Sunday, February 21, 2010

Nembo za kijiografia ni chanzo cha mapato kilichosahaulika

Brand sina neno zuri la Kiswahili lakini katika makala haya tutatafsiri kama ‘nembo’.Kimsingi ni alama ya biashara inayojumuisha rangi, alama, na vifupisho vya herufi. Nembo ikilindwa kisheria inaitwa ‘trade mark’. Katika taaluma ya biashara inaaminika kuwa bidhaa zinatambulika zaidi kwa nembo.
Hili linatokana na ukweli kwamba mteja mara zote anapata faraja ya ‘kisaikolojia’ mara anapotumia bidhaa anayoitambua kuliko kutumia bidhaa asiyoijua na jina au asiyoikubali kwa nembo ingawa inaweza kufanya vizuri.
Mfano mzuri wa jinsi akili zetu zinavyoweza kutekwa na uhimara wa nembo hadi kila kitu ukajikuta unakitambua kwa jina hilo ni nembo ya ‘Shell’, hii ni miongoni mwa kampuni kubwa ya mafuta duniani inayomilikiwa kwa ushirikiano wa Wadachi na Waingereza, lakini hadi leo katika Tanzania kila anayeenda katika kituo cha mafuta anatamka anakwenda Shell ingawa ukweli wa mambo ni kuwa Shell haipo katika biashara ya mafuta Tanzania.
Hili linaonesha wazi kuwa mteja anaponunua bidhaa mara nyingi hanunui bidhaa ananunua nembo.Kibiashara nembo inafaida nyingi, ikiwemo urahisi wa utambuzi kwa mlaji na kuhimarisha marudio ya matumizi.
Ingawa kwa sasa ulimwengu unashuhudia kuibuka kwa nembo binafsi (own brand) kwa kampuni nyingi kubwa duniani, lakini bado mauzo ya nembo zilizobuniwa na kampuni husika kama vile Lee, Levis, bado yapo juu.Katika Tanzania mageuzi haya pia yapo ndiyo tuna dangirizi za KP,Tippo, na vyakula vinavyofungwa kwa majina ya Supermarkets kama Shoprite. Moja ya kampuni kubwa inayofanya vizuri kwa kutumia nembo yake na si za wazalishaji ni Mark Spencer wenye nguo zinazokwenda kwa jina la kampuni badala kuwa nguo kama Lee, Levi’s kama tulivyozoea.
Nembo ni msingi wa biashara na ndiyo maana kuna kampuni zinachaji gharama kubwa si kwa tofauti ya malighafi tu ni kwa vile nembo yao iko na thamani kubwa na yenye kuheshimika. Wataalamu wa mambo ya fedha na mitaji wanakadiria kuwa asilimia 70 ya mtaji wa kampuni iko katika nembo.
Kwa mfano kampuni ya Zain Tanzania mwaka 2007 ilitumia zaidi ya bilioni 5. 1 za kitanzania kwa ajili ya matangazo ya nembo yake tu, hii kwa mujibu wa gazeti la Advertising Age, la Desemba 8 mwaka 2008.Mfano huu unatuonesha wazi kuwa mara nyingi kampuni zinawekeza katika kutangaza nembo zao.
Makala haya itajaribu kujadili umuhimu wa Tanzania kama nchi kupigania haki yake kutoka kwa kampuni za kimataifa au za ndani zinazotumia majina ya vivutio vyetu vya asili nasi tupate sehemu la pato kutokana na mauzo.
Katika Tanzania leo hii kuna makampuni mengi yanayotumia Kilimajanro, Serengeti, Mikumi na kadhalika kama sehemu ya nembo zao kibiashara. Takwimu haziko wazi kama Tanzania inanufaika kutokana na kampuni hizi kutumia majina yetu ya kijiografia kama nembo zao za kibiashara nchi inapata chochote.
Ila mfano wa Ethiopia inaonesha wazi kuwa nchi nyingi za Afrika zinakosa pato kubwa kutokana na matumizi ya nembo zao za kijiografia kutumika nasi hatulipwi hata shilingi.
Wakisaidiwa kisheria na Oxfam; Ethiopia ilichachamaa na kufungua madai ya haki miliki katika Ofisi za Haki Miliki nchini Marekani, ikiitaka Starbuck kampuni kubwa ya kimarekani kufikiria kuipa stahiki yake kwa kutumia nembo ya eneo moja katika Ethiopia kwa bidhaa zake za kahawa inayozalishwa na Starbuck.Kilio cha Ethiopia ilikuwa kudai pato linalotokana na chumo la 'premium price' linalovunwa na 'Starbuck' kutokana na kuuzwa kwa kahawa hiyo katika mikahawa mbalimbali inayomilikiwa na Starbuck katika Ulaya na Marekani.
Starbuck inatumia majina ya Sidamo, Harar na Yirgaeteffe maeneo katika Ethiopia kama nembo ya kahawa yake. Ikimbukwe kuwa Sidamo ni mahali ambako inaaminika ni moja kati ya sehemu ambazo mbegu ya kahawa ya kwanza ilioteshwa na binadamu, hivyo eneo hili inaonesha kuwa ni sehemu nzuri na ipo katika vichwa vya walaji makini wa kahawa na ni wazi kuwa wataithamini kahawa yenye jina hilo kwa heshima ya kihistoria.
Na ubora wa Sidamo kama eneo unatumika na Starbcuk katika matangazo yake kuinadi kahawa yake.Kahawa yenye nembo ya Sidamo ikiuzwa hadi dola 26 kwa kilo huku wakulima wa Ethiopia wakiambulia dola moja tu ya chumo.
Baada ya vuta ni kuvute iliyoanza tangu Mei 2005, Starbuck ilikubali kuipa Ethiopia dola milioni 88 kama pato linalotokana na kutumiwa kwa maeneo yake kama sehemu ya nembo ya biashara.Oxfam iliuita ushindi huu kama ‘fair trade’ ya aina yake kwani wakulima masikini wa Sidamo nao watapata chumo lingine toka kwa kutumika kwa nembo ya eneo lao.
Katika chapisho, Regional Branding Marketing, Matthew Muntberg, anataja sababu moja wapo ya kufanikiwa katika kuchagua jina zuri la nembo ya kijiografia ni kutafuta sehemu yenye heshima ya ‘kipekee’. Hivyo wanaotumia majina yetu ya kihistoria na urithi wa nchi yetu kama nembo zao kibiashara wanatambua hili kuwa ni vitu vyenye mvuto na kuheshimika.
Tanzania ina bidhaa ambazo zinatumia majina ya vivutio, kama vile mlima Kilimanjaro, Serengeti kwa mbuga ya wanyama yenye heshima kubwa Duniani. Bidhaa hizi ni kuanzia maji, bia na hoteli za kisasa zenye kutumia majina yetu ya kijiografia.
Aina ya nembo za maeneo (Regional /geographical Brand) si kitu kipya duniani, kuna Idaho Commission kakika Marekani yenye zaidi ya miaka 70, ikisimamia wazalishaji wanaotaka kutumia nembo hiyo ya eneo kwa kuzalisha viazi mbatata kulipa, huku ikijikusanyia zaidi ya dola milioni 12 kama kamisheni, ya kutumika kwa eneo lao kama nembo.
Kutoza watumiaji wa nembo za kijiografia ni chanzo kingine cha mapato kilicho sahaulika katika Tanzania. Na hili litatupunguzia kutoza kodi watu walio na hali duni hasa wakulima wa nchi hii kwa kodi ambazo ni za kidhalilishaji huku kuna vyanzo wenzetu wameviona na wanavitumia.
Basi wakati umefika wa Tanzania kama nchi nayo ipate gawio kutoka katika matumizi ya vivutio vyetu kibiashara na si kuacha watu wachache wakinufaika na huku watu wengi waliozunguka maeneo husika wakitaabika. Ethiopia imeonesha njia, tujifunze kutoka huko.Shime wataalamu wa sheria.

No comments: