Monday, March 15, 2010

‘Food miles’ changamoto kwa biashara ya chakula toka Afrika

Mabadiliko ya tabia nchi na hali ya hewa Duniani yanaendelea kufanya wanasayansi kufikiria njia za kupambana na madhara yake kwa kila namna. Inakadiriwa watu 800,000 wamepoteza maisha na jumla ya dola za kimarekani trilioni 1 kama hasara jamii ya ulimwengu huu imeipata kutokana na mabadiliko hayo ya hali ya hewa ya ulimwengu.
Katika nchi za Ulaya na Marekani nadharia inayochipua kwa kasi na kuungwa mkono na wakulima wengi ni ‘food miles’ huku wakipiga chapuo ‘local is good’. Nadharia ya food miles iliyochomoza kwanza Uingereza sasa inaonekana kupendwa pia na wakulima na taasisi zinazotoa mikopo katika Marekani.
Food miles ni nini?(nitalitumia neno hili kama lilivyo kwani sina neno zuri la Kiswahili),hii ni nadharia rahisi inayozingatia umbali kwa kupima madhara ya uharibifu wa mazingira yatokanayo na uzalishaji wa chakula toka shambani hadi mezani kwa mlaji. Hivyo walaji wanashauriwa kususia vyakula vilivyo safiri umbali mrefu kwa lengo la kulinda mazingira, yanayochafuliwa na hewa ya ukaa(KABONIDAYOKSAIDI), na badala yake watumie vyakula vilivyozalishwa nchini kwao ambavyo mfumo wake wa uzalishaji na usambazaji ni wenye umbali mfupi!
Nadharia hii iliibuliwa miaka ya 1990 na Profesa Tim Lang ambaye kwa sasa ni mhadhiri katika City University London. Tangu wakati huo kama tulivyo sema hapo awali wakulima wa Kiingereza na Marekani kupitia vyama vyao wamekuwa wakihimiza utumiaji wa bidhaa zandani (Local is good) kwa hoja ya kulinda na kupunguza uharibifu wa mazingira.
Uingereza moja kati ya masoko mazuri ya bidhaa za kilimo katika Jumuiya ya Ulaya, inakadiriwa kutumia paundi milioni 105 kwa ajili ya ununuzi wa mboga mboga na milioni 89 kwa matunda kutoka Afrika ya Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Ni wazi kuwa kushika kasi kwa nadharia hii katika biashara ya chakula kunahatarisha hali ya jamii ya wakulima wadogo masikini wa kizio cha kusini na hasa Afrika. Ingawa mpaka sasa wanasayansi wanasema kuwa mchango wa Afrika katika kuchangia uharibu wa hali ya hewa ni mdogo. Afrika inakisiwa kuchangia asilimia 0.5 ya gesi ya ukaa na bidhaa zinatoka eneo husika hulimwa kwa njia za kijadi (jembe la mkono, plau, mbole ya samadi, bila hata kutumia dawa za kuulia wadudu)
Kimsingi huu ni mwendelezo wa kuonesha wazi kuwa soko la Ulaya lilivyo kigeugeu na wala siyo la kuaminika. Lakini pamoja na hayo yote bado Afrika imekuwa ikiweka nguvu kuzalisha bidhaa kwa ajili ya soko hili. Hili tumelizungumza katika makala nyingi katika siku za nyuma.
Watetezi wa bara la Afrika nao hawakukaa kimya.Mashirika ya kimataifa kama Oxfarm GB na kampuni za wauzaji wakubwa wa bidhaa za kilimo toka Afrika kama Sainsbury wamejitokeza hadharani kupinga wimbi hili la ‘food miles’ lenye nia ya kuitoa Afrika katika biashara ya Ulimwengu kwa kigingi cha mabadiliko ya tabia nchi. Mkurugenzi Mkuu wa Sainsbury aliita hatua hii kama ‘protectionism’ ya aina yake na kampuni yake haiko tayari kukubali hii nadharia kwa ukweli kwamba kununua Afrika ni njia ambayo inapelekea ukombozi wa kiuchumi na kijamii kwa wakulima wengi wadogo wa bara hili.
Bado wataalamu wa kilimo wa Afrika na wanasayansi wanaendelea kupinga nadharia hii kwa hoja kuwa bara hili halizalishi kiwango kikubwa cha hewa ya ukaa wakati wa shughuli za kilimo na wala njia zinazotumia kusafirisha chakula toka Afrika bado hazichangii kwa kiasi kikubwa kuzalisha hewa ya ukaa. Kilimo cha Afrika bado cha jembe la mkono na kisichotumia mbolea, hivyo mazao yale yauzwayo nje ya bara hili kama kahawa, sukari, kakao, pamba, korosho, tumbaku, maua, mbogamboga chai huchangia kwa kiasi kidogo katika kuharibu ‘ozone layer’
Nchi nyingi za Afrika, kigingi hiki ni pigo kwani bado kilimo ni chanzo kikubwa cha ajira, pato la taifa, kwa mfano kwa Tanzania zaidi ya asilimia 50 ya pato la fedha za kigeni linategemea mauzo ya kilimo, Malawi ni zaidi ya asilimia 80, na Kenya ni zaidi ya asimilia 65.
Hivyo juhudi hizi hasi za kuona Afrika haifikii masoko ya Ulaya kwa kigingi cha ‘food miles’ na kampeni za kupambana na uharibu wa mazingira ni pigo kwa Afrika. Taasisi moja ya Kingereza inayojihusisha na maendeleo ya kilimo maeneo ya vijijini ilibainisha wazi kuwa msukumo mkubwa upo katika kulinda wakulima wa Kiingereza, kwani ni wazi kuwa kila kitu sasa kinaonekana kuwa kinatoka nje ya Uingereza.
Kilimo cha nyumbani (Local is good) kinapingwa pia kwa hoja kuwa hali ya hewa ya nchi hizi wakati wa wa baridi hutumia nishati kwa kiasi kikubwa (green house) na hivyo lile la kupambana na mabadiliko ya hali hewa halina nguvu.
Ni wazi kuwa suala la mazingira halina tajiri wala masikini, kila mmoja ana jukumu la kupambana na uharibifu wa mazingira, ila lililowazi kuwa Afrika safari hii inakabwa na juhudi hizi. Afrika ambayo inakabiriwa na mapigo makubwa ya mabadiliko ya tabia nchi ikiwa na tishio la kugeuka jangwa, ukosefu wa mvua, ongezeko la joto na mufuriko, inapaswa kujitahidi kupambana na haya yote.
Ila wataalamu wa mazingirwa wanabainisha kuwa, mifumo ya maisha ya wakazi wa kizio cha kaskazini ndiyo chanzo kikubwa cha mabadiliko ya hali ya tabia nchi. Katika Ulaya nyama inasadikiwa huchangia kwa kiasi kikubwa, kwani unenepeshaji wa mifugo kwa kutumia nafaka badala ya majani au nyasi. Wataalamu wanashauri kubadilisha milo toka nyama kwenda majani na mboga mboga.
Pia mtindo wa uendeshaji wa magari yenye injini kubwa (sports cars) yanayokula mafuta kwa kiasi kikubwa huchangia kwa kiasi kikubwa . Utupaji wa chakula, ambayo mabaki haya hutumia kuziba makorongo huzalisha kwa kiasi kikubwa hewa ya methane ambayo huchangia kwa kiasi kikubwa kuharibu anga la dunia. Japani hutupa tani milioni 20 kwa mwaka, hivyo rai ipo kwa watu wa kizio hiki kujitahidi kutotupa chakula.
Kigingi hiki kinatufanya kuangalia soko la ndani kwa masilahi ya Afrika. Biashara ya ndani ya bara la Afrika ni asilimia 4 tu, huku nguvu nyingi zikiwekwa katika kufikia soko la Ulaya. Ingawa ni kweli kuwa mahitaji ya fedha za kigeni ni makubwa kwa ajili ya kuagiza mahitaji mengine muhumi kama dawa, bidhaa za viwanda na mitambo. Lakini biashara ya ndani ingeweza kupanuwa uwigo wa wakulima wa bara la Afrika kuliko kukaa na kugombania kufikia katika soko la Ulaya pekee.
Soko la ndani katika nchi nyingi za kiafrika bado kufunguka huku kila nchi ikiwa iko tayari kuweka kigingi kwa nchi ya kiafrika lakini ipo tayari kufungua milango kwa nchi za magharibi. Hili la food miles ni changamoto nyingine kwa Afrika, tuna jukumu ya kuhakikisha linapata suluhu ya kudumu kwani ni nadharia inayosambaa kama moto katika nyasi za savana.Juhudi za kampeni ya kuhamasisha kupenda bidhaa za nyumbani ambayo Tanzania inafanya kupitia CTI ni suala la kuhimizwa kwa nguvu zote, na juhudi hizi zinapaswa kupelekwa katika shule na vyuo. Huu ni mwanzo mwema, kwani sasa food miles inashika kasi katika Ulaya na Marekani, kwa hoja ya mazingira. Basi yatupasa kupenda bidhaa za nyumbani.

No comments: