Friday, October 30, 2009

Stakabadhi ghalani inahitaji ubunifu zaidi na si kusambaza 'woga'(SEHEMU YA KWANZA)

Siku chache zilizopita vyombo vya habari nchini viliripoti hoja ya kupinga kwa stakabadhi ghalani (warehouse receipt) toka kwa wabunge. Miongoni mwa wapinzani wa ‘stakabadhi ghalani’ ni Mheshimiwa Zito Zuberi Kabwe(Kigoma), Mohamed Sinani (Mtwara Mjini), Dustan Mkapa (Nanyumbu),Juma Abdalah Njwayo(Tandahimba) na Rainald Mrope (Masasi), Abdalah Mtutura (Tunduru) na Ibrahim Sanya (Mji Mkongwe).
Hoja yao ni kwamba stakabadhi ghalani ni mfumo wa ‘kinyonyaji’ kwa vile unamkopa mkulima, na kuna wanaodai kuwa mfumo huu ni wa kumtenga mkulima mdogo. Tunakiri kwamba mfumo huu ulipata upinzani mkubwa tangu kuasisiwa mkoani Mtwara.
Lakini upinzani wa safari hii umekuwa ni ‘mkali’ mno.Na linalotia shaka ni kuona kupungua kwa ‘ubunifu’ miongoni mwa viongozi katika kuboresha hali ya biashara ya mazao nchini.
Ubunifu (Innovation) ndiyo msingi mkuu wa mafanikio katika biashara ya ulimwengu wa leo. Biashara haihitaji tena woga,ila inahitaji kujitoa mhanga na kugeuza ‘woga’ kuwa changamoto huku ukifanikiwa kupitiwa changamoto.
Daima changamoto hazikosekani, na kwa mbunifu hizo ndizo chachu za kusonga mbele na si kurudi nyuma wala kukiri ‘kufeli’. Tanzania ya leo inahitaji viongozi wajasiriamali na si waoga ingawa kitu ni kizuri.
Kwa mfano Mheshimiwa Mrope anasema kuwa mkulima anakopwa na hapati malipo kwa wakati, hili linawezekana kutatuliwa tukijapanga na tukiongeza ‘ubunifu’. Hili haliwezi kutufanya kufuta mfumo huu.
Lingine linalotufanye tuone ni ‘uwoga’ wa kisiasa na kupungua kwa ubunifu ni hili la Mheshimiwa Njwayo.Mbunge Juma Abdalah Njwayo alichomewa nyumba yake mwaka juzi kisa alikuwa anatetea mfumo huu,leo hii ‘amebadilika’ hautaki kabisa!Nini kinamfanya mbunge huyu kubadilika ghafla namna hii? Ni kweli kuwa stakabadhi ghalani haifai na ni mfumo wa kinyonyaji kama anavyodai Mheshimiwa Dastan Mkapa?
Hatumaanishi kuwa Mheshimiwa Mbunge Juma Njwayo hakupaswa kubadilika, la hasha, ‘flexibility’ inakubalika katika nadharia za ‘kioungozi’ hasa baada ya kuona mapungufu ya kile ulichokuwa unaamni. Ila nadharia hii ya ‘kubadilika’ kimtizamo imejikita katika kutafuta ‘ukweli’ kabla ya kubadilka.
Hapa hatuzungumzii ukweli wa ‘kisiasa’ eti kwa vile 2010 yaja basi yapasa kusaka imani za wapiga kura. La hasha ni ukweli wa mwenendo wa kibiashara duniani na hasa biashara za mazao na hali ya wakulima wa nchi masikini.
Upinzani kwa mfumo huu wa ununuzi wa korosho haupo bungeni tu. Oktoba mosi mwaka 2007 wakulima wa Tandahimba waliandamana kupinga stakabadhi ghalani. Adnani Mbwana mwenyekiti wa Chama Cha Wakulima wa Korosho Tandahimba alipata hasara ya 1.8 milioni baada ya mikorosho yake kufyekwa.Kisa anaungama katika stakabadhi ghalani!
Naye mwenyekiti wa TANECU, Mbaraka Mjagama ni mhanga wa stakabadhi ghalani kwani nyumba yake ilibomolewa, (soma gazeti la habari leo 22,Oktoba.2007). Wapinga mfumo huu hawakuishia hapo kwani waliongeza kufuri katika maghala ili kudumaza jitihada za kuanza ununuzi wa korosho kupitia mfumo huu.
Mifano inaweza kuwa mingi kwani wanasiasa kama vile katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad naye alijitokeza kupinga mfumo huu soma gazeti la Tanzania Daima, 22.Oktoba. 2007.
Lenye kustaajabisha ni kwamba wakati Tandahimba wanakebehi na kupinga stakabadhi ‘ghalani’ wakulima wa pamba wanauomba kwa udi na uvumba. Wakulima katika wilaya za Getia na Kahama wanapigia chapuo mfumo huu uende katika pamba!
Mtu makini lazima atajiuliza mara mbili kwa nini korosho waupinge, pamba waulilie! Hawa wapamaba nini kinawafanya waulilie? Jibu rahisi ni kwamba wakulima wa pamba wamechoshwa na ‘kuhujumiwa’.
Tunaweka wazi msimamo wetu kwamba upinzani wa sasa wa stakabadhi ghalani ni kupungua kwa ‘ubunifu’ miongoni mwa viongozi wetu na ni dalili za kueneza hofu bila hata kupitia mwenendo mzima wa biashara ya mazao ya kilimo katika Tanzania.
Hivyo basi makala haya itatupia jicho mfumo huu, umuhimu wake kwa wakulima wa nchi hii, chagamoto zake na kushauri nini kifanyike katika siku za baadae ili kuboresha biashara ya mazao katika Tanzania.
Stakabadhi ghalani (warehouse receipt) ni nini?Si mfumo mpya duniani, wataalamu wa historia ya biashara wanabainisha kuwa ulianza katika Mesopotamia, na ulikua na kushamiri katika Marekani katika karne ya kumi na nane. Sheria ya kwanza imara na madhubuti kuhusu stakabadhi ghalani ilipitishwa katika Marekani mwaka 1916.
Asili ya stakabadhi ghalani ni nini?stakabadhi ghalani hutumika hasa katika kilimo, ni mfumo ambao umeibuliwa ili kuweza kupunguza kuyumba kwa bei ya mazao ya kilimo (price volatility) hasa wakati wa mavuno, na kumsababishia mkulima hasara kubwa na umasikini ambao huwa unamzunguka daima dumu.
Kutokana na kukosa bei ya uhakika wa mazao mara zote kilimo kimekuwa hakikopesheki, na hatari ‘risk’ kwa mikopo ya kilimo imekuwa ni kubwa na mara zote benki zimekuwa zikionesha kisogo sekta hii.
Hili likafanya nadharia ya stakabadhi ghalani kuchipuka Duniani nia ikiwa kumpatia mkulima bei yenye kuridhisha.Mara baada ya kusambaratika kwa jumuiya ya Ki-Soviet nchi za Ulaya Mashariki nazo zilijikuta haziwezi tena kulinda wakulima wake. Nchi kama Bulgaria, Kazakhstani, Hangari, Slovakia na Lithuania ni miongoni mwa vinara wa stakabadhi ghalani na wanaitumia huku wakulima wakineemeka.
Pia wakati wa kudorora kwa bei ya mazao ndiyo ulikuwa wakati wa ‘bush buyers’ walanguzi kujipenyeza na kununua kwa ‘lumbesa’ au ‘kangomba’. Nalo hili stakabadhi ghalani imelidhibiti. Taarifa za karibuni zinaonesha kuhimarika kwa ubora wa korosho.
Kimsingi mkulima hupewa hati mara baada ya kuuza mazao yake kwa ushirika, na malipo ya kati ya asilimia 65-70 hufanyika. Na mara zote sehemu iliyobaki hutegemea mauzo yake kwa wafanya biashara wanaonunua; safari hii hawakutani na mkulima bali ushirika, na si tena gunia moja bali ni tani zilizokusanywa pamoja.
Uwezo kwa kujadili bei umeongezeka kutegemeana na ushirika imara. Ila kubwa zaidi ni kwamba hati ya mauzo yaliyo ghalani ni ‘pesa’. Ina nguvu kama ‘negotiable instruments’ kutegemeana na sheria za nchi husika. Katika nchi zilizoendelea stakabadhi inayotolewa na ghala la serikali ndiyo huwa yenyekuaminika zaidi. Benki ya Dunia inasema hadi miaka kumi wakulima wa nchi za Ulaya Mashariki huweka mazao yao ghalani, huku wakiwinda bei nzuri!
Tafiti fulani iliyofanywa katika Tanzania na Zambia inataja wanunuzi wa mazao( bush buyers) hujipatia faida ya 70 asilimia na huku wakitumia gharama za kuhifadhi kwa 25 asimilia ya bei ya kununulia baada ya muda wa miezi miwili tu toka msimu wa mavuno.
Katika Tanzania stakabadhi ghalani imeingia baada ya upembuzi ya kinifu uliofanywa na Taasisi ya Maliasili( Natural Resource Institute) ya Chuo Kikuu cha Greenwich nchini Uingereza. Tafiti hii ilifanyika katika Zambia na Uganda pia katika miaka ya 1990 na kukamilika mwaka 1997.Na mazao ya kujaribia nadharia hii yalianza kama Kahawa na Korosho. Ndipo fuko la Common Fund for Commodities lilipotoa chagizo la kuundwa kwa stakabadhi ghalani na sheria ya kwanza ilikuwa June 2005 ilifikishwa Bungeni (unaweza kutembelea www.nri.org/project)
Msimu wa ununzi wa korosho wa 2007 ulishuhudia kuanza kwa mfumo huu, ikiwa ni kivuli cha kugoma kwa kampuni za kununua korosho zilizokuwa zinanunua chini ya bei ya makubaliano.
Kampuni hizi zilipinga agizo la Rais Jakaya Kikwete, kampuni sita zilinyang’anywa leseni. Hili la kupinga agizo la Rais ni fedheha kwa nchi, na utatuzi wake lazima uwe wa kisayansi na hapo ndipo ‘stakabadhi ghalani’ inachipuka.
Serikali haikuleta mfumo huu kama ubabaishaji tu, la hasha, kwani ni kilio cha wakulima wenyewe dhidi ya uonevu wa kampuni za ununuzi wa korosho, leo hii inatushangaza kusikia kuwa wawakilishi wa wananchi( wabunge) wanataka kuundoa mfumo huu.
Wanataka kuturudisha wapi? Kule tulikotoka, kwa wafanya biashara wahuni na wevi. Hata kidogo.
Lakini lililowazi ni kwamba tumeona kuwa mfumo huu hauna muda mrefu nchini na unalengo la kumlinda mkulima wa Tanzania. Basi yatupasa kutupia jicho hizo changamoto zinazoletwa na wapinzani wa stakabadhi ghalani pia tutatoa maoni yetu jinsi ya kuzikabili na kuona mifano halisi ya mafanikio ya stakabadhi ghalani si Tanzania tu pia katika nchi za Ulaya Mashariki ambako mfumo huu unatumika pia.

No comments: