Sunday, December 20, 2009

Haki inapodumaza ukuaji wa biashara, si haki tena

Katika nchi ‘zinazofaa’ kufanya biashara Duniani Tanzania ni ya 115, kwa mujibu wa rekodi za mwaka jana za Benki ya Dunia. Ni wazi kuwa changamoto hii inasababishwa na mambo mengi ikiwemo hili la kisheria. Tanzania imekuwa ikionekana kuwa ni ‘pagumu’ mno kufanya biashara kwa sababu ya taratibu za kisheria tulizo jiwekea.
Ucheleshwaji wa haki za kisheria imekuwa ni kona moja wapo inayodumaza ukuaji wa biashara katika Tanzania. Tangu nchi kuingia katika mfumo wa uchumi unaoongozwa kwa nguvu za soko, mabadiliko makubwa ya kisheria yamefanywa, na yanaendelea kutekelezwa ikiwemo uanzishwaji wa Mahakama ya Biashara.
Mahakama hii iliyoanzishwa 16, Septemba 1999 kwa msaada wa DANIDA imekuwa ni mwanzo mwema kwa mwenendo wa kutafuta haki za kibiashara katika Tanzania. Makala haya haitajikita katika kona ya kisheria kungalia nini kinatokea huko katika sheria, ila itaangalia masilahi ya kibiashara kwa hatima ya wajasiramali ambao nchi inajitahidi kuwaibua na siku zao zijazao za ukuaji wa biashara kwa Tanzania.
Katika ukanda wa Afrika Mashariki Tanzania inaendelea ‘kuchanua’ kwa ukuaji wa uwekezaji wa mitaji toka nje. Ni wazi kuwa kiu ya mwekezaji yoyote awe wa ndani au wa nje ni kuona kuwa lengo kuu la mtaji linafikiwa. Nalo ni faida.
Ili kufikia dhima hii ‘muda’ ni suala la muhimu. Hakuna biashara isiyoendana na muda kwani hiki ni kiungo muhimu katika ya wateja na mzalishaji bila kujali muda ni wazi kuwa ‘utawachefua’ wateja wako.
Mwanamuziki wa kizaki kipya Farid Kubanda, Fid Q, katika mashairi ya wimbo wa ‘Fid Q’ anaweka wazi kuwa….muda si rafiki wa mwandamu’.Ni muhimu kukimbizana na adui muda katika heka heka za kila siku.Na mara zote ukiachwa nyuma na muda ni majuto, ndiyo maana tunasema kuwa si rafiki wa mwanadamu kwa vile matokeo yake ni ‘mabaya’.
Vivyo hivyo mteja wa mahakama anapopeleka shauri lake mahakamani anategemea kupata suluhu ya suala lake kwa haraka ili akimbizane na muda
Tanzania mambo ni kinyume chake. Wakili na Mkuu wa Idara ya Sheria ya Benki ya NBC 1997 Ltd, Felix Kibodya, anakadiria kuwa kuna zaidi ya bilioni 100 za kitanzania zimekwama katika mikono ya kisheria kwa kesi zilizofunguliwa muda ‘mrefu’ mahakamani.
Hasara inayotokana na kucheleshwa kwa haki mahakamni katika Tanzania haijawahi bado kuwekwa katika tarakimu, na inakadiriwa mara nyingi shauri uchukua kati ya wastani wa miaka 3 na zaidi.
Bilioni 100 ni pesa nyingi sana, niwazi kuwa biashara zilizoathiriwa na ucheleshwaji wa kesi mahakamani ‘zinachechemea’ na kama si kufa kabisa. Unapokuwa na ‘fungu’ kubwa kama hili halizunguki katika mfumo uliowazi wa kibiashara ni wazi kuwa tunayo yaona ni wazi kuwa ni matokeo ya ‘uzubavu’ huu.
Hili la uchelewashaji wa haki nalo linaonekana kuwa kikwazo kwa taasisi za kifedha kukopesha wajasiriamali. Asilimia 4 ya wajasiriamali ndiyo wanaofaidi na mikopo.

Ni wazi kuwa kunauhusiano kati ya taasisi iliyo na kesi nyingi na fedha nyingi zimedumaa kwa kusubiria haki kuwa itapunguza utoaji wa mikopo kwa wateja na hata kuweka masharti magumu.

Mahakama ya Biasahra ilipoanzishwa mwaka 1999, kesi 116 zilifunguliwa, huku Taasisi za kifedha zikiwa ndiyo wateja wakubwa. CRDB pekee ilikuwa na kesi 18. Tunachoweza kujionea ni kuwa kesi zipo nyingi zenye muelekeo wa kibiashara na zitaendelea kufunguliwa mahakamani.
Hapa isieleke kuwa Mahakama ya Bishara haikuwa na kasi katika kupatia suluhu ya baadhi ya mashitaka yaliyo mbele yake. La hasha, takwimu zinaonesha mwaka 2001 kesi 301 zilifunguliwa, 227 zilipatiwa ufumbuzi, 2002 kesi 351 ziliripotiwa na suluhu kwa kesi 243.
Mabadilko ya kisheria ya mwaka 2002 iliifanya mahakama hii kupopekea kesi chache mwaka 2003, kesi 153 tu zilifunguliwa na hoja 242 zilipatiwa suluhu ukijumlisha na ‘viporo’.
Upungufu huu wa kesi ulitokana na mabadilko ya sheria ambayo yalihitaji mashitaka yawe na thamani ya milioni 100 na kuendelea ili uweze kufungua kesi katika kanda hii ya Mahakama.
Kutokana na mabadiliko haya ni wazi kuwa zile zote zilizo chini ya milioni 100 zimelundikana katika makahama za mwanzo na wilaya.
Jitihada za wazi za muhimili huu wa dola wa kuongeza ajira za mahakimu ni za kupongezwa.
Lakini tunahitaji kwenda mbele zaidi na hasa katika kesi za biashara. Kwani muda hausubiri na ni wazi kuwa wajasiriamali wataathirika kwa kukosa haki kwa wakati.
Bilioni 100 ‘kukukaa’ bila kuzunguka ni hatari kwa ukuaji wa biashara katika Tanzania.
Hakuna ajuaye athari za muuza mahindi aliye na kesi mahakamani kwa kukosa mahindi zaidi ya yeye na familia yake. Kidhibiti kinakaa hadi kinaoza wakati kimeshaonekana!Kwa nini kisiuzwe, pesa ikapunguza maumivu kwa mshindi baadaye.

Biashara inahitaji haki kupatikana kwa haraka, ni vyema tukaimarisha mhimili huu wa dola kwa maendeleo ya sekta ya biashara ya Tanzania.
Kucheleweshwa kwa haki kibiashara hakuna mwisho mwema kwa taasisi za kifedha wala ‘mjasiriamali’. Ni vema tukajipanga kuondoa kero ya kuchelewa kwa haki mahakami kwa nia njema.
Jaji Mkuu, Augustino Ramadhani ameliweka wazi hili kuwa ufinyu wa bajeti ni kikwazo kwa sekta hii kuhakikisha haki inapatikan kwa watanzania. Ni wazi kuwa hili linaathiri ukuaji wa mitaji na biashara kwa wajasiriamali katika Tanzania.
Ni vema hili tukalikabili kama nchi na kwa maajaliwa ya uchumi wa nchi yetu.

No comments: