Saturday, April 18, 2009

Muhogo zao linalohitaji msukumo mkubwa

Muhogo zao linalokumbukwa wakati wa njaa,halina thamani. Nakumbuka ukiwa shule ukionekana unakula muhogo’chipsi dume’, ilikuwa unataniwa kuwa utagombana na nguruwe. Duniani zaidi ya tani milioni 202.65 huzalishwa kila mwaka, na likitoa ajira kwa watu zaidi ya milioni 500, huku likitemegewa kama chakula kwa watu zaidi ya milioni 800 ulimwenguni kote.

Tanzania inakadiriwa kuzalisha zaidi ya tani milioni 2 za muhogo kwa mwaka..Tafiti nyingi zimefanywa na zinaendelea kufanywa zikijikita katika kufanya zao la muhogo kukubalika miongoni mwa jamii za watu masikini kuwa si kimbilio la njaa bali ni chakual bora na chanzo cha pato muhimu kwa wakulima wetu.. Pesa zinaungua na zitaendela kuungua katika kufadhili tafiti za moja kwa moja na tafiti za kichunguzi.

Hakuna ubaya katika kufanya tafiti, lakini wakati umefika tujiulize,je tunahitaji tafiti zaidi juu ya muhogo, na kama ndiyo katika maeneo gani hasa ambayo yanaleta vikwazo kwa zao hili.

Ili tuwe na uhakika lazima tujue masaibu yaliyolikumba zao hili hadi kufikia kusahaulika na kuonekana kuwa halina thamani nchini hadi njaa itokee, ndiyo utasikia pandeni mazao yanayostahimili ukame kama muhogo, loh siku zote tulikuwa wapi! Ukiangalia kwa haraka utaona ni Tanzania tu ndiyo zao hili liko nyuma na halithaminiwi miongoni mwa wananchi wake. Linalotia uchungu jamii inayokataa kula muhogo si kama ni zenye neema la hasha mara zote ni watu wakulilia misaada na fadhila za serikali au wahisani.

Wakulima wengi wanaolima muhogo nchini hufanya ni kama kilimo cha kujikimu, utatembelea maeneo ya vijijini utashangaa kujionea mashamba ya muhogo yamelaa miaka zaidi miwili bila kuvunwa ilihali ni chanzo cha kipato kwao. Lakini nchi za Africa magharibi muhugo ni lulu na unaingiza chumo zuri miongoni mwa wakulima wa nchi hizo.Haya hayakutokea tu ghafla bila mipango madhubuti.

Mfano katika Nigeria ni sera nzuri zilizofanya muhogo kuhimarika na kuwa chanzo cha pato miongoni mwa wakulima wake. Katika kila uzalishaji wa unga utokanao na nafaka miongoni mwa wazalishaji wakubwa wanatakiwa kutumia 5% ya unga wa muhogo. Hili hufanya mahitaji wa muhogo kuwa makubwa katika viwanda vya ndani vya usindikaji wa nafaka na kupelekea soko la uhakika.

Hivi karibuni nchini kupitia vyombo vya habari tumesikia kilio cha wadau wa zao la muhogo katika kuiomba serikali kufanya zao la muhogo kuwa la biashara. Kilio hiki si kipya ni cha muda mrefu na napenda kuweka wazi kuwa kufanya zao la muhogo kuwa ni zao la biashara ni kwa kulitafutia namna ya kupata soko la uhakika kwa kutunga sera endelevu zilizojikita katika tafiti na maendeleo (R&D). Tahadhari uuzwaji wa muhogo usifanywe kwa ajili ya kuchangaya kwa chakuala cha wanyama nchi yetu haijafikia huko.

Pamoja na kupigiwa debe kuwa muhogo unahitaji kuwa na soko la uhakika, ni wazi kuwa tahadhari inahitajika katika uandaaji wa zao hili kwa ajili ya chakula cha binadamu, kwani liliowazi ni kwamba muhogo ukiandaliwa vibaya unamadhara makubwa kwa binadamu kama vile kupooza kwa miguu kunachongiwa kwa kiasi kikubwa na uzalishaji wa mihogo michungu yenye sumu ya cyanogenic.

Tafiti zinaonesha hiki si kikwazo kikubwa kwa vile muhogo ukilowekwa katika maji kiasi hiki cha sumu hupungua, au hata ukianika juani kuna kiasi hupungua. Hizi ni habari njema na zenye kutia moyo katika kuona muhogo unavuka kigingi cha kuwa na sumu inayoweza kufanya miguu ya mtumiaji kupooza.

Kigingi kilichobaki kwa sasa katika kufanya muhogo uenda sokoni na kukubarika miongoni mwa jamii ya kitanzania ni sera na mtizamo wa kifikira. Mitizamo yetu hasi inatufanya tuwe watu wa kulia njaa kila wakati.

Bila kubadili mitizamo yetu katika milo siku zote tutakuwa ni watu wa kuona njaa inatunyemelea kisa mahindi hatukuvuna kiasi cha kutosha. Tunajaza watoto wetu fikira za woga kuwa akila muhogo ataonekana mchovu ni kandamizi na hasi kwa vizazi vijavyo vya nchi hii.

Mbunifu wa ‘corn flakes’ Dr John Harvey Kellogs na ndugu yake Will Keith Kellogs mwaka 1906 walifanyaubunifu nchini Marekani walitumia ngano nyeusi ambayo ilikuwa haithaminiwi kwa walaji na baada ya kuibadili kuwa hizo corn flakes ambazo leo hii ukienda supermarket kubwa duniani kote zinagombaniwa asili yake ni ngano nyeusi zilizodharauliwa na walaji. Na sisi tunaweza kubadili muonekano hasi wa zao la muhogo nchini.

Lazima tubadilike kwanza kifikra dhidi ya muhogo, na hakuna mchawi mwingine wa njaa inayotukumba ni kujaribu kufikia nadharia ambazo kitaalamu ni ndoto. Utashangaa mtu anakomaa kulima mahindi maeneo ambayo mvua ni haba, kisa chakula kikuu (staple food), ili iwe nini? Lima muhogo uone utapata nini?Muhogo unastahimili ukame hili lipo wazi.

Sera imara zenye kuona muhogo unafika sokoni zitasadia nchi hii. Muhogo unachangia zaidi ya asilimia 15 ya fuko la chakula kwa mwaka , na inawezekana kuongezeka endapo wakulima wataona kuwa kuna mtetezi wa kudumu, na utetezi huo si wa maneno bali sera kama zile za Nigeria. Tafiti zimefanywa nchini katika kuona uchanganyaji wa muhogo hauthiri ladha na muonekano wa vyakula vingine kama vile chapati, biskuti,maandazi na kadhalika.

Asilimia 25 ya unga wa muhogo inahitajika katika kutengeza maandazi. Sasa maandazi mangapi yanatengezwa kwa siku nchini, unga wa ngano tani ngapi unauzwa na kampuni zetu kila siku nchini.Muhogo ni lulu tubadilike.
E-mail fagdas1980@yahoo.com

No comments: