Sunday, February 7, 2010

Tunachojifunza kutokana kupanda kwa bei ya mchele duniani

Mchele unaozalishwa kwa asilimia 90 katika bara la Asia, ni asilimia saba tu huingia katika biashara ya Ulimwengu. Ulimwengu bado unakumbuka hofu ya kitisho cha chakula ilivyopandisha bidhaa hii, huku ikifanya baadhi ya nchi kama Philippines kukosa shehena aliyoihitaji pamoja na dau kubwa la dola 680 kwa tani wauzaji na ‘waroho’ wa pesa walikataa kuiuzia tani 500,000 alizohitaji.
Tangu Januari 2008 biashara ya Ulimwengu ya chakula imekumbwa na msusuko wa kupanda kwa bei, huku mchele ambao ni chakula cha watu wengi walio masikini katika Asia ukipanda maradufu.Hali iliyofanya kuleta hofu zaidi miongoini mwa wa jamii ya kimataifa.
Kwa sasa bei ya mchele inaonekana kushuka kwa mujibu wa takwimu za FAO. Lakini Idara ya chakula ya Marekani inaonya kuwa hali bado ni ‘tete’ hasa kwa mchele na bei yake kutengemaa katika siku za karibuni.
Tanzania si muagizaji mkubwa wa mchele katika Afrika, lakini umuhimu wa zao la mchele kutoka Asia hakuna asiyeujua katika nchi hii. Mchele umekuwa siyo chakula kikuu hivyo kufanya mara zote iwe ni kimbilio letu wakati wa njaa.Mchele kutoka Thailand na Vietnam huwa ndiyo chakula mkombozi wetu wakati wa njaa.Kuna aina maarufu kama kitumbo na V.I.P ni aina ya Indica, wenye thamani ndogo katika soko la dunia.
Bei ya mchele ya ulimwengu inaonakana kuwa tata, kwa vile kuna madai kuwa India imeanza kupita kupita kwa nchi wazalishaji huku ikitangaza kuhitaji shehena ya mchele. Hii ni dalili ya wazi kuwa kitisho hiki cha India kuna jambo laja.
Ripoti ya FAO, Food Outlook, 2009, inabainisha wazi kuwa, India ipo sokoni ikiwa inavizia maeneo ya kununua mchele. Nia ikiwa kuongeza shehena yake ya mchele kwa tani milioni 9 zaidi. Ingawa haikuwa na uhakika juu ya madai ya kupipita kwa India katika kutafuta wauzaji wa mchele.Biashara ya Ulimwengu ya mchele inakadiriwa kupanda kwa tani 800,000 zaidi ya mwaka jana.
Wadadisi wa biashara ya mchele duniani wanabashiri wazi kuwa mahitaji ya ulaji ya mchele yanakadiriwa kupungua katika Asia.Lakini wanaonya kuwa kupungua kwa ulaji kwa jamii za Uchina, Thailand, India, Korea na Japan haimaanishi kuwa mchele utapungua bei kwa vile umekosa walaji.
Ila kitakachotokea ni kwamba uzalishaji wa mchele utapungua, kutokana na ukweli kuwa mashamba mengi yananyakuliwa kwa ajili ya ujenzi wa makazi kutokana na ukuaji wa miji mingi katika Asia.
Ukuaji wa miji unakadiriwa pia kuchochea ujenzi wa viwanda na barabara hali ambayo shirika la Utafiti wa mchele (IRI) lenye makazi yake Phillipines; linaelezea kuwa itapunguza ardhi kwa kilimo cha mpunga.
Pia kuna taarifa kuwa kuimarika kwa kipato cha familia kutapunguza walaji wa mchele, hali inayokadiriwa kuchangiwa mno na mafanikio ya uzazi wa mpango katika nchi nyingi za Asia ya Kusini na hasa Uchina.
Ukuaji huu wa chumo la familia unapelekea familia nyingi kubadili iana ya chakula, basi hili linajionesha wazi na kurufurika kwa maduka ya makubwa ‘supermarkets’ kutoka magharibi katika nchi hizi. Maduka kama Tesco, Asda, Mark Spencer Spencer na WalMart, wauzaji wa ‘fast food’ McDonalds, Kentucky Fried Chicken, StarBuck na kadhalika. Jamii ya Asia ya leo si walaji mchele tena, bali hupenda kula zaidi vyakula vya 'magharibi’
Mabadiliko ya chakula yanapeleka mbinyo tena katika ardhi iliyokuwa inatumika kulima mchele, sasa hutumika kulima mboga mboga , matunda, kukidhi mahitaji na mabadiliko ya jamii za Asia.
Mwenendo huu wa matumizi ya mchele katika Asia yanatufanya tujiulize juu ya siku za baadaye kwa Afrika ambayo hutumia Asia kama kapu lake la chakula wakati wa njaa?
Katika Afrika waagizaji wakubwa wa mchele ni Nigeria ambayo huagiza asilimia 6 na Senegal asilimia 4 ya mchele unaoingia katika soko la Ulimwengu, huku maeneo mengi yakiwa si walaji wakubwa wa mchele hadi ukame au kitisho cha njaa ndipo hukimbilia katika masoko ya Asia.
Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo si walaji wakubwa wa mchele, chakula kikuu ni mahindi. Pamoja na hayo lakini lililowazi ni kwamba mchele kutoka Asia ni mkombozi wa njaa katika Tanzania.
Indica, ni aina ya mchele ambao ni wenye kiwango cha chini cha ubora ukiwa umevunjika kwa asimilia 25, mara nyingi ulikuwa umeonekana kukosa soko lakini hali ya mambo hadi mwanzoni mwa Januari mwaka huu, ilionesha kuwa mchele huu utapata wateja, hii ni baada ya Philippines kuinngia sokoni akiwa ananunua aina hii ya mchele.
Lakini lililowazi ni kwamba hali ya bei ya biashara ya mchele inatarajiwa kupanda Ulimwenguni. Asia ikiwa mlimaji mkubwa wa mpunga, ndiyo pia kuna walaji wakubwa, lakini nchi nyingi za eneo hilo zimeweka vikwazo kwa biashara ya mchele kwa kuweka kodi ya mauzo ya nje na hata kuzuia kwa hofu ya kutokea upungufu wa chakula na kuathiri raia wengi walio maskini.
Tunachoweza kujifunza kwa mwenendo wa biashara ya mchele, Afrika inahitaji kuongeza nguvu katika kilimo cha chakula. Tangu azimio la Maputo kupitishwa kwa nchi za Afrika kuweka bajeti ya asilimia kumi katika kilimo ni nchi chache zimeweza kufikia lengo hili.
Hali ya mambo katika Asia, ambako mchele unalimwa inaonekana kubadilika mno, hasa kutokana na ukweli kuwa ‘style’ ya ulaji imebadilika na kufanya jamii nyingi za huko kupenda kula vyakula vya magharibi,hiki ni kitisho kwa Afrika.
Ingawa mabadiliko haya kasi yake kitakwimu hazipo wazi, lakini ongezo la maduka makubwa ya magharibi na kuongezeka uzito kunakosabishwa na ulaji wa ‘junk food’ ni dalili kuwa sasa Asia inaondoka katika kula mchele kama chakula kikuu.
Afrika haina budi kujipanga, katika kuhakikisha inalisha jamii ya watu wake, kwani kwa sasa hali ya uhakika wa chakula na biashara ya chakula duniani imebadilika mno.
Tuchague moja, kulima mau na viepepeo au kulima mazao ya chakula. Jibu tunalo waafrika wenyewe. Profesa Steve Carter na Dr Kiefer Lee, wanaonya juu ya hatari ya kufikiria zaidi soko la nje na kujitahidi kukidhi mahitaji ya soko hilo, katika kitabu Global Marketing Management wanaandika ‘biashara hii itakuwa haina maana kama chumo lake na zaidi litakwenda tena katika kuagiza kitu ambacho nchi inahitaji zaidi’
Ni wazi kuwa Afrika inahitaji zaidi chakula kuliko chumo hilo la vipepeo au maua, ambayo hata soko la ndani hakuna anayevitumia. Kenya sasa inahaha kuhamasisha matumizi ya maua kwa soko la ndani; kwani asilimia 96, hutegemea soko la nje. Ni wazi kuwa ‘ndoto’ hizi haziwezi kutimia, kwani maua si hitaji la wakenya.
Vinyo hivyo kwa nchi nyingine za Afrika ya joto tumejikuta tunaingia katika mtego kama huu, wa kuhangaika kufikia matarajio ya soko la Ulaya wakati, faida ya huko kimsingi baada ya muda inarudi tena na ziada inahitajika katika kununua chakula.
Hatumaanishi kuwa hii biashara ni mbaya, lakini yatupasa kulinganisha na kutambua mahitaji yetu je yametimizwa? Basi tuweke nguvu katika kilimo cha mazao ya chakula na tuache ‘ushabiki’, kwani hakuna mgeni atakaye kuja Afrika kuja kulima mpunga.

No comments: