Saturday, December 12, 2009

SEKTA BINAFSI NA MAJAALIWA YA TANZANIA

Kwa zaidi ya miongo miwili sasa serikali ya Tanzania inajitahidi kila iwezalo kuhimarisha sekta binafasi. Mageuzi ya kiuchumi na mifumo ya kisheria na kiutendaji inafanyika katika kuhakikisha kuwa sekta hii ambayo ni mwajiri mkubwa kwa sasa inkuwa. Kwa hakika sekta binafsi ndiyo muajiri, ndiyo muongozaji wa uchumi wa Tanzania.
Kukua kwa biashara yoyote kinadharia inahitaji kuwepo kwa kuaminiana (trust) kati ya mteja na mtoa huduma bila kusahau kuwa masilahi ya jamii husika yanalindwa. Na hili linatokea hata muuzaji akakupa mzigo wa mamilioni ya shilingi bila hata kusainishana, akiwa na tumaini kuwa utarejesha stahiki yake.
Kuaminiana ndiyo biashara ya leo ya ulimwengu, jaribu kufikira mtu anayenunua gari toka Japan akiwa Nakapanya Masasi kwa kutumia ‘internet’ ameona tu picha na maelezo ya kampuni husika akaamini na kutuma fedha bila ‘woga’ Japan bila hata kusani mkataba akanunua gari akiamini kuwa litatumwa.
Ujenzi wa imani si kazi ya siku moja katika biashara, ni mfululizo wa matukio na utendaji ndiyo yanayoimarisha mawazo ya mteja na kuhisi kuwa analindwa na kuthaminiwa na kampuni husika. Kimsingi zinatia ndani hata kampuni zenyewe zinajiendashaje, kampuni yenye madeni na kesi nyungi mahakamani za kushitakiwa ni wazi kuwa inapoteza imani za wateja.
Wateja wa sekta binafsi katika Tanzania ni watanzania, ambao wamegawanyika katika makundi mawili wateja wa nje(walaji) na wandani (wafanyakazi).Katika Tanzania sekta binafsi pia inaendesha shughuli ambazo zamani zilikuwa zinafanywa na serikali, kama kukusanya kodi, kusanya taka, kuendesha harambee, kutuo elimu mifano inaweza kuwa mingi. Lakini lililowazi ni kwamba sekta hii imechukua nafasi kubwa ya serikali katika maeneo mengi ya kiuchumi katika Tanzania.
Muunganiko huu unatufanya tuone kuwa suala la maendeleo si tena kitu cha ‘kuhodhiwa’ na serikali. Lengo kuu ni kufanikisha maendeleo kwa mtanzania. Swali ni, je mandeleo haya yatapatikana au ni ndoto tu?
Ni muunganiko unaoonesha kuwa bila kudhibitiwa hautakuwa na mwisho mwema. Matokeo mengi yanayotokea sasa katika uchumi wa Tanzania yanatufanya tujiulize hivi kweli sekta binafsi ni mkombozi au kitanzi?
Serikali kwa nia njema inashamirisha sekta hii, kuanzia miaka ya 1990. Uhusiano huu kati ya serikali na sekta binafsi (Public-Private Sector Partinership) kuna maeneo yanatupa wasi wasi!
Hivi karibuni kuliripotiwa kufutwa kwa mkataba wa kukusanya kodi katika ‘stand’ ya ubungo kwa kampuni ya Smart Holdings. Kampuni hii ilikuwa inadai inakusanya milioni moja kwa siku, lakini serikali kupitia Jiji la Dar-es-Salaam leo hii inakusanya milioni 4 kwa siku!
Smart Holdings ‘imeonekana’ tena katika jengo jipya la Machinga Complex kama msimamizi wa makusanyo, wa Jengo hilo. Na taarifa za awali zinaonesha wafanya biashara kupitia umoja wao wameikataa ‘SMART’. Hii ni fedheha.Lakini linalotia uchungu ni taarifa za kukataliwa kwa kampuni iliyoonesha kuwa inaweza kuleta pato la bilioni 1.2!
Lengo ni kupata fedha kwa ajili ya maendeleo vip tena tunakataa dau kubwa tunakubali dogo?Inawezekana ikawa aliyeleta dau kubwa ametia ‘chumvi’ hesabu zake, lakini hili halina nguvu sana katika biashara.
Sekta binafsi inaonekana wazi kuwa ni kichaka cha watu wachache kuja kufaidi jasho la walio wengi bila hata tija kwa pato wanalochuma. Kimsingi huu ni mwanguko wa maadili ya biashara.
Ni wazi kuwa hakuna maadili ya biashara kama hakuna maadili ya umma au ya kijamii. Mwenyekiti wa Jengo la Machinga Complex Iddi Azzan ‘Zungu’ mbunge wa Ilala amekaririwa akiweka wazi kuwa hata kabla jengo halijakamilika kampuni hii imepewa kazi hiyo ya kukusanya ushuru, na lenye kuumiza zaidi bila hata vikao halali vya ‘tenda’ kuketi.Sasa walijuaje kuwa kuna mshindani aliyeleta ‘dau’ bilioni 1.2 amekataliwa!Lisemwalo lipo waswahili wanasema.
Hii ndiyo Tanzania ya leo. Mwenendo kama huu wa kampuni kupewa kazi bila hata vikao halali katika Tanzania umeonekana maeno mengi na hasa katika wilaya. Kuna watu wanakampuni nyingi za mifukoni wakijipa ‘tenda’ za kuendesha kazi za serikali kwa manufaa ya umma lakini hata uwajibikaji hawana.
Hapa ndipo tunapojiuliza majaaliwa ya Tanzania katika nyakati zama za sekta binafsi, wapi sekta hii inatupekela?Isielweke kuwa hatuitaki sekta binafsi ila tunahitaji ‘mbinyo’ (regulations) zaidi katika kuongoza sekta hii kwa manufaa ya watanzania wote.
Sekta binafsi imekuwa ni watu wenye kulia sana kuomba misamaha ya kodi na uwanja huru wa biashara. Lakini lenye kutia hofu ni juu ya mwenendo mzima wa sekta hii hasa katika kulinda na kujali masilahi ya watanzaia.
Matukio ya rushwa na kuongezeka kwa vitendo visivyo vya maadili vimekuwa ni vitu vya kawaida katika mazingira ya biashara ya Tanzania.Hupati akzi kama huna ‘ten percent’ Wakati umefika wa watu walio katika sekta binafsi kujiangalia mara mbili, wanahitaji kuendesha sekta hii kwa manufaa ya Taifa au ni kwa uroho wa kujilimbikizia mali na kuwaacha watanzania wakiwa watumwa daima dumu.
Mpaka leo sekta binafsi inakaata kuongeza mishahara mipya kwa uajanja wa ujanja wa vikao visivyo kwisha. Kuendesha uchumi si kwa ‘maumivu’ ya wafanyakazi. Ni kwa masilahi ya wadau wote. Kampuni inapata faida ya bilioni 26 baada ya kulipa kodi, ‘bonus’ ya mwaka ikitoka kuna wafanyakazi wanapata 2000/= kampuni yenye wafanyakazi 600 tu.
Waziri Mkuu Mizengo Kayanza Pinda hivi karibuni amekaririwa na gazeti moja la kila wiki akiikemea kampuni moja ya Kichina inayojenga barabara ya Arusha hadi Namanga kuwa ulipaji wao wa mishahara midogo ndiyo chanzo cha kukosa wafanya kazi wenye sifa. Kwa hakika hii ndiyo sifa ya sekta binafsi, ni mishahara midogo na malipo ya ‘kujuana’ wanasema huna ‘address utaishia hapo hapo’.
Yanayotendeka huko yanatia uchungu, rafiki yangu yupo katika kampuni moja ananiambia kuwa alikuwa anaongozwa na meneja wa kidato cha nne, naye alikuwa analipwa mshahara mkubwa kuliko yeye ‘graduate’ .
Kampuni zingine zinaheshimika katika Tanzania lakini utakuta watu wake ni ‘vihiyo’ na wanalipwa pesa nyingi ili kuwavunja moyo wahitimu wenye sifa. Mwenendo huu hauna mwisho mwema kwa biashara ya Tanzania na sekta yenyewe kwa ujuma. Kwani mfanyakazi asiyepata motisha hawezi kuwa ‘mbunifu’
Sekta hii kiuchumi ni muhimu lakini tunahitaji kuiangalia mara mbili na kutunga sheria na taratibu zinazoendesha sekta hii kwa uwazi kutoka katika ajira zake, mishahara, marupurupu na stahiki zingine na si kuacha kila kitu kiendeshwe na wao kama wanavyopenda.
Kama wanahitaji misamaha ya kodi ni lazima nao pia waoneshe jinsi wanavyojali wafanyakazi wao na si kupata misamaha huku wakilipa mishahara inayodhalilisha wazawa huku wageni wakilipwa mishahara minono bila tena hata sifa za kielemu kwa nafasi wanaozishikilia.
Hakuna nchi duniani iliyojengwa na wageni wala na watu watoa rushwa na wasiopend maadili. Ni wazi kuwa kiu yetu na matumaini yetu ya kuona sekta binafsi inatupeleka katika nchi ya ‘asali na maziwa’ haitakuwa na maana kama sekta hii itakuwa inaendesha mambo yake kwa stahili ya sasa.
Tujenge mwenendo wa kuaminiana kukosa imani kwa wateja na kukataa kampuni ni wazi kuwa hili ni doa kwa sekta binafsi. Basi yatupasa kujenga imani za wateja kwa vitendo na si ubabaishaji wala rushwa havina mwisho mwema.

No comments: