Monday, January 18, 2010

Ni muda muafaka kuongeza umri wa kustaafu

Majuma machache yaliyopita vyombo vya habari vya Tanzania. vilipambwa na sakata la serikali kumnyima ajira ya mkataba, mwanazuoni nguli wa siasa za kimataifa Profesa Mwesiga Baregu wa Chuo Kikuu cha Dar-Es-Salaam (UDSM).
Waziri mwenye dhamana, Mheshimiwa Hawa Abdulreihman Ghasia, aliweka wazi kuwa serikali kwa sasa haina nia ya kumpa mkataba mpya Profesa Baregu, baada ya kumpatia mara tatu tangu alipostaafu mwaka 1999, akiwa na miaka 55.
Tangu suala la kunyimwa mkataba kwa nguli huyu lilipoibuliwa katika vyombo vya habari, kuna makundi mawili makubwa yameibuka katika kuangalia, uhalali wa kama Profesa ameonewa au serikali ipo sahihi kusitisha kumpa mkataba.
Kuna waliojikita katika itikadi za kisiasa, ingawa waziri pia amegusia hilo kuwa ndiyo kiini cha kusitisha mkataba mpya kwa gwiji huyu. Lakini kuna madai kuwa wapo wana CCM mbona wamepata, wakienda mbali zaidi wakihusisha ukosoaji wake kwa serikali kuwa ndiyo kigingi cha yeye kutemwa UDSM.
Kichuguu cha pili kilikuwa na wale wanaoona kuwa maamuzi haya ni sahihi ingawa hawa hawakupata nafasi ya kuhojiwa sana na vyombo vya habari, huku wakiweka wazi kuwa sasa huu ni wakati wa damu changa kuchukua nafasi katika taasisi mbalimbali za serikali.

Makala haya haina nia ya kusema kati ya hivyo vichuguu viwili na hoja zao kipi kipo sahihi au yupi amekosea, la hasha ila itajaribu kupitia umuhimmu wa kuangalia nini tunajifunza kama 'nchi' kuhusu sakata hili, la Profesa Baregu.Serikali imekwisha hitimisha.

Somo tunalotaka kulijadili katika makala haya ni kuhusu umri wa kustaafu katika Tanzania.Na hasa kwa wanazuoni au wataalamu wengine ambao serikali hutumia gharama kubwa kuwasomesha.

Naweka wazi msimamo wangu kuwa umri wa kustaafu unapaswa kuongezwa na hasa katika kada za walimu wa vyuo vikuu. Kwa sasa kuna wanaostaafu katika 55 na wengine 60 kwa manufaa ya umma.

Ulimwengu wa leo watu wengi wananafasi kubwa yakuishi maisha marefu hii ni kutokana na mafanikio ya kisayansi ambayo yameweza kuboresha viwango vya ubora wa maisha kwa wale wanaozingatia na kufuatilia kwa ukaribu. Magonjwa ambayo yalikuwa tishio si tena tishio kwa binadamu.

Pia mafanikio ya kisayansi yanampa nafasi binadamu kuweza kufanya kazi kwa muda mrefu, wakati zamani miaka 55, ni umri uliokuwa kweli umechoka kweli kweli. Mfano Mzuri ni huyo Profesa, tangu astaafu amepewa mikataba mitatu na bado yu mwenye siha nzuri na anaonekana anaweza kumudu mikiki mikiki ya kazi yake.

Katika Tanzania, kustaafu katika miaka chini ya 65 ni pigo kwa nchi na hasa wahadhiri ambao wengi leo hii tulionao wako mbioni kustaafu, vyuo vingi vinakabiliwa na hatari ya kukosa hawa magwiji katika miaka mitano ijayo.

Inakadiriwa katika miaka mitano ijayo wengi ya wanataaluma waliobobea katika shahada za uzamivu watakuwa wamestaafu wakiwa na umri wa miaka 60. Kimsingi hii ni hasara kwa nchi.

Hasara kwa sababu, wengi ya wanazuoni tulionao wamapata PhD wakiwa na zaidi ya miaka 45 hadi 50. Sasa ukiangalia gharama za kumsomesha mwanafunzi wa PhD alafu anatumika chini ya miaka 10 anastaafu ni nchi ndiyo inapata hasara.

Hili suala la kuomba kuongeza muda wa kustaafu walau ufikie miaka 65 si jambo geni, na wala siyo hoja mpya katika Tanzania.Kati ya watu wanaopigia chapuo kuongezwa kwa umri wa kustaafu ni Balozi Juma Mwapachu, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Sisi tumechelewa kusoma, na mifumo yetu mara nyingi inatubana kupata wanazuoni walio na umri chini ya miaka 30 wakiwa na PhD. labda katika miaka 10 ijayo tutakuwa na watanzania walio na PhD wakiwa chini ya 30 hii baada ya serikali ya awamu ya tatu kuhimiza kupeleka watoto shule mapema.

Na ujio wa shule binafsi umefungua mwanya kwa vijana wa kitanzania kwenda shule wakiwa na wastani wa miaka 4 hadi 6 kuanza darasa la kwanza huku wakirushwa baadhi ya madarasa, hasa la saba na wangine wakitumia elimu ya nje kama Kenya na Uganda kusonga mbele katika vyuo vikuu vya huko.

Ila kwa wale tuliosoma Tanzania ni wazi kuwa kupata PhD si chini ya miaka 45, na kupata Uprofesa kama ngazi ya juu ya kielimu katika kufundisha inaweza kuchukua zaidi ya miaka 10 kwa Tanzania.Ukijumlisha na uchelevu wa kwenda shule huko nyuma wengi wanakuwa maprofesa bado miaka michache kustaafu. Hawa ndiyo magwiji walioiva.

Sasa kwa nini wameiva sasa, ndiyo tunawapa taarifa ya kusataafu!Hapa pana ulakini.Katika nchi za magharibi kustaafu ni miaka 65, na wengi huku wamepata PhD wakiwa chini ya miaka 25. Hivyo anaitumikia nchi yake kwa zaidi ya 30.

Ni wazi kuwa atarudisha fedha ya walipa kodi kwa kazi atakayoifanyia nchi yake.
Hasara yake ni kwamba wakati tumetumia pesa nyingi kuwasomesha katika vyuo vya nchi za magharibi kwa gharama zisizopungua milioni 100 kwa mtu mmoja kwa PhD tunamtumia chini ya miaka 10,kwa vile tu sheria inasema astaafu chini ya miaka 65!

Pesa nyingine zinakuja kama mikopo, hivyo hata mkopo haujalipwa na mtu hajaitumikia jamii yake anaambimwa astaafu kwa manufaa ya umma.

Ni sheria inapaswa kufuatwa. Lakini sheria hii kwa mmtazamo wangu nahisi ina matatizo na hasa kwa nchi yetu hii changa. Mbona Uingereza wanastaafu wakiwa na miaka 65.

Lengo kuu la sheria au taratibu za jamii yoyote ni kuwatumia jamii husika, sasa sheria hii inaonekana haina manufaa kwetu yatupasa kuijadili na kutafuta suluhu ya kudumu.

Rai yetu ni kwamba huu ni wakati muafaka wa kufikiria kuongeza kwa umri wa kustaafu iwe kwa hiyari au kwa manufaa ya umma umri uwe miaka 65.

No comments: