Sunday, January 10, 2010

Bila walaji 'makini' ushiriki wetu u-mashakani

Gwiji wa Uchumi Profesa Michael Porter wa Chuo Kikuu cha Harvard katika nadharia yake maarufu kama 'Porter's Diamond Model' au 'faida ya ushindani'(Competitive Advantage) anabainisha wazi kuwa nchi ili ifanye vyema katika biashara ya kimataifa inahitaji kuwa na 'walaji makini'(Sophisticated Customers). Walaji wanaojua kuwa hii bidhaa haina ubora, na wapi waende ili wapate haki zao mara wanapokosa huduma bora toka kwa kampuni husika kwa 'uwongo' wa makusudi wa kibiashara.
Porter’s Diamond model inataja viashiria vikuu vinne vinavyo weza kufanya nchi iweze kushamiri katika biashara ya kimataifa, rasilimali (endowment factor),mahitaji ( demand condition), uhusiano wa kiviwanda (relating and supportive industries) na mbinu za kibiashara (firms strategy).
Makala haya itajadili umuhimu wa walaji makini kwa ustawi wa sekta ya kibiashara katika Tanzania na hasa viwanda. Tanzania inahaha kupanua wigo wake wa biashara ya nje, lakini wakati wote imekuwa haifanyi vyema.Kumekuwa na kauli mbiu za kila aina na taasisi kama CTI imekuja pia na kauli mbiu ya ‘kuwa mzalendo tumia bidhaa za nyumbani’
Kimsingi hakuna nchi iliyokuwa na kuimarika katika uchumi wake bila uchumi wa nchi husika kuimarika kwanza katika soko la ndani. Soko la ndani ni muhimu na mara zote limekuwa halina hadhari kubwa kama vile soko la kimataifa.
Tafiti fulani inabainisha kuwa kampuni nyingi zilizokwenda katika soko la kimataifa asilimia 50 zilianguka, kwa sababu mbalimbali. Pamoja na ukweli huo soko la kimataifa bado limebakia kuwa ni suluhu moja wapo ya kuimarika kwa uchumi si kwa nchi changa kama Tanzania tu bali hata nchi tajiri nazo zinahaha kuweza kujiimarisha katika masoko ya kimataifa mapya (Emerging markets) ya Asia na Afrika.
Sekta ya viwanda kwa sasa Tanzania ipo nyuma pamoja na mambo mengi inayoielemea sekta hii likiwemo uchakavu wa mitambo, miundo mbinu, ukosefu wa nishati(umeme wa mgao) lakini pia hili la kukosa walaji makini linasababisha kilio kwa viwanda vyetu.
Kwa mujibu wa Profesa Porter, soko la ndani linanafasi kubwa kwa kuchochea uhitaji wa bidhaa zenye ubora wa hali ya juu na hivyo kuipa changamoto kampuni katika kuinua na kuboresha bidhaa zake.
Ripoti ya Benki ya Tanazania(BoT) ya mwaka 2006/2007 inataja kuwa sekta ya viwanda imekuwa huku ikichangia pato la taifa kwa asilimia 9.2, ikiwa kuna mauzo ya nje kwa bidhaa za viwandani zenye thamani ya dola za kimarekani 226.8, huu ni mchupo wa dola milioni 34.6.
Mauzo yameimarika katika masoko ya Rwanda, Burundi na Kongo-Kinshasa kwa bidhaa za nguo kama vitenge na kangha, glasi, plasiti kukiwa na mafaniko toka kwa kiwanda cha Simba Plastiki inayouza katika nchi za SADC na pia viwanda vya chuma vinavyouza nondo.Uuzaji wa pombe kali kama konyagi na bia.
Ripoti hii haitaji kuhusu viwanda vya bidhaa za walaji kama sabuni na dawa za meno, lakini kuna taarifa za sabuni ya Foma Gold kufanya vizuri katika masoko ya Malawi na Zambia.
Pamoja na mafanikio haya tuliyojaribu kuyaorodhesha hapo juu, bado Tanzania inakaribiwa na mchango mdogo kutoka katika sekta ya viwanda vyake katika pato la taifa.
Mara zote kilio kimekekuwa kutoka miongoni mwa walaji na wazalishaji kuwa bidhaa za watanzania hazinunuliki sokoni.
Unaweza kujiuliza pamoja na kilio cha ubora mdogo wa bidhaa toka Uchina? Mbona bado tunagombania bidhaa hizo?Hii ni wazi kuwa walaji wa soko la Tanzania, siyo makini.
Ni walaji wanaoweza kununua kiatu cha plastiki kwa bei ya elfu 15000 toka Uchina na kuacha kiatu cha ngozi cha pale Moshi-Kilimanjaro.
Ni wazi kuwa mzalishaji wa kiatu naye atapunguza umakini hali ambayo itafanya kudorora kwa ubora wa bidhaa zake ili aweze kupambana na bidhaa feki za Uchina. Lakini kwa kufanya hivi ni wazi kuwa mbio hizi zinapunguza uwezo wetu katika kuyafikia masoko ya nje.
Ni walaji ambao hatuangalii ubora, ila tunajali uwingi na faida ya mlinganisho wa kifedha ya muda mfupi.
Mlaji makini anafahamu ubora wa bidhaa anayotaka kutumia kwa thamani ya fedha zake.Uhitaji wa bidhaa zenye ubora wa juu katika soko la ndani unavifanya viwanda husika kufikiri namna ya kuongeza jitihada katika tafiti zao(research and development)
Walaji wa Tanzania tunapokea kila kitu hatuko makini, hili linafanya viwanda vyetu vya ndani kubweteka na kusahau kuwa kuna siku za ushindani na hivyo ujio wa bidhaa toka nje zikipiga hodi.
Juhudi za kamisheni ya usawa wa biashara (FCC) za kuponda bidhaa mbovu zinazoingizwa nchini ni zenye kuungwa mkono kwani hizi bidhaa feki zinalemaza si tu walaji na wazalishaji pia.
Kabla ya Tanzania kuingia katika mfumo wa soko huria nadharia iliyokuwa imejengeka ni kuwa kwa vile ni serikali ndiyo mmiliki mkuu wa viwanda hivi hakuna namna ya kudhibiti, wala mteja hakuwa na nguvu ya kupinga bidhaa mbovu ikiwa imezalisha katika kiwanda cha umma.

Lakini imani yetu dhidi ya soko huria kuweza kutuletea bidhaa zenye ubora, imedimimizwa na ujio wa bidhaa feki.
Ni wazi kuwa sasa hivi tatizo ni walaji wasiolindwa wala kupata elimu juu ya umuhimu wa kiuchumi na kiusalama na afya wa kutumia bidhaa zenye ubora.
Ni ngumu kupata wateja walio makini kwa kutegemea nguvu za kiuchumi(soko) tu, yatupasa kuunda chama cha walaji. Chama cha walaji kitadai haki za walaji toka kwa watoa huduma hadi wazalishaji wa bidhaa.
Kwa kudai bidhaa zenye ubora ni wazi pia wazalishaji wa ndani wataamka na kuzalisha bidhaa zenye ubora kwa soko la nje pia.

No comments: