Monday, March 1, 2010

Wakulima wadogo masikini watakombolewa na ‘fair trade’?

Ni mashamsham ya maazimisho ya wiki mbili ya kuhamasisha ‘fair trade’ katika nchi za Ulaya na Marekani kwa zaidi ya siku kumi na nne, toka Februari 22 hadi Machi 3. Miongoni mwa nchi zilizo katika mpango wa Fairtrade ni Uingereza, Ujerumani, Marekani, Japan,Ufaransa, Italia, Uholanzi, kuzitaja kwa uchahe tu. Kimsingi nchi hizi ndiyo masoko ya bidhaa za kilimo na za ubunifu wa mikono zinazotengenezwa katika nchi za Dunia ya tatu zikiingia sokoni kwa nembo ya fair trade.
Fair trade ni nadharia iliyojikita katika ‘utu’ huku ikiwa na msukumo wa kidini na maadili ili kuona wale watu waliomasikini kabisa duniani kutoka nchi masikini wanapata nafasi ya kufaidi jasho linalo tokana na kazi yao.Lengo kuu ni kuhakikisha bidhaa za watu wa kizio cha kusini zinafika katika masoko ya Ulaya na Amerika na wateja wakinunua bidhaa hizo ni wazi kuwa sehemu ya pato hurudi moja kwa moja katika nchi husika kusaidia maendeleo ya watu wa eneo hilo.
Nadharia hii inaweka katika vitendo, kile tunachokiita ‘trade not aid’. Lakini kwa sababu mfumo wa ulimwengu hauko wazi na bei za mazao mara zote zinaporomoka basi wakulima wa kizio cha kusini watapata nafuu, kwa kutoza bei ya juu kwa walaji wa kizio cha kaskazini na ile ziada iliyokuwa zaidi ya soko inakwenda kwa watu walio masikini.
Msukumo wa fair trade katika nchi za magharibi unaanzia katika makanisa, huku zaidi ya makanisa 6000 yakiwa yamejiunga katika mpango huu. Awali nimesema kuwa mpango huu umejikita katika maadili ya kiroho zaidi, na nyumba za ibada na taasisi za kidini na mashirika yao ndiyo yanayoongoza mpango huu wa ukombozi kwa watu wa kizio cha kusini.
Nguzo kuu ya maadili ya fairtrade yapo katika biblia, methali 13:23’Shamba la masikini hutoa mazao mengi , lakini bila haki hunyakuliwa’. Maneno hayo yamepamba baadhi ya makanisa katika Uingereza yanayojinadi kutumia bidhaa zenye nembo ya fair trade. Kupitia taasisi za kidini na mashirika yake wanaamini walaji wa nchi tajiri inabidi wanunue vitu kwa bei ya juu ili ziada irudi katika nchi asili ambako zao limelimwa ili kusaidia wakulima masikini.
Katika kutekeleza mpango huu njia moja wapo kuwa na chama cha ushirika na wakulima ujiunga pamoja kwa hiyari.Wakulima ni wale walio wadogo chini ya hekari 3 huku wakiwa wanaendesha shughuli zao za kilimo. Ingawa sasa kuna mjadala mkali wa kuangalia nini mantiki ya kutaka wakulima wadogo wapate haki ya kuuza kupitia mpango huu.
Inakadiriwa zaidi ya wakulima 500,000 na vyama vya ushirika 300 vipo katika mpango huu katika kizio cha kusini. Mauzo yanakadiriwa kufikia Euro bilioni 2.4 kwa mwaka jana.
Gazeti la The Independent la tarehe 25 Februari 2008 lilipoti mauzo ya bidhaa za fair trade kufikia paundi milioni 500 kwa Uingereza pekee. Huku idadi kubwa ya kampuni kubwa kama Mark Spencer, Waitrose,ASDA , Morrison na Tesco zikijiunga na kuahidi kuweka bidhaa za fairtrade katika maduka yao.
Fairtrade ni biashara inayovutia sana makampuni makubwa kwa sasa na kifimbo kinaonekana kupokonywa kutoka kwa taasisi za kihiyari kama Oxfarm, Traidcradt, Cafod sasa imekuwa ni biashara pendwa. Huu ni ushahidi wa wazi kuwa watu wengi wameitikia wito wa kununua kwa bei ya juu ili kwenda kusaidia watu masikini wa kizio cha kusini.
Tanzania inatajwa kama nchi ya kwanza kunufaika na mpango huu wa fairtrade, kwa kahawa kutoka Kagera mwaka 1988 kupitia chama cha Ushirika, Kagera Cooperative Union. Mpango huu pia unatumiwa na Kilimanjaro Native Cooperatives (KNCU) kwa kahawa yao kuuzwa Ulaya kupittia mpango huu.
Pia wamiliki wa mashamba ya chai wa Kibena, Iringa Tanzania ni miongozi mwa wafanyakazi wanaonufaika kwa bidhaa zao kufanikiwa kujipenyeza katika masoko ya Ulaya. Pia kuna bidhaa za mikono, zilizopo katika masoko ya Ulaya na Amerika kutoka Tanzania.
Mwenendo wa biashara unaonesha wazi kuzinufaisha nchi za dunia ya tatu. Tanzania kupitia KCU imeweza kuuza asilimia 7 ya kahawa yake yote inayozalisha. Kwa Mujibu ya mtandao wa taasisi ya Fair trade, inabainisha wazi kuwa wakulima wa Kagera wameweza kununua hisa za kiwanda cha Tanica kinachozalisha kahawa kwa asilimia 51.
Kahawa ya Arabica kutoka Afrika imewekwa katika bei ya dola 2.80 kwa Kilo,huku sent 11 dola za kimarekani kama bei ya juu (premium price) kwa kilo ikiwa fedha hii inapaswa kutumika kwa ajili ya maendeleo ya wakulima husika.
Bently W.R na wenzake katika Jarida la kisomi, Sustainable Development toleo 13, 2005 makala waliyoiita ‘What Tanzania’s farmers can teach the world’ wanabainisha kuwa kuna nyongeza ya kipato kwa wakulima wadogo wa kahawa wale walio katika mpango wa Fairtrade kulinganisha ni mifumo mingine .
Mafanikio mengine ni pale KNCU ilipoweza kuwalipia ada wanafunzi wanaokadiriwa kufikia 278, hawa ni wanafunzi wa shule za sekondari za serikali ambao wazazi wao wamefariki kwa ugonjwa wa Ukimwi au wanaoishi katika mazingira magumu.
Profesa Faustin K. Bee katika tafiti ‘Fair trade Fair futures: KNCU scholarship programme for children made vulnerable by AIDS’, 2009 anabaninsha wazi kuwa kipato cha kahawa kinachotokana na fairtrade kimekuwa si cha kuaminika kwa KNCU.Mwaka 2004 ilipatikana milioni 175 mwaka 2008 milioni 105. Majaaliwa ya mipango mizuri yote inawekwa majaribuni!
Haya ni mafanikio makubwa kufikiwa kwa wakulima wadogo waliojiunga chini ya chama cha ushirika. Lakini swali letu linabaki kuwa fairtrade ni mkombozi wa wakulima masikini toka mfumo mbovu wa biashara ya ulimwengu?Lililowazi ni kuwa fairtrade inaendeshwa nje ya nguvu za soko za ‘demand and supply’, kwani mlaji analipa zaidi ya bei ya soko na ziada inakwenda kwa wakulima wa nchi masikini.
Lililowazi kwamba wakulima wa Tanzania bado wanakumbukumbu ya maumivu ya walafi wachahce waliokula mali za ushirika bila kuchukuliwa hatua na safari hii fair trade inahimiza ushirika. Je Fair trade kupitia ushirika tutafikia lengo katika Tanzania, au yale yale?
Walaji wa Ulaya na Amerika hawatakuwa tayari kuona maadili ya utu yanavunjwa huku wao wakilipa bei ya juu kuliko bei ya soko na walafi wakihujumu chumo la fair trade. Ni wazi kuwa watasusa. Jukumu la kusukuma mbele malengo ya fair trade ni wazi kuwa Tanzania kama nchi ina nafasi kubwa ya kushiriki kuhakikisha wakulima wadogo wanalindwa na makucha ya walafi wanaojificha katika ushirika. Shime wenye mamlaka.

No comments: