Monday, January 4, 2010

Tanzania na hatari ya majengo ya kifahari

Yapata miongo minne tangu Profesa Rene Durmont, kuandika kitabu chake 'AFRIKA INAKWENDA KOMBO' au kwa kiingereza 'FALSE START IN AFRIKA'.
Kitabu kilihusu Afrika ya 'WEUSI' yaani Kusini mwa Jangwa la Sahara na hasa, Afrika Magharibi.
Na kwa uchache kwa maombi ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliandika kuhusu Tanganyika iliyokuwa katika siku za mwanzo wa UHURU wake.
Mambo mengi yaliyoandikwa na mchumi huyu toka Ufaransa, mpaka leo yapo na yanaisumbua Afrika. Kwa hakika ni muendelezo wa matukio ambayo ukiyasikia unajiuliza, zamani tulikuwa tunadai matatizo yetu yalikuwa yanatokana na kutawaliwa(UKOLONI). Lakini mbona yale yale tu hata baada ya UHURU?
Jambo moja linalonifanya nikumbuke kitabu hiki na Tanzania ya leo ni, juu ya 'pupa' ya kuhitaji majengo ya 'kifahari' yanayomilikiwa na serikali.
Hili aliliona mapema na akalindika na kuionya Afrika , Tanzania ikiwemo, kuwa yapasa kuchagua njia moja ya maendeleo. Ni 'ufahari' wa majengo ambayo haujawahi kumpatia binadamu shibe isipokuwa fedheha, au kujibana huku mukitekeleza mambo muhumimu kwa taifa.
Leo hii Tanzania, inasononeka na ujenzi wa nyumba mbili za BoT zilizogharimu bilioni 2.5Nyumba hizi ni za gavana na naibu wake.
Hii ni baada ya kutujengea minara pacha iliyotugharimu pesa nyingi na kufanya kesi kuwepo mahakamani hadi leo.
Wataalamu wa maendeleo wa Ulaya na wanahistoria mara zote husema kuwa matatizo ya Afrika hayakuletwa na wakoloni tu, bali hata uongozi katika nchi zenyewe. Ilichukua muda kukubali ukweli huu kwa upande wa Waafrika.
Lakini kwa hali hii, ni wazi kuwa sasa vijana na damu mpya ya Tanzania inaona na kushuhudia kuwa taabu zetu ni 'mazao' ya viongozi weusi.
Kuna hoja za utetezi kuwa huu ujenzi ulishapitishwa na bodi miaka ya nyuma, hivyo Gavana wa sasa hana kosa. Sawa lakini, hiki kipindi alichojenga nyumba ni kipindi 'hatari'Uchumi duniani unayumba na tunasikia jinsi pato la taifa lilivyoathirika yeye alishindwa nini kuzuia kwa dhana hiyo kuu ya kiuchumi?Tena ni mchumi?
Niliwahi kuandika siku za nyuma katika gazeti la Majira Jumapili siku za mwanzo za ujio wa Profesa Beno Ndullu, kuwa yakupasa kuzingatia kuwa hutatoka kwa aibu BOT.
Leo, yanaendelea kutokea ni ushahidi kuwa labda utabiri utatimia.
Taasisi hii nyeti ya fedha katika nchi hii imekuwa ni mfululizo wa fedheha kila baada ya fedhea.
Katika magazeti ya Tanzania kila siku tunaoana picha za wanafunzi wakikosa madawati, wakikosa vyoo, wanafunzi wakisoma chini ya miti na majengo mabovu ya madarasa. Sasa hili la ujenzi wa nyumba za watu wawili kugharimu bilioni 2.5 katika nchi masikini kama Tanzania, chanzo chake nini?
Hatumaaninshi kuwa fedha hizi zingemaliza 'mashaka' yetu kwa siku moja yote, la hasha. Isipokuwa tunaona kuwa kama nchi tumekosa muelekeo, na kufahamu nini tunahitaji katika kujenga jamii yenye umoja na upendo.
Tanzania inahitaji nyumba ya bilini moja na ushei kwa familia moja?Ukiamka unaenda kazini unapita mitaani unakutana na watu wako wakiwa na mashaka sura zimekunjamana unajisikiaje?
Mipango katika nchi imekwama kwa hoja ya 'fungu' halitoshi! Tena mipango endelevu. Lakini inapokuja fungu la nyumba ya familia moja kugharimu bilioni fungu linatosha.
Serikali ya Tanzania inahitaji kubadilika, katika kupanga na kutekeleza miradi yenye tija kwa wananchi.
Mwalimu Nyerere alisema kupanga ni kuchagua, nasi lazima tuchague maendeleo chanya na si hasi.
Lazima tutumie kidogo tulicho nacho kwa maendeleo ya nchi na watu wake si vitu.Kimsingi maendelao ya vitu iachiwe sekta binafsi ndiyo ihangaike kujenga majumba ya kifahari, serikali kujenga nyumba ya bilioni moja na ushei hakuvumiliki.

No comments: