Monday, March 29, 2010

Ushirika na maajaliwa ya ‘Fair Trade’ katika Tanzania

Tanzania ni nchi ya kwanza Kusini mwa Jangwa la Sahara kuingizwa katika mpango wa ‘FAIR TRADE’(biashara huru), ila makala haya itatumia neno 'fair trade' moja kwa moja. Mpango huu ambao ulianza mwaka 1988 kupitia kahawa, kwa sasa unahusisha pia chai na samani hasa zenye kurembwa kwa shanga.
Kagera Cooperative Union (KCU) ni chama cha kwanza kunufaika na ‘Fair Trade’, kwa kuanza kuuza kahawa yake katika masoko ya Ulaya na Amerika. Kimsingi mpango huu umejikita katika nadharia ya kuwapa nguvu wakulima masikini wadogo wa nchi changa kuweza kufikia masoko ya Ulaya, huku wakinufaika kwa kazi ya jasho lao, kwa kulipwa bei nzuri ambazo ni zaidi ya bei ya soko la dunia.
Baada ya manufaa ya mpango huu kwa sasa nchini Tanzania vyama vya ushirika kama Karagwe District Cooperative Union, Kilimanjaro Native Cooperative Union pia wapo katika kuuza kahawa. Pia wafanyakazi wa mashamba ya chai katika Kibena ana Luponde Iringa na Lushoto, Tanga wapo katika mpango huu. Pia kuna mau yanayouzwa na kampuni ya Kiliflora ya Arusha kwa kutumia nembo ya 'Fairtrade' yakiwa chini ya Max Havelaar nembo inayoratibu masoko ya Uholanzi, Ubelgiji na Ufaransa.
Ili kufanikisha mpango wa fair trade ushirika imara ni muhimu kwa uhakika wa soko na mgawo wa pato la mauzo. Ushirika ndiyo kiunganishi kati ya wanunuzi na wakulima. Na hili la kuundwa kwa ushirika imara ni moja kati ya masharti makubwa ya kuweza kusajiliwa kama mzalishaji wa kahawa chini ya mpango wa 'fair trade'. Kwa wamiliki wa mashamba makubwa ya chai moja ya masharti ni kuundwa kwa vyama vya wafanya kazi huru vikiundwa na wafanyakazi wakipata hali bora kama huduma za kiafya na elimu kwa ajili ya watoto wao kutokana na chumo la 'Fair Trade'.
Mpango wa Fair Trade unashika kasi katika Afrika, Uganda na Malawi zinauza sukari, Kenya na Afrika Kusini zikijikita katika chai.Ingawa Tanzania ni mmoja kati ya wakongwe katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara lakini ushiriki wake unaonekana kupungua. Na hii si kama bei ya kahawa au chai inaonekana kutengemaa sokoni la hasha.
Kwa mujibu wa mtafiti Profesa Fautini Karani Bee katika chapisho Fair Trade- Fair Future anabaisha wazi kwamba mauzo ya chama cha KNCU ya kahawa katika mpango huu, ni milioni 105, 069, 272, kwa mwaka 2008 wakati mwaka 2004 yalikuwa 175, 320, 894. Pato hili ni ile pesa ya ziada ambayo walaji wa Ulaya na Marekani wako tayari kulipa, achiliambali bei ya zao husika kuwa ipo juu ya bei ya soko.Ni wazi kuwa ushiriki wetu unalegalega.
Fair Trade imaleta hali bora kwa wakulima wadogo wa Tanzania , kuna wanafunzi zaidi ya 250 wamepata udhamini wa kupata elimu ya sekondari kupitia mpango uliobuniwa na chama cha KNCU. Pia washirika hawa wameweza kununua hisa katika Kilimanjaro Cooperative Bank.
Upepo wa mafanikio pia unavuma kwa washirika waliochini ya KCU ambao wameweza kununua hisa za kiwanda cha kahawa cha Kagera. Haya na mambo mengine mengi ni mafanikio ya juu wakulima wameweza kujipatia kupitia mfapongo huu.
Changamoto za Fair Trade katika Tanzanai ni nyingi , miongoni mwa hizo ni ukosefu wa vyama vya ushirika imara. Vyama vya ushirika ndiyo nyenzo ya Fair Trade, hivyo kufanya juhudi zote za kuondoa walanguzi sokoni kutegemea vyama hivi.
Wakulima wa Tanzania wamedhalilika na kuoenewa sana na vyama vya Ushirika. Ushirika umekuwa ni mzigo mzito kwa wakulima wa Tanzania. Ingawa ni kweli kuwa hakuna kesho bila kuwa na ushirika na hasa kwa wakulima wadogo na masikini wa Tanzania. Inashangaza ni kwanini serikali imekuwa na kauli nyingi bila vitendo!
Mtafiti Pirotte (2006) katika tafiti ‘Fair-Trade coffee in Nicaragua and Tanzania: a comparison’ iliyochapwa katika jarida la kisomi la Development in Practice , chapisho la 16 namba 5 anabainisha wazi kuwa wakulima sasa katika Tanzania, wamefikia hatua ya kuona FAIR TRADE, ni sawa na wafanyabiashara wengine (walanguzi), lakini hili limechangiwa zaidi na mwenendo wa ushirika. Ni wazi kuwa aliyeumwa na nyoka akiona unyasi atastuka. Maoni hayo yanaonesha wakulima walivyo kata tamaa na Ushirika hivyo lolote lilillochini yake ni wazi kuwa ni ulaghai!
Ni wazi kuwa mwenendo wa ushirika hauridhishi na wenye kuhitaji kurekebishwa ili kufikia lengo la kuwanufaisha wakulima wa Tanzania.
Hivi karibuni Waziri Mkuu M.K. P Pinda na Waziri wa Kilimo J. Wasira kwa nyakati tofauti wakiwa ziarani Japan na Vietnam wamesikika wakiweka wazi juu ya umuhimu wa ushirika imara kwa masilahi ya wakulima wa Tanzania.
Hili la kilio cha kukosa ushirika imara si jambo jipya. Ni kilio cha muda mrefu, na wala kauli za viongozi wetu katika kuhimiza ushirika imara si mpya pia.
Kauli za viongozi ni sahihi lakini zinahitaji vitendo katika kuwajengea wakulima imani dhidi ya ushirika na hili la Fair Trade linaonesha wazi jinsi tunavyochezea shilingi chooni.
Hali ya mambo inaonesha wazi kuwa kukosekana kwa ushirika imara Tanzania iko hatarini kupoteza nafasi yake katika kufikia masoko ya Marekani na Ulaya kupitia mpango huu. Mtafiti Paul Attontile anabainisha wazi kuwa mapungufu ya watendaji na viongozi wa ushirika yamewafanya hata wanunuzi wa kahawa chini ya mpango huu kufikiria kama kuna namna nyingine ya kuwafikia wakulima wadogo wa Tanzania.
Wakati Tanzania inalega lega kutumia nafasi hii, lakini nchi nyingine wao wako wanapambana kuongeza ushiriki wao kwa kusajili bidhaa nyingine mpya zilizoingizwa chini ya mfumo huu, kama vile asali, ndizi, nguo za pamba na bidhaa za mikono.
Mauzo ya sasa duniani kote ni zadi paundi 1.6 bilioni ukijumalisha masoko ya Ulaya na Amerika. Ingawa biashara ya Fair Trade ni wastani wa asilimia 1 ya biashara ya ulimwengu, lakini lenye kutia moyo ni kukua kwa kasi kwa biashara ya mauzo ya huku Itialia ikukua kwa asilimia 404 na Uingereza asilimia 72.
Walaji pia wa masoko ya Ulaya wako tayari kununua bidhaa zenye kujari masilahi ya wakulima masikini wa Kizio cha Kusini kwa zaidi ya asilimia 70. Mwenendo huu wa walaji na soko unaonesha kufanikiwa kwa mpango huu katika kulifikia soko na ‘kukuna’ nyoyo za walaji za ‘Trade not Aid’
Tuimarishe ushirika, kwani majuto ni mjukuu na Fair Trade imeonesha wazi kuwa inamwisho mwema kwa wakulima wa Tanzania, basi tusichezee shilingi chooni, shime viongozi wetu maneno matupu hayavunji mfupa.

No comments: