Sunday, January 3, 2010

Tuwalinde watoto na matangazo ya 'Junk' food

Tafiti fulani iliyofanyika katika mkoa wa Morogoro kuhusu afya na ulaji, ilibaini watu wazima wenye umri kati ya 45-51 wanakabiliwa na hatari ya unene kwa asilimia 45.5. Hali ni mbaya kwa watoto, hasa kwa vile wanakula kula hovyo juisi na ubuyu kwa nyakati tofauti wakiwa nje ya mikono ya wazazi.
Unene ni hatari inayoinyemelea Tanzania, na ndiyo maana ongezeko la magonjwa ya ‘shinikizo’ la damu, kisukari imemekuwa ni hali ya kawaida. Kisukari sasa kinasumbua watoto wadogo. Haya ni magonjwa yatokanayo na ‘ulaji wa vyakula hatari' pia.Kliniki za kisukari zinachipua kila mahali, hali ambayo haikuwa kawaida katika muongo mmoja na nusu hivi.
Obesity( Unene usio na tija) ingawa ni vigumu kutambua chanzo chake kama vile ni sababu za kibailojia au mabadilko ya kimazingira. Lililowazi ni kwamba mifumo ya maisha ya siku za leo huchangia sana.
Tafsiri rahisi ni ya ‘unene’ ni kuwa tumekula zaidi ya mahitaji halisi ya miili yetu katika chakula husika katika kufanya kazi. Wadadisi wa mambo wanadai katika India kuna zaidi ya asilimia 10 ya watoto wanaohitaji kushona nguo kwa vitambaa vya watu sita wa umri wao!
Hili kwa sasa ni hangaiko la Ulimwengu, na hasa katika nchi zilizoendelea kila nchi inajitahidi kupambana vilivyo ili kulinda jamii ya watu wake. Inakadiriwa hadi kufikia 2015 kama hali itaendelea kama ilivyo Uingereza itahitaji paundi bilioni 50 kutibu magojwa yatokanayo na unene unaosababishwa na ulaji.
Katika Tanzania tabala la kati ‘linachapua’ kila siku, tabaka hili likiwa na hali ya kipato cha wastani na kuweza kujikimu ndiyo wateja wakubwa wa maduka ya haya ya chakula.Ni vijana hawana muda wa kupika, chakula chao ni ‘fast foods’ na juisi za makopo!
‘Fast Food’ and ‘Take Away’ zinaongezeka katika miji mbalimbali, na lililowazi ni kuwa uangalizi wake haupo wa kutosha.Wanapika nini? Wanapikaje? Hakuna anayejua.
Migahawa haina tatizo, tatizo linakuja namna ya uendeshaji wa migahawa katika nchi zinazoendelea mara zote ni kilio mara baada ya muda mfupi. Kwa mfano waendeshaji wa migawa iliyojaa Sinza wanahitaji elimu ya lishe na afya itolewe, ili wajasiriamali hawa wajue madhara ya chumvi, mafuta na sukari. Hii ni kwa faida ya Tanzania na kama nilivyosema wateja wakubwa ni vijana wenye kipato cha wastani (tabaka la kati).Hili la elimu linawezekana na ni mbinu endelevu.
Mila zetu zinachangia kuhusu matatizo ya ongezeko la tatizo hili la kiafya na hakuna anayejua gharama nchi inayoingia kwa mwaka katika kutibu magonjwa yanayotokana na unene.
Hatari inayotukabili ni jinsi watoto wetu walivyokuwa ‘windo’ jepesi kwa kampuni hizi za vyakula. Kuanzia vyakula vya sukari kama juice, biskuti, ‘chipsi kuku’, siagi,pipi na chumvi nyingi kama Pringles!
Hii ni hatari, katika Ulaya na hasa Uingereza matangazo yote ya vyakula hayawausishi watoto ni marufuku. Niliwahi kukumbana na kisa cha mtoto wa miaka mitatu ‘anayejipendelea’ blue band pekee kwa kulamba. Mukisahau kopo limekwisha kwa utamu wa chumvi!
Nchi nyingi zipo katika vita hii,nguvu zimeelekezwa katika kuwalinda watoto, dhidi ya ‘ulaghai’ wa matangazo ya redio na televisheni na mabango ya barabarani.
Ulaya wameenda mbali zadi hata uwekajiwa bidhaa katika ‘shelf’ unaratibiwa, haipaswi kuweka vyakula vyenye chumvi na sukari nyingi karibu na uwezo wa watoto kuona! Hii yote ni katika kulinda taifa la kesho ili lifanye maamuzi sahihi ya uchaguzi wa chakula.
Katika Uingereza sheria inakataza kurusha matangazo ya vyakula ambavyo ni ‘junk’ food kati ya saa 12 hadi 4 asubuhi. Vyakula hivi mara nyingi ni vyenye sukari na chumvi nyingi yenye ‘kurembwa’ na mafuta.
Kampuni za vyakula zinatumia matangazo ya redio na televisheni kuhamasisha ulaji wa siagi tena kwa kauli mbiu za watoto. Unilever wanainadi Blue Band kwa tangazo la’ HAKUNA B, Bila, B’ likisindikizwa na sauti za watoto. Huku wakifadhili vipindi kama LEO TENA cha CLOUDS FM kirushwacho kati ya saa 3 hadi sita.
Kimsingi kampuni za kimataifa( Multinational Companies) zinajukumu la kutulinda lakini kampuni hizi zimesaini mikataba ya kudumisha na kujali haki za wateja nyumbani kwao na zinajitahidi ‘kupumbuza’ watu wa magharibi kuwa ni wanajali afya za walaji katika Dunia ya tatu.
Society Marketing inayoshika kasi katika Ulaya haimaanishi kampuni hizi zitatufanyia kwa staha lazima tutambue kuwa hakuna mtafutaji atakayejali jamii kama hakuna sheria za kudhibiti mwenendo wa wa wafanyabiashara hawa
Ukweli wa mambo wanapofika huko ‘hawachezi’ fair. Wanaongeza sukari na chumvi kuliko viwango na matangazo ya hamasa yanatumika kama kawaida. Mfano mzuri ni jinsi kampuni za kimataifa zinavyolishambulia soko laThailand.
Kampuni kubwa za chakula na wauzaji wa chakula kwa pamoja mara zote wamekuwa wakaidi hata kupinga tafiti za kitaalamu. Bado tunakumbuka jinsi walivyokuwa wakipinga kupunguzwa kwa chumvi kwa madai kuwa tafiti zilizofanyika zinaonesha tu ‘uhusiano’ kati ya chumvi na magonjwa ya shinikizo la damu .Na si kwamba ni kisababishi.
Madai yao yalikuwa ya kibiashara zaidi na wanajua kuwa wakipunguza utamu wa chumvi katika Pringle au nyama ni wazi kuwa ulaji utapungua.
Unene unapofikiriwa kuwa ndiyo utajiri wa familia mara nyingi ni hatari na kampuni hizi hazifanyi makosa. Katika Thailand, mtoto mnene ‘Baby Elephant’ ilikuwa ndiyo ‘hulka’ ya familia.
Nazo kampuni kama Nestle, Kellogg’s, Tesco,ASDA,Coca Cola, KFC zilipopiga hodi kwa mgongo wa FDI hazikufanya makosa waliijaza nchi na vyakula hatari kwa afya.Leo hii takwimu ni za kutisha katika nchi ambayo watu wake walikuwa walaji wa vyakula vya baharini na mboga mboga.
Kwa mfano katika Uingereza 5g tano ya sukari ndiyo itakuwa kipimo cha sukari kwa vyakula.Wakienda masoko ya kimataifa wanaweka zaidi ya hapo hadi kufikia 20g ripoti zinaonesha kuwa Thailand ya leo ni wahanga.
Tanzania haijakwepa uchu wa wawindaji hawa wa uchumi wa kimataifa, kuna matangazo na supermarkets zinaanzishwa pia kampuni tanzu zinazosambaza vyakula hivi zikiwa na matawi katika mikoa.Kampuni za juisi, chewing gum, pipi biskuti nakadhalika.
Ukosefu wa sheria za kudhibiti kampuni hizi ndiyo chanzo cha hatari hii. Wanaruhusiwa kufanya matangazo ambayo ni hatari.
Vifungashio vya pipi kwa sasa vina picha za wachezaji bora duniani, wapiganaji wa mieleka mashuhuri na mabondia.
Jojo (Chewing Gum) zimefungwa na picha za Christina Ronaldo, Didier Drogba, Nicholas Anelka, Samuel E’Too na Evander Holyfield.
‘Mbinu’ hizi hawarushusiwi kutumia ulaya.
Ni marufuku kutumia ‘model’ kwa ajili ya kuhamasisha vyakula hatari na hasa ukitambua kuwa kuna watu wanaweza kufanya maamuzi kwa vile tu wameona picha ya Drogba.
Hawa ni watoto, lakini vyakula kama chocolate, na biskuti zinafungwa katika mtindo huu.
Hili ni bomu, tunashindwa kutibu malaria, itakuwaje kisukari cha umri wa utotoni?
Hali itakuwa mbaya zaidi kwa nchi ambayo viwanja vya mazoezi tumeuza tumekubali kuasi mipango miji kwa, hongo ya kula siku mbili tatu.
Watoto hawa hawana muda wa mazoezi shuleni wala nyumbani, na familia hazimudu kuwapeleka ‘gym’
Tunaloliweza ni hili la kudhibiti matangazo ya yanayochochea watoto kula vyakula hatari. Na hasa kwa kutumia picha za watu mashuhuri.
Kipindi cha watoto kinadhaminiwa na kampuni ya kutengeza ‘junk’ food tena mbaya zaidi gramu za sukari ni zaidi ya 20!
Hii ni vita ya nchi moja moja ulimwengu unatutizama, na kwa vile sisi ni watu wakusubiri misaada hata katika jambo dogo la kutumia maarifa tu yakuzaliwa nayo tumezubaa.Adui wa afya za watoto wa Tanzania ni kwashiorkor. Mpaka leo unatushinda, sasa tukizalisha tatizo jingine itakuwaje?
Yatupasa kubadilika, tuuanze mwaka 2010 kwa kuwalinda watoto wetu na matangazo ya vyakula hatari pia.Tubuni sheria zinazobana matumizi ya picha za watu maarufu kwa ajili ya matangazo ya vyakula hatari, pipi, juisi, biskuti na kadhalika.

No comments: