Saturday, December 26, 2009

Vyombo vya habari na matangazo ya biashara ya elimu feki

Biashara ya elimu ‘feki’ ama kwa kiingereza‘diploma/degree mills’ inaendelea kushamiri Duniani.Hili ni tatizo la Ulimwengu, huku wadadidi wa mambo ya biashara ya Elimu wakikadiria kuwa zaidi ya karne sasa Ulimwengu unasumbuliwa na kansa hii.

Nini maana ya ‘Diploma mills’ hii ni taasisi iliyokuwa tayari kukupa hati ya kielimu bila hata ‘kisomo’ au kuingia darasani. Tafsiri hii inatia ndani pia hata kama ukawa unahudhuria na testi umefanya na kufaulu kwa viwango vya taasisi yako lakini ‘doa’ ni kwamba hautambuliki.

Katika zama za mawasilinao ya ‘kompyuta’ ambapo mtu anaweza kufyatua vyeti na kuthibitisha kuwa na taaluma husika kwa ngazi ya shahada ya kwanza, ya uzamili au Uzamivu(PhD) biashara hii imekuwa kwa kasi mno. Watu wengi ama kwa kufahamu au kutofahamu wamejikuta wakiingia katika mkumbo wa kupata shahada feki.

Ulimwengu unahangaika, watu maarufu na viopngozi wa umma na taasisi zake wako bega kwa bega kupiga vita ‘elimu feki’. Mwa mfalme Prince Charles, amewahi kukemea suala hili na kutaka juhudi za wazi zichukuliwe ili kudhibiti hali hii.
Tanzania ya leo inasukwasukwa na wimbi la upatikanaji wa wataalamu wenye vyeti feki.

Pamoja na tahadhari zinazotolewa juu ya hatari ya shahada ‘feki’ lakini la kustaajabisha ni kwamba idadi ya watu wanaopata na kununua elimu hii inaongezeka, FBI na Interpol wanaweka wazi kuwa biashara hii inashamirishwa na wateja wenyewe.

Katika Amerika sheria za majimbo zinajaribu kukaba, na kupambana vilivyo na hali hii, lakini yatupasa kufahamu kuwa kabla hatujasema chuo fulani kuwa kuna vyuo vimenyagwanywa ‘hadhi’ katika ya safari baada ya kubainika kuwa mchezo wao si mwea kitaaluma.

Kutotambulika ni hasa pale unapotaka kujiendeleza, mathalani umefanya elimu kwa ngazi ya cheti kwa elimu ya kompyuta kwenye chuo fulani pale ‘Kariakoo’. Cheti hiki kama hakikupi kinga ya kujiendeleza kielimu kwa ngazi ya Diploma ya elimu ya kompyuta katika vyuo makini, kama vile UDSM, IFM! Ni wazi kuwa chuo ulichosoma ni ‘feki’.

Biashara hii imekuwa ikishamiri na kwa kiasi kikubwa ingawa hakuna takwimu sahihi lakini kuwepo kwa wahitimu hao ni dalili ya wazi, pia kuongezeka kwa vyuo vyenyewe ni mwanga tosha kuwa biashara yao ina wateja. Mafanikio haya yamechangiwa na vyombo vya habari pia sekta binafsi kwa kukubali wahitimu wa vyuo hivi.

Magazeti makubwa kama Forbes, Herald, the Economist yamekuwa yakitoa matangazao ya vyuo hivi ingawa yanaelewa ni njia maoja wapo ya kushamirisha ‘dploma mills’. Mara zote wahariri wanapoulizwa kuhusu, mustakabili wa wao kukubali kutoa matangazo ya vyuo ‘bomu’.Hudai kuwa wasomaji wao ni watu makini na wanajuanini wanachokifanya kwa hivyo ni jukumu la wateja kujikinga.

Safari hii mteja hana msaada na amekuwa daraja la watu kujipatia utajiri. Katika Tanzania magazeti yetu na TV za umma na binafsi vinashindana kutangaza vyuo ambavyo havitambuliki na NACTE, VETA wala TCU kwa taaluma wanazotoa.

‘Intake’ ya Januari inakuja kwa vyuo vingi vya Ulaya, Amerika na Asia Kusini. Ni wazi kuwa usipokuwa makini utajikuta umeingia katika ‘gogoro’ la kusoma chuo feki.

Makala haya itajaribu kutoa mbinu chache ili uweze kujinasua na mtego wa kuingia gharama za kusoma chuo kisichotambulika.

Mosi ni vyema kufuatilia kila wakati ilikujua mwenendo wa Chuo chako ukoje .Je kinaendelea kutambulika au kimeingizwa katika mkumbo wa vyuo feki?Na hasa unapoenda kusoma Vyuo binafsi nje ya Tanzania.

Kwa mfano Chuo cha Pacific Western University (PWU) ni chuo kilichoanzishwa mwaka 1977, kikiwa na wasomi wengi hodari na walioweza kufikia katika ngazi ya U-profesa na wengine Marais wakiwa wanaheshimika na taasisi kubwa kama IFM na Benki ya Dunia.

Profesa Bingu wa Mutharika, PhD yake ya ‘Development Economics’ kaisomea PWU, mwaka 1984 (fuatilia htt://www.un.org/ecosoc/docs/pdfs/Mutharika.bio.pdf.)

Chuo hiki kilikuja kupoteza hadhi yake pale kilipotoa PhD ya miezi 12!Katika 2006 kwa mmoja kati ya wakurugenzi wa Taasisi ya Marie Currie, taasisi yenye kuheshimika sana Duniani.

Hii haimaanishi kuwa PhD ya Mheshimiwa Rais Bingu wa Mutharika ni feki, hapana kwani Chuo kilipoteza hadhi wakati yeye keshamaliza. Tunachosema hapa ni mwamba yakupasa kufuatilia mwenendo wa shule yako mara kwa mara.

Ni wazi kuwa katika mfumo wa soko huria ukaona kuna rafiki yako ambaye amesoma chuo ‘feki’ akiwa ameajiriwa katika taasisi binafsi. Hili lipo sana, vyeti hivi vinakumbana na ‘kigingi’ pale vinapojaribu kupenya katika taasisi za ‘serikali’Fulani kasoma pale haitakusaidia sana. Utawezaje kutambua kuwa shahada hii au chuo changu ni feki?

Tumeshaonesha hapo juu kuwa, biashara ya Ulimwengu ya vyeti feki inashamirishwa na vyombo vya habari hasa TV, magazeti redio tena ni vyombo vinavyoheshimika.

Chukulia mfano Chuo A unakikuta kinatangaza nafasi za masomo katika gazeti la The Economist, hadhi ya hicho chuo utakichukuliaje?Ni wazi kuwa unaweza ukanasa katika mtego huo.Vivyo hivyo magazeti ya nyumbani kunayanayoshamirisha elimu feki.

Ukiona chuo chako kinatoa elimu chini ya muda uliozoeleka, diploma ya miezi ya sita, PhD ya miezi 12, hapa anza kuwa na shaka!

Fuatilia kama chuo kimesajiliwa na kinatambulika kweli.Tahadhari kuwepo kwa utambulisho kutoka kwa wahusika kunaweza kukupumbuza. Mara nyingi wanatumia nembo za ithibati za kitapeli ambazo wala nazo hazitambuliki.
Kwani mara zote vyuo hivi feki vimekuwa vikijinadi kwa kuweka nembo na ithibati zenye kuthibitishika lakini ukweli wa mambo ni ‘waongo’. Yakupasa kutembelea tovuti za nchi husika za elimu. Na kama unaweza tembelea balozi ya nchi husika kwa taarifa za awali.

Kwa Tanzania kuna taasisi zinazojihusisha na mwenendo mzima wa kuratibu elimu, kuna VETA, NACTE na TCU ni vyema ukatembelea tovuti zao, ama kubisha hodi katika ofisi zao kabla hata hujalipa ada.

Ada pia inaweza kuwa kigezo cha kukustua pia. Vyuo bora na vyenye kuheshimika katika Uingereza kwa mfano kwa ‘elimu’ za kijamii vinaanzia na ada ya paundi 8,500 kwa mwaka kwa wanafunzi wa kimataifa. Ukikuta chini ya hapo, weka shaka!

Hatutaki kusema kuwa bei ndiyo kigezo muhimu lakini pia elimu bora siku hizi inahitaji pia gharama hasa kwa elimu za magharibi. Profesa atakaye fundisha mwanafunzi wa cheti, atafundisha pia kwa PhD na amshahara wake uko pale pale hivyo ada itakuwa juu kwa cheti pia.

Kuwa makini na vyuo vya binafsi. Katika Ulaya na Marekani vyuo vingi vya umma vina majina ya miji husika. Sasa unapokwenda katika vyuo ambavyo vinamajina matamu ya watu, jaribu kutia shaka. Ni wazi kuwa yakupasa kutoamini kila kitu, na hasa siku hizi za utapeli wa kielimu.

Chukua tahadhari na vyuo vinavyotofautiana herufi. Hapa namaanisha kwamba kuna vyuo vinajaribu ‘kukopi’ sasa tofauti ni ndogo tu unaweza kuingia katika mtego wa elimu feki. Kwa mfano Greenwich University hiki ni feki, halisi ni University of Greenwich. Wamecheza na maneno. London School of what what, hawa ni jamaa wanaoiga ukongwe wa London School of Economics kuwa makini!

Kama unaenda kusoma Marekani ni vyema ukatembelea tovuti ya www.edu.gov, huku utakuta mwenendo mzima wa vyuo feki na vyenye hadhi na ‘wameposti’ ili ukasome kwa heri katika vyuo vyenye heshima na thamani ya pesa yako.

Epuka mtego wa taasisi za kidini zinazoendesha vyuo vikuu na hasa Marekani.Taasisi hizi zimeruhusiwa kutoa shahada za elimu za dini, lakini inapokuja kuwa wanatoa shahada nyingine kuwa makini na vyuo hivyo. Vingi ya vyuo hivi vinaanzishwa baada ya kanisa kufunguliwa na ndani ya wiki mbili wanaleta PhD sokoni tofauti na elimu ya dini.
Mara nyingi Serikali ya Marekani imeshindwa kuvibana vyuo hivi lakini ukweli wa mambo vingi havina hadhi.
.
Mapambano ya elimu feki, diploma za miezi sita na PhD za miezi 12 ni vita ya jamii nzima. Vyombo vya habari Tanzania vina nafasi ya kusitisha kukua kwa biashara hii, pasi kujali faida kwao tu, bali pia kujali masilahi ya Tanzania.
Vyombo vya habari kwa sasa vinaangali nani ana elimu feki tu, lakini wao kimsingi wanachangia vijana wa kitanzania kuingia katika mkumbo huo kwa kukubali kutoa matangazo haya.
Matangazo ya vyuo vya Ulaya, Marekani na Asia kusini yamejaa kweli kweli katika magazeti ya Tanzania. Hakuna anayejiuliza kama kweli vyuo hivyo vina hadhi na ithibati katika mfumo wa elimu ya Tanzania.
Tupo kimya. Yatupasa kubadilika, na kubadilika ni kukataa matangazo ya vyuo feki pia katika magazeti yetu. Na si kusubiri wasome wakirudi ndiyo tuanze kuwashambulia.

Hili la kukataa matangazo ya vyuo feki tunaweza, ni vyema tukilifanyi

No comments: