Sunday, January 10, 2010

Ni China au ni Afrika ambayo haiwezi kusema 'hapana'?

Katika siku za karibuni ongezeko la bidhaa 'feki' limekuwa ni tatizo kwa nchi nyingi zinazoendelea na Tanzania ikiwemo. Wakati wote huu Uchina imekuwa ikibeba lawama kuwa ndiyo mhusika na ni muendelezaji wa uuzaji wa bidhaa feki, kwa Afrika.
Niliwahi kuhudhruia sherehe moja ya harusi, nikashuhudia mama mmoja akipatwa na kadhia ya kuvunjika kwa kisigino cha kiatu chake cha ‘mchuchumio’ (High heels). Nilipomdadisi aliniambia kuwa ndiyo kwanza anakivaa(ulikuwa palo wa sare ya sherehe). Lakini alijifariji kuwa, amenunua 15000 tu, kariakoo.
Hasara ni hasara, je wale wanaounguliwa nyumba kwa kutumia nyaya au vifaa vyenye viwango vidogo!Ingawa ni ngumu kupata takwimu sahihi, lakini lililowazi ni kwamba miongoni mwetu tupo tunaopata hasara kwa kutumia bidhaa zenye viwango duni kutoka Uchina.
Tanzania bidhaa zenye ubora mdogo zinatusumbua. Makala haya itajaribu kutupia jicho hali ya kibiashara kati ya Uchina na Afrika.Lakini iweje katika maduka ya nchi za magharibi bidhaa za kichina zimejaa, lakini hawalalamiki kuwa kuna 'ufeki' kwa kiwango kama cha Tanzania?
Biashara kati ya Afrika na Uchina imeimarika kuanzia miaka ya 1990, huku Uchina ikiwa inaongoza kwa kufanya biashara na Afrika kwa miongoni mwa nchi za Asia, ikiwa na asilimia 39 ya biashara yake na Afrika.
Kutoshiri katika siasa za ndani za nchi za Afrika kunaifanya Uchina iwe kimbilio la bara hili.Hii ni sera ya mambo ya nje ya Uchina. Hivyo dikteta ana nafasi sawa na mlinda haki za binadamu mbele ya Uchina, ili mradi tu wao wanapata wanachohitaji na masilahi yao yanalindwa.
Biashara kati ya Afrika na Uchina imejikita zaidi katika , ujenzi wa miundo na usakaji wa malighafi hiki ikinunua mafuta kutoka Angola na Nigeria na Sudan. Ujio wa Uchina katika Afrika unahusishwa zaidi na kiu yake ya kusaka mafuta na maliasili zingine, huku ikiwa mtumiaji wa pili wa nishati ya mafuta baada ya Marekani ni wazi kuwa ni mshiriki mkubwa wa Afrika inayokidariwa kuwa na hifahdi ya asilimi 9 ya hifadhi ya mafuta ya Ulimweungu, lakini lenye kuvutia zaidi ni kuwa bara hili bado linaendelea kuvumbua vyanzo vingi vya mafuta katika maeneo mengi ya bara hili.
Jitihada za ushiriki wa Uchina unaimarishwa zaidi na jitihada zake za kufuta madeni ya bilioni 10 za kimarekani kwa nchi za Afrika. Ni wazi kuwa China ni mshiriki mzuri na mwenye kuangaliwa vyema katika kila analolifanya kwa maendeleo ya bara hili.
Kwa mujibu wa vyombo mbalimbali vya habari vya Uchina, Tanzania ni nchi inayoongoza katika Afrika kwa kupata misaada kutoka Uchina. Ni China ndiyo inayotoa mabilioni ya misaada katika kupiga’ jeki’ bajeti yetu na vyombo vya habari vimeripoti ‘mvua’ ya mabilioni ya mikopo kwa Tanzania katika siku za karibuni.
Misaada ipo kaitka kila kona, elimu, afya, jeshi, miundo mbinu nakadhalika. Ushiriki wa Uchina katika maendeleo ya Tanzania ni wa muda mrefu tangu (enzi zaMwalimu) awamu ya kwanza.
Urari wa kibiashara kati ya nchi hizi mbili upo chanya kwa China, huku ikiuza bidhaa zenye thamani ya dola milioni 128 na Tanzania ikiuza bidhaa zenye thamani ya dola milioni 6.62 kwa ripoti za mwaka 2002.
Kwa sasa biashara miongoni mwa nchi hizi mbili imeingiwa na mdudu ‘bidhaa feki’ huku Uchina ikipewa lawama, kwa kila bidhaa inayokamatwa na kila lalamiko katika Tanzania.
Wadadisi wa biashara za Uchina, wanabainisha kuwa ni ngumu kwa Uchina kudhibiti uzalishaji wa bidhaa hizi kwani baadhi ya majemedari wa jeshi wanamiliki au wanahisa katika baadhi ya viwanda.
Lakini, Uchina si muuzaji wa Afrika tu, akiwa na urari wa biashara wa zaidi ya dola 102 bilioni , ni muuzaji mkubwa katika masoko ya Ulaya na Marekani pia.Ni wazi kuwa kieneo si ni sehemu ndogo sana ya chumo lake biashara ya nje.
Tunachojiuliza ni kwa vipi bidhaa za kichina ziwepo kwa wingi na kutumiwa katika nchi kama Uingereza. Ufeki huku haupo kwa kiwango cha Tanzania?
Kamisheni ya Ushindani (FCC) inataja kuwa kiwi za milioni 20 na ‘tubelight’ za aina ya Phillips na Britimax zenye thamani ya dola 18000 zimeteketezwa mwaka 2007, kwa mujibu wa gazeti la Daily News la 1 May 2009.
Pia inakadiriwa kwa mwezi machi pekee 2008, bidhaa zenye thamani dola za kimarekani 224,000, ziliteketezwa na FCC. Ni wazi kuwa FCC kwa uchanga wake inafanya kazi kadiri inavyoweza ili kudhibiti bidhaa ‘feki’.
Vita hii inaonekana kwa sasa inasumbuliwa na ‘balkanization’ kila wizara na idara ya serikali ikipigana kutoka kivyake vyake. Kimsingi vita ya bidhaa feki ni ya jamii nzima, na bila chama cha walaji imara kinachoundwa na walaji wenyewe wafanya biashara wetu watandelea kujaza nchi yetu na bidhaa feki.
Vyombo vyenye mamalaka vimekuwa vingi hadi tuchanganyikiwa tuna TFDA, TBS, FCC.Walaji hatujui tukipata bidhaa ‘feki’ tuanzie wapi? Je tunaitambuaje bidhaa feki?Kuna muongozo wa viwango vya bidhaa, kuwa ubora wa bati unapaswa kuwa ni mchangayiko wa malighafi hizi kwa viwango anuai?Mlaji anayefahamu haya yote?Ni ngumu kwa baadhi ya mbinu kwa mlaji kuweza kutambua.
Ni wazi kuwa vita hii inahitaji kuongezewa nguvu na sheria inayowapa walaji nafasi ya kuwa na chama imara chenye kuwalinda tena chenye nguvu ya kulinda masilahi ya walaji.Katika nchi nyingi vyama hivi vipo na vimekuwa mwiba na vimefanikiwa kulinda nchi zao kuwa majalala ya bidhaa ‘bomu’ si toka nje tu hata wazalishaji wa ndani.
Vyama vya walaji(consumer Associations) vimekuwa vikiheshimiwa kuliko hata taasisi za serikali, kwa vile mara nyingi zimekuwa zikitoa taarifa bila kulinda masilahi ya kisiasa. Mfano mzuri ni imani ya waingereza juu ya FSA(Food Standard Agency) ni ndogo kwa vile ‘walibinya’ ukweli kuhusu homa ya kichaa cha ng’ombe (Bovine spongiform encephalopathy) kwa nia ya kulinda uchumi kwa gharama za walaji!
Ukiangalia mfano huu ni mingine sehemu zingine Duniani, utapata picha kwamba chama cha walaji kinahitajika zaidi kwa sasa Tanzania ili kulinda wateja katika siku za mfumo huu wa soko huria.Kwa sasa kuna chama cha kutetea wasafiria, hii ni hatua nzuri. Lakini yatupasa kukiimarisha chama hiki ili kiendelee kulinda manufaa ya walaji katika sekta ya usafairi.
Hii ni hatua moja tu kama nilivyosema, Tanzania ni kubwa na ushawishi wa wafanya biashara wetu katika kuleta na kufanikiwa kuingiza bidhaa feki unongeeka kila siku. Kwa mfano ukimwambia mteja kuwa ataweza kutambua bidhaa feki kwa tofauti ya jina(brand) hii inakosa nguvu sana kwani kwa sasa biashara ya Ulimwengu imejawa na wazuaji wa nembo zao(Own brand).
Hivyo tajiri anaweza kuagiza tani za vitasa toka Uchina akavipa jina la hardware yake. Ila hoja yetu ya ‘ufeki’ ipo katika malighafi zilizotumika kama zinakubarika katika soko la Tanzania.
Kwa kuangalia uwingi wa bidhaa za uchina katika nchi za magharibi na jinsi zinavyojipenyeza huko na kupapatikiwa na walaji kwa ‘upenyo’ wa bei ni wazi kuwa hatuna njia zaidi nasi pia kutumia bidhaa kutoka Uchina.
Ila kama nilivyokwisha kusema, hapa ni wauzaji wetu ndiyo walio kuwa na kasoro, ama hawana ufahamu na viwango vya nchi kwa bidhaa mbalimbali pale wanapoagiza. Suala la viwango vya ubora ni suala ‘tete’ na ni wazi kuwa viwango vya Tanzania, si sawa na Uingereza, ingawa kuna viwango vya bidhaa vya Ulimwengu, pia kuna nchi wanatumia viwango vyao bila hata kujali hivyo vya ulimwengu.
Hatuwatetei wajasiriamali ila yatupasa kupeleka elimu ya viwango kwa waaagizaji wa bidhaa toka nje, si kwa walaji tu. Inawezekana pia kati ya waagizaji ni wachahe wenye ufahamu juu ya viwango au kuona ‘muongozo’ wa viwango wa TBS, katika saketi inayotakiwa Tanzania iwe na ubora gani, kwa malighafi na uzito upi.
Pendekezo letu katika vita hii, mosi ni kuundwa kwa chama imara cha haki za walaji na pili kutungwa kwa sheria zenye kumpa mlaji haki za kiuchumi pale itakapogundulika kuwa bidhaa aliyotumia haikuwa na viwango husika,maana kwa sasa vinachomwa moto tu, vipi waliotumia wanapata malipo yoyote?Jibu ni kuwa hatupati
Pia tunapendekeza kutolewa kwa elimu ya viwango kwa waagizaji wa bidhaa toka nje ya nchi wafahamu kabla hatujawahukumu.
Ingawa Uchina ni mdau mkuu kwa maendeleo ya Tanzania kama nilivyokwisha kuonesha, yatupasa kuungana kama nchi kusema ‘HAPANA’ kwa bidhaa feki toka Uchina kwa masilahi ya nchi yetu. Tukiungana tunaweza.

No comments: