Monday, June 14, 2010

RFID ni suluhu moja wapo kwa bidhaa feki kwa nchi zinazoendelea

Radio Frequency Indentification (RFID) si teknolojia mpya duniani, ila inaelezewa kuchipua sana katika miaka ya 2000. Teknolojia hii ilianza kutumika kwa mara ya kwanza wakati wa vita ya pili ya Dunia na waingereza katika rada za kijeshi kuweza kutambua ndege za maadui na washirika wake.
Tokea wakati huo RFID imekuwa ikitumika sana katika mambo ya kijeshi, ila miaka ya karibuni kuna mabadiliko makubwa hasa katika nyanja ya biashara kuanza kutumia technolojia hii katika kuongeza uongozi wa usambazaji bidhaa (supply chain management) na kupunguza hasara kampuni imekuwa zikipata.
Kampuni kubwa General Motor, imeanza kutumia tangu miaka ya 1984 kwa utambuzi wa bidhaa zenye thamani kubwa hasa injini za magari, pia Toyota kwa kiwanda chake kilichopo Afika Kusini. RFID ni nini?
RFID ni miali ambayo inasafiri katika mawimbi ya redio ikiweza kufanya utambuzi wa kitu bila hata kuweza kuangaliwa moja kwa moja na muhusika. Kwa sasa ulimwengu unatumia ‘bar code’ ili kuweza kutambua kama mzigo husika ni sahihi kwa kusoma namba na kutafsiri, lakini kwa RFDI unaweza kupata taarifa toka mbali bila hata kuona mzigo kama tulivyokwisha kusema.
Katika bidhaa husika badala ya kubandikwa ‘bar code’ RFID tag itabandikwa na msomaji akisaidiwa na mtambo ambao unafahamika kama RFID reader ataweza kung’amua nini kinaendelea kwa mzigo husika. Kuna aina tatu za RFID tag lakini tofauti kubwa ambayo wataalamu wa TEKNOHAMA wanaikubali ipo,ni ile inayotumia betri na isiyotumia betri.
Bidhaa ambazo hazina thamani kubwa hutumia ‘RFID tag’ zisizo na betri, ili kuweza kung’amua mpangilio wa bidhaa ndani ya ghala au hata bidhaa iliyo katika hatari ya kuharibika kwa uzembe wa mpokeaji. Kwa mfano maziwa yanaweza kusahaulika kuwekwa katika hali ya ubaridi RFID tag ina uwezo wa kupeleka taarifa kwa msomaji na kutambua kuwa kuna mabadiliko ya joto kwa bidhaa husika, hivyo kuharakisha uhifadhi sahihi wa bidhaa kama hizi zenye kuhitaji umakini wa hali ya juu.
Katika siku za karibuni ongezeko la bidhaa 'feki' limekuwa ni tatizo kwa nchi nyingi zilizoendelea na zinazoendelea Tanzania ikiwemo. Wakati wote huu Uchina imekuwa ikibeba lawama kuwa ndiyo mhusika na ni muendelezaji wa uuzaji wa bidhaa feki, kwa Afrika.
Hivi karibuni kuna sakata la kondomu feki, likiwa tu linafuatia baada ya sanya sanya ya taulo za usafi za kina mama, ‘always fake’ kukamatwa katika maduka mkoani Arusha. Hangaiko la bidhaa feki ni la uliwengu mzima, lakini jithihada za kupambana zinatofautiana toka nchi moja hadi nyingine.
Tanzania bidhaa zenye ubora mdogo zinatusumbua. Makala haya itajaribu kutupia jicho hali ya bidhaa feki na uwezekano wa teknolojia ya RFID katika kukabili changamoto hii.
Kamisheni ya Ushindani (FCC) inataja kuwa kiwi za milioni 20 na ‘tubelight’ za aina ya Phillips na Britimax zenye thamani ya dola 18000 zimeteketezwa mwaka 2007, kwa mujibu wa gazeti la Daily News la tarehe 1 Mei 2009.
Pia inakadiriwa kwa mwezi Machi pekee 2008, bidhaa zenye thamani ya dola za kimarekani 224,000, ziliteketezwa na FCC. Ni wazi kuwa FCC kwa uchanga wake inafanya kazi kadiri inavyoweza ili kudhibiti bidhaa ‘feki’.
Ni wazi kuwa vita hii inahitaji kuongezewa nguvu na sheria inayowapa walaji nafasi ya kuwa na chama imara chenye kuwalinda tena chenye nguvu ya kulinda masilahi ya walaji.Katika nchi nyingi vyama hivi vipo na vimekuwa mwiba na vimefanikiwa kulinda nchi zao kuwa majalala ya bidhaa ‘bomu’ si toka nje tu hata wazalishaji wa ndani.
Wataalamu wa TEKNOHAMA wanaelezea RFID kama teknolojia moja wapo yenye nguvu yakuweza kumpa mtu uwezo wa kutambua bidhaa tangu pale inapotengezwa kusafirishwa hadi kufika kwa mteja. Kimsingi inaongeza usalama na uwezo wa kufuatilia bidhaa wapi imetoka na imekumbana na hitilafu gani njiani.
Kwa sasa teknolojia hii ingawa iko katika majaribio makampuni mengi kama wauzaji wa bidhaa za reja reja (supermarkets) kama Wal-Mart, Tesco, ASDA , Zara na IKEA, lakini inaonekana kuvutia mno kampuni hizi kubwa, huku IKEA kampuni kubwa ya samani ikitaja kuweza kudhiti upotevu wa kontena zaidi ya arobaini kwa mwaka.Pia imeonekana ina manufaa kwa sekta ya afya katika kupambana na dawa feki na wagonjwa wasio meza dawa kwa wakati.
Marekani pekee inakadiriwa kupata hasara ya karibia dola bilioni 30 kwa mwaka katika dawa pekee kwa kuingizwa sokoni dawa feki na kughushiwa kwa nembo za kampuni husika (counterfeit). Taasisi ya chakula na dawa ya Marekani kwa kuzingatia hilo imepitisha azimio tangu mwaka 2007 kuhitaji wasambazaji wa dawa kutumia RFID ili kuongeza utambuzi wa dawa.
Wanazuoni Castro Linda na Fosso Wamba katika jarida la kisomi,Journal of Technology Management and Innovation, juzuu ya pili toleo la kwanza la mwaka 2007, wanabainisha wazi kuwa RFID ni teknolojia ya kipekee itakayo ongeza ufanishi na uwazi katika sekta ya afya kwani dawa zitaweza kuonekana tangu malighadi hadi kufika kwa mtumiaji wa mwisho.
Huu ni ushindi dhidi ya mapambano ya bidhaa bandia kwani kampuni nyingi kubwa sasa zinataka wasambazaji wake watumie RFID katika kufikisha bidhaa ili kukabili hali ya bidha feki.Hii ndiyo hali iliyoifanya serikali ya Marekani kuhitaji wasambazaji wa dawa na bidhaa za kitabibu kutumia teknolojia hii ili kuweza kuhakiki kwa uwazi.
Changamoto kubwa iliyopo katika kutumia teknolojia hii ni ukosefu wa wataalamu, bei ya RFID tag bado ni kubwa na nchi nyinyi bado hazijakubali matumimzi ya mawimbi ya redio kwa ajili ya usambazaji wa bidhaa. Na kubwa kuliko yote ni changamoto ya haki ya kuwa na siri (right of privacy), kwani kama RFID tag ikibandikwa katika kiatu ni wazi muuzaji ataweza kutambua wapi kiatu chake kipo, tangu akiuze kimepita, ingawa hili linategemea sana na aina ya RFID tag ambayo kwa hali ya kawaida hakuna kampuni itaweza kuweka tag ya namna hii kutokan na gharama yake.
Changamoto ya kukosa siri imefanya RFID kupingwa na watu wengi katika Marekani, hasa watetezi wa haki za binadamu wakidai kuwa teknolojia hii inaweza kufanya mtu kuweza kufuatiliwa na watu wa usalama na kumnyima uhuru wake.
Pia gharama ya tag ya RFID bado ni ghali, huku ikadiriwa kufikia senti 30 za Marekani kwa tag moja isiyo kuwa na betri, ambayo inakisiwa kupandisha gharama za uzalishaji kwa asilimia 26-60 ya zile za usafirishaji kwa masoko ya Ulaya na Marekani.
Pamoja naukweli kwamba RFID tag bei yake kuwa kubwa sokoni lakini kuna dalili kuwa bei yake imeanza kupungua na hasa baada ya kigingi cha haki miliki kupata suluhu na kampuni nyingi za Asia kuanza kuzalisha. Ila lililowazi ni kwamba Afya haiwekwi rehani ili kukabili dawa feki taratibu Tanzania inaweza kujongea katika matumizi ya teknolojia hii.

No comments: