Monday, April 20, 2009

Kupambana na umasikini sawa ila njia tunazotumia si sahihi

Profesa Fernando De Sotto gwiji wa uchumi mdogo (Micro economics) kutoka Peru katika kitabu chake cha ‘The other path’ anaandika ‘mifumo mibovu ya uchumi uzalisha vyanzo vya kipato visivyo halali’ Kitabu hiki kilitokana na tafiti yake aliyoifanya Peru. Peru ni sawa na Tanzania ina mashaka yanayofanana nasi ingawa mazingira yetu ya kijiografia yanatofautina ila lililowazi nikwamba mifumo mibovu ya uchumi inayoinyonga Peru ndiyo hiyo hiyo inayoinyonga Tanzania.

Nimeona vema nianze na nukuu ya gwiji huyu ili kuweka bayana kuwa upatu kwa naman oyoyte ni matunda ya uchumi wenye mifumo kandamizi, na isieleweke hata kidogo kuwa kutokana na kuchipuka kwa vikundi hivyo vya ujanja ujanja kuna mwisho mwema miongoni mwa washiriki.

Katika mazingira kama haya ya kuona riziki inaweza kupatikana kwa kujifanyia mambo ya kupora haki za waliowengi kwa njia za ujanja ujanja mara zote huonekana kama ndiyo tija ya watu wachache. Mara nyingi tulio masikini tumekuwa hatujifunzi jambo kutoka na na aina hizi za udanganyifu za kupata mafanikio kwa pupa.

Lazima ieleke kwamba Serikali yoyote Duniani jukumu lake kubwa ni kulinda haki za watu wake na si kuona kila wakati tunanyanyasika na kupokonywa hata kile kidogo tulichonacho. Mara zote masikini wamekuwa wagumu labda hili linatokana na hali yetu na kufikia kuona kuwa ‘liwalo na liwe’.

Mwaka 2007, tulijionea jinsi wajanja wachahce walivyo jipatia utajiri kupita michezo hii ya upatu. Tulipokuwa shule rafiki yangu alikuja na fomu ya kampuni ya ‘Faidika Investment’ na kunishauri kununua fomu ile kwa elfu 50,000/=. Nami baada ya mzunguko nitapata nafasi ya kupata fomu zangu tano zitakazopelekea kupata 250,000/=.

Uhakika wa fedha zangu kurudi itategemea sana na jinsi nitakvyoweza kushawihsi wengine kujiunga kwa kununa fomu yenye majina matano kwa shilingi elfu hamsini. Nilisita na kumwambia wazi kuwa asimuambie mtu kwani ameshaibiwa, huo ni upatu hauna mwisho mwema.

Kwa vile tulizoea kuwa na mijadala alihisi kuwa ndiyo chochoko zangu za mijadala zimeanza,akanishawishi kuwa huu si upatu kwani unachezeshwa na waumini wa kilokole wa EAGT ambalo yeye ni muuni wake. Nilijibu ulimwengu wa pesa mgumu hauna mlokole wala aliye karibu na madhabahu angalia unaibiwa, nilisisitiza.

Miaka miwili leo hii tangu FAIDA isimamishwe na mkurugenzi wake kufikishwa mahakamani ambaye alikuwa raia wa Kenya, sijui nini kiliendelea , ila yeye alipoteza shilingi 100,000 mpaka leo hajui aingilie ofisi gani ili kudai haki yake.Huo ndiyo upatu hauna mwisho mwema.

Nipo kibaruani mfanyakazi mwenzangu anakuja akitamba kuwa ana taarifa za mafanikio nazo kuhusu DECI akinimabia yeye amepanda 200,000/=. Nilimuambia nyamaza utachekwa ukweli wa mambo umeibiwa huo ni upatu, hauna mwisho mwema. Kitaaluma huyu ni mtaalamu wa Uchumi nilimtania kuwa kwa nadharia za biashara ulizosoma darasani ni lini ulipoambiwa kuwa mtaji unaweza kuleta faida ya asilimia zaidi ya 20 tena baada ya kulipa kodi nayo ikawa ni biashara halali kama si utapeli ni nini?

Liliowazi ni kwamba haya matukio ya FAIDA na DECI yanayahusisha makanisa ya uhamsho na yanatia ndani hulka ya pupa. Wakati umefika wa kuchambua mambo kwa kina na uwazi juu ya baadhi yetu tunaotumia kivuli cha madhabahu kuendesha dhuluma.Taasisi zenye dhamana ya kulinda usalama wanchi zichunguze kwa kina makanisa haya ya uhamsho.

Niliwahi kuandika katika siku za nyuma (2006) katika gazeti hili juu ya kushamiri kwa ‘pupa’ miongoni mwa watanzania kunakodhihirisha na kuibuka kwa michezo ya kamari nchini.

Pupa mara zote ikitawala hata uambiwe nini husikii, Naomba ielekwe bwana wa pupa ni shetani yule muovu.Faida investment imekuja imekula fedha za watanzania kwa kutumia ‘pyramid’ imeondoka leo hii tunashauriwa kuikubali DECI. Hii nini!Hatushangai kuona watanzania hawajakoma kwani hii ni kawaida yetu na hasa kwa vile pupa imekua ndiyo nguzo yetu ya maisha siku hizi. Chukulia mfano wa mchezo wa karata tatu unavyoumiza watu lakini bado utawaona wanang’ang’ania kucheza.

Naomba ieleweke kuwa kinachogomba si kwamba DECI haiwezi kuleta unafuu wa maisha kwa watanzania tuliowengi, wala si kwamba haiwezi kutoa mihela kwa watu waliowanyonge baada ya kukosa mikopo toka benki. La hasha isipokuwa ni kwamba njia inayotumiwa si halali ni njia ambayo kwa miaka mingi na matukio mbalimbali nchini imethibitisha ni utapeli mtupu.

Chumo la DECI asili yake wapi? Taasisi yoyote inafanya biashara ya fedha inatoa chumo lake kubwa toka katika mikopo na marejesho yanayotokana na mikopo kama riba ili kuendesha taasisi husika. Pia inaweza kupata fedha toka katika uwekezaji katika taasisi au shughuli mbalimbali za kiuchumi kama vile ununuzi wa hisa katika kampuni au hata benki na ununuzi wa dhamana za serikali.

Sasa chumo la DECI asili yake wapi, linalofanya kuweka 200,000 upate 500,000 ndani ya miezi mitatu. Nadharia za biashara zinabainisha wazi kuwa hakuna faida halali inayozidi asilimia 20. Nilitegemea menejimenti ya DECI ingeweka wazi sikuile PTA kuwa sisi tunaweza kutoa laki tano kwa mtu aliyetupa laki mbili kwa sababu ‘pando’ la mteja linawekezwa kwa jinsi hii nasi tunapata faida .

Lakini haikufanya hivyo ila ilikuja na hoja ya kuwa wao wanabinywa kwa vile kuna udini. Hii hoja si hai, ni kuishiwa kutoa hoja zinazojenga. Wanaendelea kutoa kilio kwa Rais Kikwete awatetee, sasa atetee nini? Taasisi gani inayoweza kuendeshwa kwa michango ya wanachama, eti inawanachama 600000 na kila mwaka wanachangia elfu 30, nasi tunajipatia bilioni 18, hivyo kwa pato hili sisi hatuwezi kutetereka!
Huku ni kuishiwa hoja walipaswa pia watuambie kuwa wakipata bilioni 18 wao wanazifanyia nini ili zikue,na hao wateja wasipokuja kinatokea nini?Au wanajifanya hawajui mzunguko wa biashara (business cycle) kuwa kuna siku utakuwa kileleni(Peak) kuna kipindi kutakuwa na ‘anguko’(recession)!

Gazeti la jumapili la mwananchi la tarehe 12.04.2009 lina taarifa ya mtu mmoja anayekiri kupata mafanikio kutokana na DECI pia anaeleza wazi kuwa kuna mtanzania ameweka zaidi ya milioni mia moja. Tuulizane DECI inafahamau kuwa kuna kitu kinaitwa ‘kuosha fedha’. Katika fedha zaidi ya trilioni moja (kama ilivyoripotiwa na gazeti moja la kila siku) ambazo inazo katika akaunti yake ni kiasi gani ni fedha halali?

Wakilili na Mhadhiri wa Chuo cha IFM, Eugene Mniwasa katika kazi yake ya ‘Detection and suppression of money laundering in Tanzania ; alivitaja vyanzo ambavyo vinapelekea mapato ya fedha haramu kuwa ni pamoja na mikopo isiyo rasmi. Sasa tujiulize katika shughuli hizi zinazofanywa na asasi hii ni kwa kiasi gani imechochea uoshaji wa fedha haramu. Menejimenti ya DECI inapaswa itujibu.

Sheria ya 2004 ya udhibiti wa fedha haramu pamoja na mambo mengine inataja juu ya kumtambua mteja (Customer identification) kabla ya kupewa huduma ya kufunguliwa akaunti sasa hawa jamaa wanakopeshana kwa kufungua kwa kiasi kidogo dogo kitu ambacho ni hatari, hii ni mbinu ya kusafisha fedha kati ya zile nyingi hii inaitwa layering (utagaji).

Muosha pesa huwa anakuwa na akaunti zaidi ya moja katika benki moja na anaweka kiasi kidogo kidogo ili asijulikane kiurahisi kuwa anachanzo cha chumo lisilo halali. DECI inawezekana bila kulitambua hili imejikuta inawezesha uoshaji wa fedha haramu.

Tanzania ni yetu sote lazima tulindane kwa kuhakikisha chumo halali linapatikana kwa kila mmoja wetu, ni wazi kuwa kuna kipindi waliowengi wanaweza kuona wanaonewa. Ila ifahamike kwamba umasikini wetu hauwezi kupunguzwa kwa kutetea kamari. Hatuna kinyongo na harakati zozote za kupunguza umasikini, ila zifuate njia za halali na si ujanja ujanja.

Kimsingi serikali inapaswa kulinda mali za watu wake, basi jicho la kumulika taasisi za mikopo ya fedha isiyo rasmi lazima liangaze kila kona ya nchi kwani DECI ziponyingi na kwa kutumia mwanya huo fedha haramu zinaoshwa kiurahisi kabisa.

Prince Niccollo Machiavelli aliwahi kubainisha wazi kwamba ‘raia anaweza kusahau na kukusamehe hata ukimuua babake lakini si kupora mali yake’Taarifa ya habari ya TBC1 14.04.2009, usiku saa imeripoti kadhia aliyoipata ofisa wa DECI maeneo ya mabibo pale wanachama walipogomba asitoke hadi polisi walipokuja kumuokoa,na taarifa zinasema Kenya waliuana mambo hayo hayo ya upatu, niwazi kuwa maneno ya Niccolo yana ukweli.

Shime wenye mamlaka,tekelezeni wajibu wenu na si kuona mambo yanaenda hovyo mnakaa kimya, kwani DECI iliomba kuwa SACCOS sasa mlikuwa munasubiri nini wakati mnaona kila kitu hakiendi sawa, au kwa vile ni walokole?Hii siyo sawa.

Kila mmoja wetu na atambue pupa haina mwisho mwema acha kucheza kamari. Mwenye masikio na asikie.

No comments: