Saturday, December 5, 2009

kuhamasisha mitaji toka nje ni 'mbio' za ubora si uwingi

Katika ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla Tanzania inafanya vyema katika kuvutia mitaji toka nje. Ripoti ya UNCTAD ya mwaka 2008 inataja eneo la Afrika Mashariki kuvutia asilimia 4 ya fedha zote zilizoingia Afrika, huku Uganda na Tanzania zikijizolea chumo kubwa. Ila changamoto kubwa ni kupunguza migogoro inayochangiwa na kuvutia mitaji ‘isiyo na ubora’ bali ni kujali ‘uwingi’.
Tanzania sasa ‘inazizima’ na vyombo vya habari kila kukicha vinapambwa na hekaheka za TRL ni vilio na maneno ya kukata tamaa toka kwa wateja(abiria) na wafanyakazi. Ni wazi kuwa hali si shwari, hali ya sintofahamu imetawala lakini lililokubwa ni majaaliwa ya sera zetu katika kuvutia mitaji toka nje(Foreign Direct Investment).
Changamoto hii ya migogoro katika kila ujio wa mwekezaji imekuwa ni ya kawaida sasa nchini, ila wakati wote imekuwa hatujifunzi somo. Ni kwanini migogoro hii kwa kiasi kikubwa inakuwepo katika mitaji(FDI) inayowekezwa na watu kutoka nchi zinazoendelea?
Mbio za kutafuta mitaji tangu zilipoanza katika Tanzania na hasa hizi za pili akiacha zile za miaka ya 1960, imekuwa ni kuangalia wingi tu na si ‘ubora’ wa mitaji. Wakati wote taarifa tunazopewa nikuwa tumeajiri watu wangapi na wala si kama kinachotumika na kampuni husika kina kiachangiaji katika kuinua hali za watanzania ya Tanzania. Manufaa yake ni chanya au hasi.
Mwanazuoni maarufu Profesa Issa Shivji anawaita wawekezaji ‘uchwara’ ni wazi kuwa jamii nzima toka wasomi hadi watu wa kawaida siku hadi siku wanaona FDI na namna tulivyoikumbatia nadharia hii kama mkombozi wetu wa kiuchumi haina mwisho mwema.
Mgogoro wa NBC ambao bado unafukuta ndani kwa ndani ni mwekezaji toka Afrika Kusini, kiwanda cha Sukari Mtibwa ni ‘mgogoroo’ kati ya Mwekezaji toka ‘Mauritius’, Kilombero Sukari ni hao hao toka ‘Afrika Kusini’. Wajasiriamali wanalia hawapati hata nafasi ya kuuza ‘embe’ kila kitu kinatoka ‘Afrika Kusini’ ndiyo mwekezaji aliyechukua hoteli tulizojenga wakati wa Ujamaa anatoka Afrika Kusini!NetGroup Solution walitoka Afrika Kusini na ATCL iliwahi kuwa na ndoa yenye utata na Shirika la Ndege la Afrika Kusini. Hili la sasa la TRL ni mwekezaji toka India.
Hatuna nia ya kusema kuwa wakati umefika kwa kuangalia miradi ambayo inakuja nchini inatoka wapi (origin) lakini kila dalili inaonesha hawa wenzetu wanaokuja katika nchi zetu hawana nia ya kutuona tunaneemeka, wala hawana nia ya kuiona nchi inajikongoja ila ni kuhakikisha wanatafuta ,malighafi’ na ‘masoko’ kwa ajili ya viwanda vyao.
Lazima tutambue kuwa hawa wawekezaji toka nchi zinazoendelea wanamashaka kama yetu na yatupasa kujipanga vizuri kisera na kimaamuzi.Ni wazi kuwa mitaji hii kutoka nchi zinazoendelea ni sawa na kucheza na mtu hatari(Dancing with devil), huku ukiamini labda amebadilika, lakini tunayoyaona nchini ni wazi kuwa uwekezaji huu hauna mwisho mwema.
Tumefika mahali tumegeuzwa soko la bidhaa zao huku sisi tukizalisha malighafi na kuwauzia kwa bei ya ‘kutupa’ kwa faida ya ajira ya watu 500 hadi 1000 tena vibarua wasio na bima wala kitambulisho wakifanya kazi kwa zaidi ya miaka 5!
Mwekezaji atafungua hoteli utapewa takwimu za kuwa anaweza kuajiri watanzania zaidi ya 100 ajira ya moja ya moja kwa moja na 300 ajira ya isiyo moja kwa moja! Mbio hizi hazina mwisho mwema na ndiyo hizo zimetukisha hapa tulipo.Yote haya ni mbio za ‘wingi’(quantity) huku tukikipa kisogo ‘ubora’(quality).
Ni vigumu kutafrisi ubora wa ‘mtaji’ ukawa na tafiri inayoichukua kila nchi,lakini lililokubwa ni kuangalia hali ya maendeleo ya nchi na nini inataka kupata kutokana na huo mtaji (FDI Spillover effects). Kwa mfano Tanzania haihitaji muwekezaji anayekuja kuuza ‘pipi au vyombo’ vya plastiki kama wale Wachina wa Kariakoo, au wale Wahindi wanaozunguka na biskuti duka hadi duka kutafuta mnunuzi wa jumla!
Hizi biashara ni za wazawa, lazima tuweke maeneo ya wageni kuja kuwekeza na wakiwekeza basi kuwe na tija kwa wazawa si kuwekeza katika kiwanda kisha unaleta mahitaji yote kutoka katika nchi ‘mama’.
Tunakumbuka jinsi TBL walivyoanza kuagiza chupa za bia kutoka Afrika Kusini mara tu walipochukua kiwanda huku tunakiwanda cha KIOO hali ambayo ilisababisha watanzania kukosa kazi, hadi leo hii mambo yamebadilika lakini baada ya vuta ni kuvute.Hali pia inatia matumaini kwa wakulima wa shayiri mkoani Arusha ambao wamepata nafasi ya kuuza malighafi yao kwa TBL huku wakihimarishwa katika kulima shayiri bora, hii ndiyo mitaji yenye ubora kwa nchi (positive spillover of FDI).Lakini hali si kwa viwanda vyote nchini.
Sasa tunalia na kiwanda cha betri cha Yuasa kilichopo vingunguti, kimefungwa kisa kuna mwekezaji anaagiza betri kutoka Uchina na Thailand. Tumegeuzwa soko huku kiwanda tunacho. Sasa wale vijana tunaowasomesha uhandisi na ufundi michundo huku tukiimiza wapende sayansi na tukiwalipia ada kwa asilimia mia watapata kazi wapi kama viwanda vinakufa ‘kibudu’ namna hii! Atalipaje deni lake la mkopo wa elimu kama hana kazi kwa vile kiwanda kimefungwa kwa kujali tu mwekezaji aliyefungua ‘store’ ya kuuza betri za magari toka nje.
Kilio kipo kwa KIBO Match group dhidi ya mwekezaji mjanja mjanja anayejidai anazalisha viberiti kumbe ameweka ghala na anavileta kutoka Pakstani. Huu si ushindani hata kidogo!Vile vile kwa wazalishaji wa makaa ya mawe Mbeya, ambao wakipeleka katika kiwanda cha sementi pale Wazo Hill wanaambiwa hayana ubora hivyo wanaagiza ‘makaa’ ya mawe kutoka Afrika Kusini. Ila tumekosa soko ndani Ujerumani wanasema haya ndiyo bora tena yenyewe. Hii ni ajabu, lakini ndiyo hali halisi.
Hili la kuongeza mbio katika ‘wingi’ tukiacha kuweka mkazo katika ‘ubora’ limepelekea kuibuka tatizo la uwekezaji ambao haufanani na kile walichokisema wakati wa kutia saini kwa mbwembwe za miali ya kamera na ‘champagne’. Hili la kukosa ‘ubora’ ni kero hasa kwa mitaji toka nchi zinazoendelea.
Kwa mfano Brookside wasindikaji wa maziwa ambao wapo Kenya wakiendesha kiwanda cha usindikaji wa maziwa na bidhaa zake. Mwaka 2007 walikuja Tanzania wakanunua kiwanda cha maziwa Arusha kwa ahadi ya kuwekeza zaidi ya dola milioni 20 kwa kiwanda cha UHT chenye uwezo wa kusindika lita 60,000 kwa siku. Baada ya miaka miwili ikabainika kuwa wamegeuza Tanzania kuwa eneo la kukusanya malighafi huku wakipeleka maligahfi hiyo Kenya! Sasa kampuni hii imezuiwa kufanya Tanzania kama ‘shamba la bibi’ na badala yake itimize yale yaliyokuwa yamewaleta.
Huu ni mfano mmoja lakini kampuni nyingi zimekuja nchini kwa ahadi na maneno kede kede ya kuwekeza katika mitaji ambayo ina manufaa kwa nchi badala yake wakaanza kuleta mitumba na kujenga gesti.
Changamoto nyingine ya mitaji hii kutoka nje ambayo inaikabii Tanzania ni hili la kufukuzia mitaji toka katika nchi ambazo zinaongoza kwa rushwa. Kenya, Nigeria zinawekeza katika Tanzania lakini hizi nchi zinatajwa kuwa zinaongoza kwa rushwa. Sasa unapokuwa na mwekezaji ambaye asili yake ametokea katika rushwa ndiyo yale yale kila ‘skendo’ mbili moja ni mwekezaji anatoka katika nchi zinazoendelea. Hii inadumaza ubora wa mitaji katika kufikia lengo.
Rushwa ni adui wa haki hivyo yule aliyekuwa makini na mwenye sifa hakupewa kapewa mtoa rushwa, kila siku ni vurugu na hatutaki kila kona badla ya kuchapa kazi kwani hana mtaji ana maneno. Haya ndiyo majaaliwa ya rushwa.
Katika siku za mwanzo za uhuru wake Kenya alichagua kuwabana wawekezaji toka nje na kuwaonesha maeno ya kuwekeza na si kila eneo walipewa nafasi. Wawekezaji hawakuruhusiwa kuwekeza katika maeneo ambayo wazawa waliweza na hili lilifanyika bila kificho. Leo hii Tanzania inaugulia namna ya kuwabana wawekezaji wanauza matufaa na vyombo vya plastiki mitaa ya kariakoo.
Nchi zisizokuwa na rushwa yenye kukera ndizo zinazopendwa sasa sisi kwa nini tusiamue kuwakataa hawa watu wanokuja kuwekeza kwetu kutoka maeneo ambayo rushwa ni tatizo. Matatizo yake ndiyo hayo Waziri Mustapha Mkulo amekiri wazi kuwa rushwa ni ngumu kuisha katika Tanzania na serikali haiiwezi, sasa kama jibu ndilo hilo haki za wafanyakazi na ubora wa mwekezaji utaupata wapi?
Katika siku za mwanzo za uongozi wake Mkuu wa Mkoa wa Dar-Es-Salaam William Lukuvi aliweka bayana kuwa atapambana na wamachina ambao ni ‘wamachinga’ katika mitaa ya kariakoo, lakini hadi leo hali ya mambo ni ngumu.
Mitaji yenye ‘ubora’ ni suala la kisera pia si suala la maneno ‘matamu’ yasiyoongozwa na kanuni wala ‘miongozo’.
Tangu ukoloni ilikuwa inajulikana wazi kuwa benki na vyanzo vya fedha vilivyoanzishwa vilikuwa kwa ajili ya matabaka, na ni wazi kuwa waafrika tulikosa kufaidi utamu wa uchumi katika ardhi yetu wenyewe kwa kukosa vyanzo vya kifedha. Hali hii iliendelea katika siku za mwanzo za Uhuru hadi pale tulipotaifisha taasisi hizi kuwa za taifa. Lakini leo hii hali ile ile imejirudia mtanzania hakopesheki, ila mgeni anakuja na dola moja anarudi na mtaji kwao.
Kilio cha kuwa hatukopesheki ni dhidi ya benki nyingi zenye asili ya India, Kenya na Afrika Kusini. Ni wazi kuwa mitaji hii imewekwa ili kuwanufaisha binamu zao wanaofanya biashara nchini! Kati ya watu waliokuwa katika jopo la kushauri juu ya kuuzwa kwa NBC kwa ABSA, Wakili Nimrod Mkono amekiri kupitia vyombo vya habari kuwa walifanya kosa kuiuza NBC kwa dola milioni 15!
Hili linawezekana kwa vile wao ndiyo wanamiliki mitaji na maduka ya kuuza mitaji yaani benki,hivyo mitaji kama hii haina maana wala tija kwa Tanzania hata kama ikawa benki zipo na zinachipua kila siku lakini ni za wageni maana yake wanakuja kurahisisha ndugu zao kujipatia mitaji na kuongoza uchumi wetu.
Haya ndiyo makaosa ya FDI bila kujali itakuja kumtumikia nani?Umepokea bila kujali ulikuwa umeweka mawazo katika uwingi.Na ndiyo manaa ukimuuliza mtanzania wa kawaida atakwambia pato la taifa linakuwa lakini haoni manufaa yake, kwa vile hawa waliokuja na mitaji yao wakipata tano yote inaenda kwao kununua matufaa(apple) kuku, nyama ya ngombe. Wakati matufaa yapo Iringa yanaoza. Zaidi ya asimilia 60 ya matunda Tanzania yanaaribikia shambani huku tunaagiza mananasi toka Afrika Kusini mukiyashabikia katika maduka ya Shoprite na Games.Hapa kuna tatizo nalo ni kwamba hatukuangalia ubora.
Shirika la Umoja wa mataifa la UNCTAD linabaisha wazi kuwa senti 75 za kila dola inayoenda Singapore kama mtaji toka nje katika kiwanda cha kufyatua Compact Disc (CD) inabaki humo humo, Afrika ni senti 37 tu. Tena hizi ni Takwimu za Nchi zenye mafuta na zenye uchumi imara miongoni mwa bara hili.
Hali inawezekana ikawa ngumu kwa Tanzania ambayo inaruhusu muwekezaji kukodi ndege kuagiza nyama ya kuku huku kuku wapo wanafugwa Kibaha, ukiuliza wananuka ‘dagaa’! Ohh mara hawana zaidi ya kilo mbili. Mbona ukienda katika supermarket zao utaona wapo wa kuanzia gramu 700 hadi 2500 katika majokofu na wanauzwa bei tofauti tofauti sasa siwachuukuliwe na hawa wawekwe katika mtindo huo huo!Muwekezaji anatupangia sisi nini cha kufanya katika nchi yetu kwa manufaa yake!
Hali inaonesha tunahitaji zaidi mabadiliko ya kisera Tanzania ni yetu leo na vizazi vyetu kesho. Makosa yetu leo kwa hongo zisizo na maana nikikwazo kwa vizazi vijavyo. Sera zetu lazima zioneshe kuwa tunahitaji ‘ubora’ katika FDI na si kuhesabu miradi mwaka huu ni mia kadhaa, haina mwisho mwema.
Shime wenye mamlaka, sasa wakati umefika wa kufikiria zaidi Tanzania kwanza si mpaka mukitoka ofisini ndiyo mnajifanya kujuta kupitia magazeti.
Mungu Ibariki Afrika
Mungu Ibariki Tanzania.

No comments: