Wednesday, June 2, 2010

wazalishaji wa ndani nao wajichunguze

Si kampeni mpya duniani na hasa kwa wale walio na nia ya kulinda ajira na uchumi wa nchi yao. Tanzania kupitia Confederation of Tanzania Industry inahimiza utumia wa bidhaa za nyumbani kwa sababu kadha wa kadha lakini lililokubwa ni kunusuru uchumi wa Tanzania. Katika Amerika kuna nembo kama ‘made in NY state’, ‘A taste of Iowa’ nakadhalika zote zikihimiza kupenda bidhaa za eneo lako.
Pia katika Amerika kuna wanaharakati wanavalia fulana za ‘Toyota made in Japan, Poverty made in Japan, Unemployment made in Japan’ Si unyanyasaji wala aina fulani ya ubaguzi ni jitihada tu za kukumbushana kuwa yatupasa kupenda bidhaa za nyumbani.
Hivi karibuni kuna ujumbe wa e-mail wenye kuhimizana miongoni mwa watanzania kupenda bidhaa za nyumbani mtandao. Huu ni mwanzo mpya lakini hili kama tulivyokwisha kusema si jambo jipya, ila sasa linaonekana kushika moto miongoni mwa watanzania, hasa baada ya CTI kulivalia njuga.
Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi zinazochipua kiuchumi tatizo kubwa inalokabiliana nalo wakati wote ni uzalishaji ‘supply side’ kwani mahitaji(demand) ni makubwa na mara nyingi chochote kinachoingia sokoni huwa kinapata wateja, na kutokana na hilo ndiyo maana bidhaa hizi za kutoka Asia zimefurika katika soko la ndani. Na nyingi ya bidhaa hizi hazina ubora, lakini tutafanyaje heri lawama kuliko fedheha, hapa ndipo inachukua nafasi.
Madhara ya kufurika kwa bidhaa hizi toka Asia, tumekwisha yaandika katika makala nyingi, leo hapa hayana nafasi ya kujadiliwa. Ila makala haya itajaribu kujadili mbinu za kukabiliana na madhara ya kupenda bidhaa za nje hasa kwa wenye viwanda Tanzania.Kwani hili ndilo suala kubwa tunalopambana nalo, wataalamu wa biashara wanaiita ‘Country of Origin effects (COO)’
Made in……mara nyingi ni moja kati ya vitu vinavyomfanya mlaji apunguze hofu kuhusu bidhaa anayotumia na hasa kuhusu ubora ikiwa kama hana taarifa sahihi kuhusu nchi iliyotengezeza bidhaa hiyo. Ingawa wataalamu wa tabia za mlaji (consumer behaviour) wanalumbana kuhusu uhalisia wa COO kuwa kama moja ya ‘extrinsic values’ mteja anayoweza kuitumia lakini matokeao yameonesha wazi kuwa hii ni moja kati ya maeneo mteja anaweza kutumia kufanya maamuzi ya kutumia bidhaa au la!
Fikiria mtumiaji wa chakula cha watoto cha viwandani atakavyofikiria mara mbili pale anapoona chakula kwa ajili ya watoto kimetengezwa Uchina. Hofu moja kwa moja itatawala na hasa akijaribu kuhusianisha na tatizo la melamine lililoikabili viwanda vya chakula cha watoto katika China. Hiyo hili linafanya mara moja mnunuzi aamue kuacha na kutafuta mbadala. Hiyo ndiyo changamoto inayoikabili sekta ya viwanda Tanzania kwa sasa kwani walaji wameshatendwa, sasa wakiona unyasi (Made in Tanzania) wanastuka.
Kupenda bidhaa za nyumbani ni ‘ethnocentrism’, yaani ni hali ya kuona chako ni bora kuliko cha mwingine anatafrisi Profesa Constance Falk katika jarida la kisomi, Agribusiness, toleo la pili, mwaka 1996.Hivyo hutia ndani imani kwa mlaji kuwa kutumia bidhaa za nje ni kudumaza uchumi wa ndani, na kusababisha kukosekana kwa ajira na nikukosa uzalendo (patriotism).
Hivyo basi ‘Ethnocentrism’ ni zaidi ya uzalendo, kwani hii ni hali ya kuweka maneno katika vitendo huku ukijigamba kuwa wewe ndiyo bora na kuringia nchi yako anaandika Profesa Falk (Tafsiri ni yangu). Ndiyo maana tafiti fulani inaonesha kuwa walaji katika Marekani zaidi ya asilimia 80 wanaona nyama bora na tamu ni ile inayozalishwa na wafugaji wa kimarekani. Wanajivunia cha kwao, na hili tumeliona katika medani za kimataifa katika mambo mengi, kuhusu ubora wa muamerika na Amerika yenyewe.
Lakini hali ni tofauti katika Asia, ambako kubeba begi la ‘GUCCI’ au ‘PRADA’ lililotegnezwa magharibi ni kuonesha kuwa we ni mtu wa thamani na mwenye kwenda na wakati, huku ukionesha kuwa uko na kipato kikubwa. Homa hiyo imeikumba Tanzania, ambako serikali iko tayari kutumia bilioni 3 kwa ajili ya samani toka Uchina, Malaya na Singapore huku wajasiriamali wa Changombe, Suma JKT kutaja wachache tu wakikosa soko la bidhaa zao!
Hali ndiyo hiyo hiyo kwa mtu mmoja mmoja ambapo kunywa juisi ya Del Monte toka Kenya au Ceres toka Afrika Kusini ni ufahari badala ya ile yaUnnat, Kingolwira Morogoro. Orodha inaweza kuwa ndefu kwani kuna vilio vingi vya wazalishaji wa ndani.
Wazalishaji wa ndani watambue kwamba serikali haiwezi kuzuia hili kwani tumelia vya kutosha, makala nyingi zimeandikwa za kutosha watu wamepata shahada zao kuhusu haya mambo na madhara yake na hata walio madarakani baadhi yao hizi ndiyo ‘titile’ za tafiti zao wakati wanasotea shahada zao!
Lakini leo hii katika vitendo ni vurugu tupu, hakuna anayesikia kilio cha wazalishaji. Serikali haiwezi kuacha hili kwa vile yenyewe inataka kodi tu, kwisha. Hivyo ni muhimu kwa wazalishahji kujipanga, na kutafuta mbinu za kibiashara kukabili hii hali, kwani tunaozungumza nao si wasikivu.Na kama wanatarekebisha itachukua muda.Hebu tutupie jicho kidogo mbinu ambazo tunaamini wenye viwanda wanapaswa kuzitumia kukabili ‘country of origin effects’.
Garantii inahitajika kwa bidhaa ambazo zinadumu kwa muda mrefu na zenye thamani kubwa. Kwa mfano, kufanya vizuri kwa magodoro ya Dodoma ni kutokana na kuwepo kwa garantii ya muda usiopungua mwaka kama likibonyea rudisha kwa ‘muuzaji’ naye atarudhisha kiwandani. Hii inafanya mlaji kuona kuwa kuna uhakika wa ubora kwani mzalishaji yupo tayari kupokea bidhaa zitakazorudiswa kwake (reverse logistic) ambayo kimsingi ni gharama kubwa.Hivyo niwazi kuwa kiwanda hakiko tayari kuona inaingia mtegoni, basi ubora ndiyo ngao yao.
Lakini wazalishaji wa nyumbani wengi hawana ‘garantii’ kwa bidhaa zao wala ‘motisha’ sasa anapokuja muuzaji toka nje naye anaweka ‘garantii’ kuonesha ubora wa bidhaa zake ni wazi kuwa ataliteka soko la Tanzania. Mfano mzuri wa ‘garantii’inavyovunja mwiko wa ‘Country of Origin’ ni Honda magari toka Korea yalipoingia Amerika kwani yalikosa wateja kwa dhana kuwa Korea si mtengezaji mzuri wa magari na hakuna anayeitambua kwa umakini katika eneo hilo. Pia kwa Czech magari yao ya Skoda na Hyundai katika soko la Uingereza.
Honda waliweka ‘garantii’ ya miaka kumi, hali iliyofanya wateja kuamini kuwa magari ya Honda si masihara katika ubora leo hii, Honda ni katika wauzaji wakubwa wa magari katika Marekani.
Kuimarisha mawasilinao, ya simu na wavuti. Kampuni nyingi za Tanzania zinatengeneza bidhaa na kuzileta sokoni huku wenyewe wakijificha wasijulikane wako wapi na wanafanya nini. Hili huchangia kwa kiasi kikubwa woga kwa mmlaji. Huu ni ulimwneug wa mawasilino ambako mlaji anafanya uchunguzi na kujiridhisha kabla hata kutumia bidhaa kunawaokwenda katika internet na kutafuta wahusika wa kampuni wanapatikan wapi na kwa namna gani lakini sisi hata ukienda katika website ni madudu tu.Hupati taarifa kamili.
Namba za simu zikitolewa zitaita hadi itakata hakuna anayepokea wala kujali. Sasa kama mteja anataka kutoa oda mpya unadhani atakuwa na imani na kampuni husika. Ukitembelea tovuti zao taarifa zipo kwa kificho sana zaidi ni picha na sanduku la posta,sasa mteja anajiuliza kama huyu ni mzalishaji makini kwa nini anaficha taarifa zake?
Mfano mzuri ni Tanzania Meat Pride kiwanda cha nyama cha Morogoro, wanaozalisha ‘soseji’ ukiwa muuzaji unahitaji soseji zao lakini hawana mawasialiano ya simu wala internet katika paketi zao, sasa sijui mteja akitaka kuongeza oda anawapata wapi. Ingawa wamefanikiwa katika kupunguza wasiwasi kwa walaji wa dini zingine kwa vile wanadai nyama yao imenchinjwa kwa imani ya dini ya Kiislamu (Islamic Doctrine) na BAKWATA wameweka muhuri wao katika kila duka lao na taarifa yao lakini hili pekee haliondoi hofu kama wewe ukiwa bado hutaki kuleta taarifa sahihi ya kuwa uko wapi , na unapatikana vip?
Taarifa kama faida na hasara zilizokaguliwa na wataalamu wa fedha si tu zinawafanya mupate mikopo, la hasha hata walaji wanavutiwa nazo. Kwani kampuni ambayo taarifa zake za kifedha zipo wazi mlaji anaamini kuwa kampuni inaimarika hivyo anaweza kutumia bidhaa husika. Hili ni hasa kwa watengezaji wa vitu vya urembo.
Watumiaji wa mafuta ya ngozi (lotion) na vipodozi vingine hawependi kubadili badili vipodozi kwa hofu ya kuchanganya ‘mambo’Hivyo taarifa hizi za kifedha zitawapa moyo kuwa munafanya vizuri hivyo kuamua kutumia bidhaa zenu kwani wanaimarika na muna nguvu ya kwenda mbele kwa muda mrefu. Hivi ni kwanini kampuni za simu zinatoa taarifa zao au benki unadhani ni kwa sababu ya sheri tu? La hasha walaji nao wanazisoma, ili kufanya maamuzi, kwani walaji wa leo si wale wa Tanzania ya jana, leo soko lina vizazivya 1980 (Generation Y) tena wengi ndiyo hao wapo daraja la kati. Hawa ni wepesi kuiga na wako tayari kujifunza, sasa usipokuja na mbinu za kisasa ni ngumu kuwashawishi.
Nembo za viwango vya ubora. Kulalamika tu hakutasaidia kitu lazima tupambane kisayansi. Njia moja wapo ni hii ya kupata nembo ya ubora kama vile TBS. Nembo hii inapunguza hofu kwa mlaji na kuanza kuamini kuwa bidhaa husika ina ubora inaotakikana. Kwa mfano kufanya vizuri kwa dawa ya meno ya White Dent ni pamoja na kupata hati ya ubora toka kwa Tanzania Dental Association (TDA), hivyo ingawa Aha ilikuwa chini kwa bei kuliko White dent lakini leo hii Aha haipo sokoni. Ni wazi kuwa TDA imeingozea White dent thamani na ubora miongoni mwa wateja .
Hivyo tunahimiza pia si kuamini katika nembo za kiserikali tu hata vyama vya kitaalamu vinapunguza hofu kwa wateja na hasa vyama hivi kwani vingi viko huru.Pia tunaona kuwa punguzo la bei si ushindi kwa kampuni sokoni.
Lingine ni hili la kujitangaza, wazalishaji wa ndani wengi hawajitangazi labda wanaamni katika msemo wa Kiswahili ‘chema chajiuza kibaya chajitangaza’. Ukweli ni kwamba katika sayansi ya bishara na hasa kwa upande wa mlaji(consumer behaviour), mlaji anahusianisha ubora na matangazo kwani kampuni isiyojiamini haiwezi kuweka fedha katika matangazo kwani inaogopa kupata hasara.
Hivyo ile kampuni inayojitangaza mara nyingi inakuwa inanafasi kubwa ya kupata ‘utiifu’ wa mlaji kwa dhana kwamba hii inaubora wa kutosha ndiyo maana imeingia gharama kujitangaza la sivyo isingeliwekeza katika matangazo. Matangazo ni gharama kurasa moja ya gazeti tena isiyo ya rangi ni zaidi ya laki tano katika Tanzania sasa kampuni isiyo na viwango inaogopa kuwekeza katika gharama kama hizi.
Ila mambo ni kinyume chake katika Tanzania leo hii ni kinyume chake kampuni nyingi zinadai zinazalisha bidhaa bora lakini hazijitangazi kwa nini? Jibu rahisi linaweza kuwa wanawasiwasi na bidhaa zao kuwa si bora. Angalia makutano ya barabara kubwa nyingi katika Tanzania kampuni za juisi za matunda toka Kenya na Afrika kusini ndiyo zimeweka mabango ya matangazo yao.Hivyo hili linawajengea imani wateja kuwa kama kampuni hizi zinagalikuwa zinazalisha bidhaa ‘feki’ wasingaliweka mabango na kukubali kuingia gharama, wamefanya hivi kwa vile wamejiamini. Hivyo wazalishaji wa Tanzania nanyi jitangazeni.
Mwisho ni hoja iliyotelewa na Profesa Han C Min mtaalamu wa Marketing, katika jarida la Marketing Reasearch toleo la 26, mwaka 1989, makala ‘Country image: Halo or summary construct? Profesa Han anahimiza wazalishaji kutolindana hasa kupitia umoja wao ili kulinda ubora wa bidhaa zao. Hili la kulindana ndiyo tatizo la wazalishaji wa nchi change Tanzania ikiwemo, kwani kama mutapata sifa kuwa munazalisha bidhaa bora na nzuri wanatokea watu wachache wakiharibu ni taswria ya nchi nzima. Ni taswira ya wazalishaji wote haina mjadala. Leo hii watu wanalalamika kupigwa ‘bambo’ mifuko ya simenti ya kilo hamsini haitimii, wazalishaji wako kimya, sasa ikija sementi toka nje munakimbilia kulalamika wakati kimsingi wenyewe ndiyo musioojali wala kusikiliza mteja anamashaka gani.
Watu wanaozalisha bidhaa feki za konyagi, unga wa mahindi, kufunga vipodozi visivyo na ubora wanaonekana na wanajulikana tena wakati mwingine wanatumia kampuni zilizosajiliwa lakini hakuna kukememeana na kuchukuliana hatua miongoni mwa wazalishaiji na taasisi zao.
Ni vyema kampeni hii ya kuwa mzalendo tumia bidhaa za nyumbani ikawagusa pia wazalishaji nao pia watafute mbinu za kisasa kupambana na hii hali makala haya imebainisha chache tu, lakini kimsingi mbinu za kukabili ‘country of origin effects’ zipo nyingi. Tukishirikiana tunaweza.

No comments: