapa kukubali kulinda maadili ya biashara. Tunachojifunza hapa ni kwamba Ulimwengu wote sasa umetambua kuwa hangaiko hili la Uchumi limetokana na kukosekana kwa maadili miongoni mwa wafanyakazi wa taasisi za fedha. Hili likafanya wawe wasiri ingawa taasisi zao zilikuwa zinaanguka.Ndiyo hayo ya Ponzi Scheme!
Tanzania si kisiwa, nayo elimu ya MBA inashamiri kila kukicha vyuo vikuu vingi kwa sasa vinatoa elimu ya MBA.Huku,Mzumbe University mwaka jana ikiwa na wahitimu wanaokadiriwa kufikia 400 wakihitimu katika ‘Campus’ ya Elimu ya Biashara ya Dar-es-Salaam, pekee. Huu ni mwanzo mwema.
Lakini tunapaswa kujiuliza kama tunachokifanya darasani kuwaandaa viongozi wa biashara katika misingi ya kulinda ‘masilahi ya taifa’ au bado tunawafundisha wanafunzi ‘michakato’ ya biashara. Wanazuoni Leonidou na Kaleka wanaweka wazi kuwa elimu ya biashara kwa kiasi kikukwa imeweka msukumo katika, mbinu(strategy) mifumo na michakato badala ya ‘kufinyanga’ watu (1998)
Tanzania ya leo imekumbwa na rushwa katika sekta ya biashara huku ushindi wa rushwa kwa kupata ‘tenda’ ndiyo yamekuwa mambo ya kawaida.Sasa tunarudishiwa zaidi ya bilioni 30 za kitanzania kutokana na kashfa ya rada, Mheshimiwa Membe anaita chenji yetu!
Lakini hii ni changamoto kwa shule ya biashara, yatupasa kuandaa wasomi watakao ona kuwa kujihusisha na rushwa na kutojali masilahi ya watu wengi si jambo jema. Hapa ndipo suala la elimu ya maadili ya biashara linapoibuka.
Katika makala ya kisomi, ‘Challenges faced by business schools within newly founded catholic universities: the case of Tanzania, Mtawa (Sister) Dokta Helen A Bandiho, pia ni Mkuuwa wa Kitivo cha Biashara cha SAUT,Mwanza; anataja kuwa jukumu la shule za biashara ni kujenga jamii yenye viongozi wa biashara waliotayari kulinda masilahi ya taifa kwa kupigania masilahi ya wengi.
Akionya juu ya rushwa, ‘usiri’, matumizi mabaya ya mali ya umma,upendeleo katika zabuni havina mwisho mwema kwa shule za biashara.Hii ndiyo changamoto kubwa kwa shule za biashara kwa sasa katika Tanzania na ulimwengu kwa ujumla. Katika Tanzania ya leo huwezi kufanikiwa bila kuwa ‘network’ isiyorasmi katika biashara!
Network ya aina hii haina mwisho mwema kwani wasio na sifa ndiyo wanapata kazi na tenda, huku walio na sifa wakikata tamaa.Mara zote huwa ni majuto ambayo makala haya ikiyaorodhesha yatajaa kurasa. Mbaya zaidi wale waliotayari kuongeza bei ‘quote’ ndiyo wanaonekana kuwa wajanja, huku nchi ikiteketea. Hela zinazojenga vyumba vya madara kumi shule binafsi shule ya serikali ni vyumba viwili tu na haviishi! Hii ni hatari.
Tunahitaji kuhimarisha shule za biashara kwa kufundisha maadili ya biashara kwa kuwaandaa wanafunzi kupambana na rushwa, huku wakiwa tayari kuchukua madaraka ya kutoa maamuzi. Ingawa itaweza kutolewa hoja kuwa maadili ni suala la mtu binafsi na alivyofunzwa akiwa na familia yake.Hii ni sawa.
Lakini bado shule ya biashara ina nafasi kubwa katika kubadilisha kwa ‘kufinyanga’ wasomi wenye maadili na waliotayari kutetea masilahi ya taifa katika kila nafasi ya uongozi watakayokabidhiwa.
Kwa sasa katika Tanzania vyuo vingi vinavyotoa elimu ya biashara havina elimu ya maadili (business ethics) isipokuwa ni IFM tu waliokuwa na kozi hiyo tena kwa Shahada ya MB-International Business wanayoitoa kwa pamoja na Taasisi ya Biashara za Nje ya India.
Katika vyuo vingi kuna waliobuni Business Ethic and Law kama kozi, lakini lazima ifahamike kuwa ‘business ethics’ siyo sheria, ila ni elimu ya kumpa mwanafunzi uwezo wa kung’amua mema na mabaya, ingawa sheria inaweza ikawa inakupa nguvu.
Kwa mfano hakuna sheria itakayo kubana ukiwa unataka kufungua bar au kioski cha kitimoto karibu na msikiti. Lakini kimaadili hili si sawa. Ndivyo hivyo tunaona mifano mingi ambayo kama watoa maamuzi katika sekta ya biashara wangeweza kupata msasa kuhusu elimu ya maadili wasingaliweza kufikia maamuzi wanayoyapinga leo.
Msusuko wa Ulimwengu umefanya Harvard kufikiria kuweka kiapo kwa wasomi,wa biashara, basi yatupasa nasi kufikiria kufundisha maadili ya biashara, kwani mashaka yetu ya ubadhirifu wa mali ya umma, rushwa, upendeleo na mengine ya hovyo yanachangiwa na kukosa maadili.
MUNGU IBARIKI TANZANIA,
MUNGU IBARIKI AFRIKA.

No comments: