Monday, March 29, 2010

Changamoto ya mitaji toka nchi zinazoendelea

Ripoti ya mwenendo wa uwekezaji (World Investments Report) ya shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Biashara na maendeleo (UNCTAD), ya mwaka 2009 inataja nchi zinazoendelea kuwa zimeweza kuhimili hali mbaya ya Uchumi wa Ulimwengu kwa kuweza kupata asilimi 27 ya mitaji toka nje (Foreign Direct Investments). Ingawa kiwango hiki ni cha chini ukilinganisha na mwaka 2007 lakini ni hali yenye kutia moyo.
Jumla ya dola za kimarekani bilioni 88 zimekezwa katika Afrika, kwa mwaka 2009 pekee, pamoja na mafanikio hayo bado miradi mingi toka nje ilishindwa kuendelezwa kutokana na heka heka ya kuyumba kwa uchumi wa Ulimwengu.
Eneo la Afrika Mashariki lilijizolea shilingi bilioni 4, ikiwa ni eneo lililopata mgao mdogo kwa muda wa mwaka wa pili mfululizo. Pamoja na hali hiyo mitaji toka nchi zinazoendelea imeendelea kumiminika Afrika, wawekezaji wakubwa kutoka nchi masikini ni Uchina, India na Afrika Kusini. Huku Uchina ikijikita katika usakaji wa rasilimali ya mafuta katika Angola, Sudan na Nigeria, bila kusahau miradi mikubwa ya ujenzi katika Kongo-Kinshasa na Afrika Magharibi, pia Afrika Kusini ikifanya vyema katika uwekezaji wa madini katika Tanzania kwa kufanikiwa kununua hisa za Ghana na ikisambaa katika ufunguzi wa maduka ya rejareja (supermarkets) toka Nchi za SADC had ECOWAS, bila kusahau ufunguzi wa mabenki.
Wawekezaji wakubwa wa mitaji katika Tanzania ni Afrika Kusini, Kenya, Uchina, India, Pakistani, Mauritius na Malaysia. Lakini tangu ujio wa wawekezaji hawa mara zote imekuwa kilio katika hali ya uchumi wa Tanzania. Toka wafanyakazi, wafanyabisahara na viongozi wetu wetu wa kitaifa.
Wakati fulani Raisi Kikwete akiwa ziarani nchini Japani aliwahi kunukuliwa na vyombo vya habari akiwaasa wajapani wasiwape kazi za kusimamia mitaji yao wahindi na wapakistani kwa vile ‘wanawapunja’ watanzania.Pia Waziri Mkuu M. Pinda aliwahi kunukuliwa na vyombo vya habari akiwaambia wahandisi wa kichina mkoani Arusha kuwa wanakosa vijana wahandisi wa kufanya nao kazi katika kampuni zao kwa vile wanawalipa mishahara midogo. Hivi ni vilio vya kila siku
Katika Tanzania, nchi zinazoendelea zimewekeza kwa wastani wa asilimia 47, hivyo wawekezaji hawa kutoka nchi hizi ni nguzo muhimu katika mageuzi ya uchumi wa Tanzania. Tukitumia takwimu za idadi ya mitaji, Kenya mara zote uhibuka kama muwekezaji namba moja lakini kwa thamani ya pesa Afrika Kusini ndiyo muwekezaji mkubwa katika Uchumi wa Tanzania.
Mitaji toka nchi zinazoendelea imejikita katika maeneo mawili masoko na kiu ya utafutaji wa malighafi kwa viwanda vyao vya nyumbani. Hii ni changamoto kubwa kwa siku zijazo za majaaliwa ya Tanzania na ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii yake.
Lengo kuu la kuhimiza mitaji toka nje na kufanya mabadiliko makubwa ya kiuchumi tangu miaka ya 1980 ilikuwa ni kupata ahueni ya kiuchumi na kimaendeleo kwa jamii yetu. Swali la msingi ni je hawa wawekezaji wa kizio cha kusini wana mwisho mwema katika lile lengo letu?
Makala haya itajaribu kukusanya vipande vipande kuelekea ukweli. Kwani tunaamini uwekezaji ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa Tanzania ila yatupasa kuangalia na kujali masilahi yetu kama nchi na basi lengo kuu ni kujaribu kukumbushana hasa juu ya mwenendo wa uwekezaji wa siku za karibuni uliojitokeza na makampuni toka Kusini.
Na wala isieleweke kuwa tunataka kutia chumvi au tunapinga harakati za mageuzi ya uchumi la hasha, lengo ni lile lile kujenga Tanzania yenye neema na heshima kwa wananchi wake.
Tunapotupia jicho wawekezaji toka kusini haiimaanishi kuwa wawekezaji wa kasikazini ndiyo wazuri la hasha ila yatupasa kujadili hali ya mambo katika misingi ya makundi ili walau tujue wapi tunakwenda kwa kuzingatia kile tunakichokiona kulingana na matarajio yetu.
Kwa sasa Tanzania ipo katika hali ngumu ya kujaribu kufuta hali ya sura yake katika biashara ya kimataifa, baada ya RITES wakezaji katika sekta ya usafiri mkataba wake kusitishwa. RITES ni kampuni ya India, ni wawekezaji toka nchi zinazoendelea.
Huu si mktaba wa kwanza Tanzania kuufuta, kuna mkataba wa awali ambao nchi iliuingia na wawekezaji toka Uingereza Biwater na wakashindwa kufanya kazi nao ulifutwa , huku Biwater ikienda mahakamani na kushindwa na ikitakiwa kulipa paundi milioni 8 kwa serikali ya Tanzania.
Lakini lililowazi ni kwamba hatujifunzi somo, na kwa sasa kuna hali ya kuendelea kwa yale yale yaliyopita kwa Biwater ndiyo yametokea kwa RITES. Labda tuweke wazi kuwa hili la RITES lilionekana toka mapema kwani mwekezaji mwingine GAPCO aliyepewa hisa bila hata kuwa na mtaji alidumaza jitihada za kufufufua shirika hili, kwani uwepo wa GAPCO ulifanya IFC kusita kutoa pesa za mkopo dola milioni 44, kwa hoja kuwa huyo aliyepewa hisa, GAPCO, ni mdeni wa IFC hivyo kuna ulakini kama hatua hii itaenda sawa kama ikipewa tena dhamana ya deni la dola milioni 44!
Kutokana na GAPCO kukumbana na kigingi cha IFC, serikali ikaingia kuwa mbia na RITES bila maandalizi.Ni wazi kuwa hatua hii ilichangia kwa kiasi kikubwa kuyumba na kupungua imani miongoni mwa wafanyakazi kwa RITES. Katika mchakato huu kuna mwekezaji mwingine toka India aliyekuwa na wastani wa hisa mbili alijitoa! Bila shaka maji yalizidi unga waswahili wanasema naye aliweza kubashiri vyema.
Hili la RITES si la kwanza ila inaonekana hatujajifunza somo hasa inapokuja wawekezaji toka Kusini, kwani mwaka 2007, Brookside kampuni ya Kenya ilinunua kwa mbwembwe kiwanda cha kusindika maziwa cha Arusha na kuahidi kufanya uwekezaji wa dola milioni 100, katika sekta ya maziwa. Lakini kilichokuja kushuhudiwa ni Tanzania kugeuzwa kuwa shamba la malighafi na uzalishaji unafanyika Kenya.
Mwaka jana ndipo waziri mwenye dhamana ya Afrika Mashariki Dk.Deodorus Kamala alipoifukuzilia mbali Brookside. Ingawa sura ya Tanzania imechafuka lakini liliwazo kuwa hawa wawekezaji toka nchi zinazoendelea mara zote wamekuwa ni wajanja wajanja na wanafanikiwa kwa gia ya kuonekana kama watu wanaoweza kustahimili hali ngumu za miundo mbinu ya Afrika lakini mwisho wake ndiyo haya.
Wawekezaji toka kusini kila wanapowekeza kila wakati imekuwa ni vitendo vya malalamiko na manung’uniko nchini. Hivi karibuni kuna wawekezaji katika sekta ndogo ya ngozi wenye asili ya India na Pakistani kuwa hawapo tayari kuongeza thamani ya ngozi katika viwanda vya ndani na badala yake wanasafirisha ngozi ghafi kwao!
Hilo likiwa halitoshi Ripoti moja ya FAO inataja kuwa kuongezeka kwa vyakula toka nje ya Tanzania ni kwa sababau wawekezaji katika sekta ya utalii na hasa hoteli huagiza vyakula toka nje huku vikiweza kupatikana Tanzania.
Hivi karibuni Waziri Ngeleja amenukuriwa na vyombo vya habari kuwa wawekezaji katika migodi waache kununua nyama nje ya Tanzania badala yake wanunue nyama Tanzania ili tuongeze tija katika viwanda vyetu vya ndani na kuongeza ajira. Katika sekta ya nyama kuna SAAFA ya Rukwa na Tanzania Meat Pride Morogoro. Hatua ya muheshimiwa Ngeleja, ni rai njema sijui katika vitendo itakuwaje, ni suala la kusubiri na kuona, ila ni mwanzo mwema.
Kila kitu sasa tunaagiza toka nje huku ndani kuna wajasiriamali wadogo waliowekeza katika kilimo na usindikaji wakitaka kupata hizo kazi tunapewa hoja chakavu kuwa minofu yao haina viwango mara minofu ya kuku ina harufu ya dagaa!
Bila mabadiliko ya kisera katika kuhakikisha wawekezaji wanatumia bidhaa za ndani ni wazi kuwa tutabakia kuwa watazamaji. Kuna nchi zimeweka wazi kuwa mwekezaji anapaswa kufanya nini anapoingia nchini na asilimia ngapi ya malighafi anayotumia inapaswa kutoka soko la ndani.
Bidhaa wawekezaji wa ndani wanaikataa lakini inapenya na kufanya vyema katika masoko ya Ulaya, tena ikisifiwa kuwa na viwango bora. Kuna mifano mingi ya bidhaa za kilimo zinazofanya vyema Ulaya lakini nyumbani hazina nafasi!
Tusibwete katika ‘kulainisha’ mambo kwa kigezo cha kuvutia mitaji. Hili la kuwa na wachuuzi wa Kichina Kariakoo, Kenya majirani zetu tangu miaka 1960 wameweka wazi kuwa mwekezaji wa nje hapaswi kuingia katika sekta ya’ juakali’. Lakini Tanzania hapana.
Niliwahi kuhudhruia ‘carrier workshop’ ya moja ya benki katika Tanzania, wakati wa majadiliano kuhusu mishahara Mkurugenzi wa Benki alieleza wazi kuwa hataweza kulipa zaidi ya mshahara wa serikali. Kigezo alichotumia ni kuwa serikali inawalipa wenzenu TGSD, tena wenye shahada kama nyinyi!
Kumbe katika malipo ni sisi ndiyo tumejimaliza na hakuna mchawi ila ni serikali kuwa na viwango vidogo vya mishahara na wageni wakija wanaangalia ‘skeli’ za serikali nao wanatumia kigezo hicho hicho katika hali kama hii ni vigumu kuona mitaji kutoka nje ikiwaneemesha watanzania.

No comments: