Monday, January 4, 2010

Sekta changa ya 'mboga mboga' na kitanzi cha VAT

Hivi karibuni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imenukuliwa na Gazeti la Serikali Daily News la tarehe 26 Desemba 2009 kuwa limepitisha ‘tozo’ mpya ya kodi ya ongezeko la thamani ,VAT, kwa wauzaji wa masoko ya nje hata kama muuzaji ana pato lililochini ya milioni 40.
Mabadiliko haya yanatekelezwa kwa utetezi wa masilahi ya kulinda nchi hii ni kwa mujibu wa TRA. Safari hii VAT itatozwa hata kwa wale wajasiriamali wadogo, lakini tatizo si VAT, ila ni marejesho kuwa ‘yanabagua’. Kimsingi mlipaji wa VAT ni mlaji, kwani muuzaji hurejeshewa malipo yake, lakini hawa wadogo waliochini ya milioni 40 hawana cha ‘kurejeshewa’.
Tatizo hili la kukosa kuwarudishia ‘wajasiliamali’ ndiyo kiini cha makala haya. Tutajaribu kuangalia manufaa ya dhana hii kwa Taifa na pia tutatoa mchango wetu kuhusu hili.Ingawa tunaaamini hiki inawezekana ikawa ni kilio cha samaki machozi huenda na maji anaimba gwiji wa muziki wa dansi, Dr. Ramadhani Mtoro Ongala.Lakini tunaamini sauti yetu itasikika.
Kati ya sekta zilizoathirika na marekebisho haya ya kisheria ya VAT, ambayo kimsingi kamishina wa kodi ananguvu kisheria kuamaua nani alipe VAT ingawa sheria yenyewe ya inasema ni yule mwenye zaidi ya milioni 40.Sheria ya VAT kifungu sura ya 148 kifungu 19 kifungu kidogo 4, kinampa uwezo Kamishina wa Kodi kuamua nani alipe ingawa utakuwa upo chini ya milioni 40.
Ni vyema ikaeleweka wazi kuwa hatuna nia ya kujenga wala kutetea jamii ya watu wasio penda kulipa kodi, ila tunashaka na maamuzi haya kama kweli ya nia kuona nchi hii inang’ona ‘nanga’ kiuchumi.
Jitihada za kupambana na anguko la uchumi duniani imeona serikali nyingi zinahamasisha kuuza katika masoko ya nje, na zinatoa motisha ya punguzo la kodi kama si kufuta kabisa. Itakumbukwa pia katika siku za mwanzo za msukosuko huu kauli iliyokuwa inapigiwa chapuo na Marekani ni kuhakikisha nchi hazifungi mipaka yake ya kibiashara kwa kutumia njia kale (traditional barriers kama vile kodi za aina yoyote)
Ni kweli kuwa Tanzania inahaha ikitafuta kujinasua kutokana na msukosuko wa kiuchumi wa dunia kwa kutafuta kuongeza pato lake. Lakini kwa njia hii ya kutoza wauzaji wa nje na hasa wauzaji wa sekta changa ya mboga mboga ambayo imejawa na wazalisahjo wadogo wengi hauna mwisho mwema.
Sekta hii changa ya mboga mboga (horticulture) lakini katika makala haya tutajumlisha pia na floriculture, pale tutakoposema mboga mboga inakadiriwa tani kati ya 15 hadi 40 husafirishwa kwa wiki, kuelekea masoko ya ng’ambo kwa kutumia usafiri wa anga.
Hii ni bidhaa inayohitaji kufika sokoni haraka kutokana na tishio la kuharibika haraka (fast moving consumer goods). Kupitia chama chawazalishaji wa mboga mboga (TAHA) Tanzania ilijinyakulia tuzo ya shaba katika maonesho ya Amsterdam kwa mara ya kwanza wakati tukiwa washiriki kwa mara ya kwanza mwaka 2007.
Ikiwa inaleta chumo la dola milioni 50 kwa mwaka, na kuajiri watu wanaokadiriwa kufikia 10000, huku zaidi ya kampuni 20 zikiaminika kushiriki katika sekta hii. Ni wazi kuwa inahitaji kuangaliwa vizuri. Tanzania inakila sababu ya kuilinda sekta hii inayochipua kwa kuipa motisha lakini yanayotokea nchini ni kinyume chake.
Uzalishaji mkubwa wa mboga mboga upo Arusha, Kilimanjaro, lakini mikoa mingine kama Morogoro, Mbeya, Rukwa ,Tanga na Iringa nayo inafanya vyema na inakila hali ya kijiografia kuiwezesha kufanya vyema.
Mwenendo wa soko la ulimwengu wa mbogamboga katika nchi za Ulaya ni wenye kutia matumaini kwa siku za baadaye wa sekta hii nchini. Hii inatokana na ukweli kwamba katika Ulaya kuna mwamko wa kiafya kupinga ulaji wa nyama nyekundu kuanzia miaka ya kati ya sabini hali iliyopelekea kukubalika kwa nyama nyeupe kama kuku na nguruwe miongoni mwa watu wazee.
Uoga wa ulaji nyama ulishamiri zaidi baada ya kuibuka kwa ugonjwa kichaa za ng’ombe, BSE( Bovine spongiform encephalopathy) katika Uingereza miaka ya 1996.
Mwenendo wa soko umeimarika baada pia kuongezeka kwa hali ya kulinda wanyama, na ongezeko la walaji majani katika nchi hizi kwa imani za kisayansi. Kwa mfano tangu ongezeko la vitisho hivi soko la walaji wa nyama wa Uingereza umepungua ukiwa ni kilo 14.4 tu kwa mwaka.
Ni wazi kuwa Tanzania inazewa kunufaika na hakuna shaka kuwa sekta hii changa inahitaji kupigiwa ‘chapuo’ kuhakikisha kuwa tunakataa kuwa wauzaji wa wanunuzi wasio makini kama vile Kenya ambao hununua vitunguu na matunda toka kwetu kisha kuuza Ulaya kwa faida kubwa.
Hili la tozo ya VAT ya asilimia 18, ambapo hawa wadogo hawarejeshewi imevunja nguvu za wajasiriamali wanaohaha usiku na mchana kuona wanaunganishwa na soko la nje, na ni wazi kuwa si njia sahihi. Kwani Tanzania sasa hivi haihitaji kutoza kodi kubwa na hasa wauzaji wa nje ili kuongeza pato inahitaji kuhahakikisha wajasiriamali hawa wanauza katika soko la nje na wanapata suluhu katika mashaka yao.
Iweje wakubwa walio na pato kubwa la milioni zaidi ya 40 warudishiwe lakini wadogo wasirudishiwe? Hii si sawa. VAT analipa mlaji lakini safari hii wamekandamizwa wazalishaji tena wa sekta changa, kwa kigingi cha kulinda masilahi ya Taifa.Taifa gani linalolindwa wakati utekezaji wa sheria hii ni wazi kuwagawa watanzania, na hasa hawa wakulima wadogo wa mboga mboga!
Tanzania inavyanzo vingi vya kodi na tangu tumeamua kuchauga mabadiliko ya kiuchumi miaka ya 1980 ya soko huria, nia ilikuwa kuona utawala wa kodi unakuwa huru na wa haki.
Lakini safari hii tunaona kodi inakuwa kandamizi tena wakati wa hangaiko la Uchumi. Sekta hii ya mboga mboga nayo pia imepata msuko msuko, huku la soko la Uingereza likiwa limepungua kwa asilimia 20 kwa bidhaa toka Tanzania.Ni wazi kuwa sekta hii inahitaji kulindwa hasa ukizangatia kuwa ni wakulima wadogo ndiyo wanaoshiriki katika kuzalisha bidhaa hizi katika maeneo mengi nchini.
Kukosa pato kwa TRA kusihusishwe na kubinya walipa kodi waliojitoa na kukubali kulipa kodi kwa maendeleo ya Taifa. Na hili ndilo tatizo la Tanzania, mara zote nchi inakuwa iko mbele kuhakikisha inawakamua wale walipa kodi na si kuziba mianya ya uvujaji wa kodi.
Hivi karibuni gazeti la serikali Daily News la tarehe 20 Desmeba 2009, lilikuwa na taarifa kuwa wauzaji wa magogo na mbao nje ya nchi walikuwa wanataka kupunguzwa kwa kodi. Ombi ambalo serikali kupitia Waziri wa Viwanda na Biashara, Dr. Mary Nagu amekubali kulipokea na kuliona, huku Naibu wa Waziri wa Maliasili akilipigia ‘chapuo’ kuwa nchi inahitaji kupunguza tozo ya mbao na mazao mengine ya misitu ili kuongeza pato la taifa na hasa mauzo ya nje. Kwa sasa tozo ni 200,000/= kwa meta za ujazo.
Cha ajabu hapa tunapigia chapuo uvunaji wa maliasili ambayo ikivunwa ni hatari kuliko ikiachwa. Na wala hakuna anayeomba punguzo katika ‘mboga mboga’. Makala haya inaweka wazi kuwa Tanzania haiitaji kupunguza kodi kwa ajili ya mavuno ya misitu kama magogo na mbao, isipokuwa inahitaji kuweka ‘udhibiti’ ili kupambana na upotevu unaokisiwa kufikia dola milioni 58 za kimarekani kutokana na udanganyifu na utoroshaji wa mavuno ya misitu katika Asia na hasa Uchina.
Pia kuna eneo jingine nalo ni la uuzaji wa pombe kali(spirit) ambako TRA inaweza kuziba mianya ya upotevu na si kuwabinya wajasiriamali. Inakadiriwa zaidi ya bilioni 2 za kitanzania zinapotea kutokana na wakwepaji wa kodi wanaouza pombe kali. Na hivi karibuni kuna hawa wakurugenzi zaidi ya saba ambao TRA inawatafuta kwa kukwepa kodi ya uuzaji wa pombe kali.
Hatujitaji kupandisha kodi Tanzania ili tuweze kuendesha serkali yetu, changamoto ni katika kukusanya kodi kwa ufasaha na kwa uwazi.
Sekta ya mboga mboga inahitaji kung’oa nanga, ni vizuri ikiachwa ikue na ni vema kuiongezea motisha na si kuizima kila inapochipua. Chonde TRA angalieni mara mbili uamuzi wenu wa kutoza VAT ya asilimia 18 kwa mizigo inayosafirishwa kwa ndege nje ya nchi na wajasiriamali katika sekta ya mboga mboga.
Kwa sasa kuna madai kuwa wajasiriamali wameanza kutumia Kenya kusafirisha mizigo yao, ingawa hatuna takwimu za wazi, lakini kuna vitu tunapoteza. Njia ya Kenya haina mwisho mwema kwani mwaka 2007/2008 hasara ya bilioni moja ya kitanzania ilipatikana kutokana na kukatishwa kwa ruti kufuatia mapigano ya wenyewe kufuatia sintofahamu ya matokeo ya Uchaguzi.
Tunahitaji kufikira mara mbili katika kipindi hiki cha ‘msukosuko’ wa uchumi tunahitaji kupandisha kodi au kupunguza na hasa bidhaa tunazouza katika soko la nje. Jibu sahihi ni kwamba hatuhitaji kupandisha kodi kwa bidhaa za kilimo.
Yatupasa kuilinda sekta hii changa, kwa maendeleo ya watanzania na hasa waishio vijijini, ambao wanajishughulisha na uzalishaji wa mboga mboga. Na si kuwapigania wavuna magogo na wauza mbao.

No comments: