Wednesday, October 21, 2009

Kilimo kwanza na changamoto ya nishati katika chai

Tatizo la nishati katika ‘chai’ changamoto ya KILIMO KWANZA

Takwimu zilizowahi kutolewa na Shirika Kongwe la Umeme Tanzania (TANESCO) baada ya kuibuka mjadala wa ‘tozo’ kubwa kwa ‘unit’ kwa watumiaji, ilikuwa ni ya kujigamba kuwa wateja wa Tanzannia ndiyo wanaokula umeme kwa bei ya chini katika Afrika Mashariki, 0.08 US huku Kenya na Uganda walaji wakitozwa 0.16.
Tanesco walitoa taarifa hizi kupitia Ofisa Uhusiano wa wakatia huo zilizojaa uhakika wa kutatua tatizo la nishati na mara zote zilikuwa ni za kutia matumaini. Pamoja na matumaini hayo yote na bei kuwa ndogo katika ukanda huu bado Tanzania ni nchi yenye watumiaji wachache wa Umeme kwa asilimia 10 ya wananchi wake ndiyo wana umeme.
Katika nchi yenye watu zaidi ya milioni 40 kwa takwimu za 2008 za Benki Kuu ya Dunia, ni wazi kuwa, ukuaji wa sekta nyingine zinazoendana na nishati utabaki kuwa nyuma. Sekta ya viwanda ni moja wapo ambayo inaonekana kuchangia kiasi kidogo katika pato la taifa, na hili ndilo hasa linachangia katika kutufanya tuwe watu wakuuza nje mazao ‘ghafi’.
Ukiwa na mashaka ya upatikanaji wa nishati, niwazi kuwa utakuwa na uwezo mdogo wa kuvutia wawekazaji katika viwanda, hali inayochangia kabisa kudorora kwa kilimo. Nishati ni Viwanda, Viwanda ni Kilimo, basi Kilimo nacho ni Nishati! Uhusiano huu wa wazi unaweza kufanya mnyororo usikamilike endapo mahali popote panalegalega hufanya kukatika kabisa.
Sekta ya Kilimo bado haijaweza kuvutia mitaji toka nje na jitihada nyingi zinafanywa katika kuboresha hali ya wawekezaji katika kilimo ikiwa kubadilisha sheria ya ardhi ili kutoa umiliki wa muda mrefu wa hadi miaka 99. Mageuzi pia yanatokea katika sekta za fedha ili kuchochea mikopo katika kilimo.
Kitaasisi kuna maeneo ya uwekazaji kama EPZ ( Economics Processing Zone) ambayo yanampatia ‘motisha’ mwekezaji ya kufanya biashara kwa miaka kumi bila kutozwa baadhi ya kodi, ikiwa pia anatakiwa kuuza asilimia 80% katika soko la nje. Jitihada zipo nyingi lakini bado tunaendelea kushuhudia asilimia 5 tu ya FDI katika kilimo, na ushiriki wa Tanzania katika AGOA ndiyo unatoa mwanga kamili jinsi ya ugumu wa kukitoa kilimo chetu kilipo bila nishati.
Jitihada za ubinafsishaji bado hazijazaa matunda kwani wengi waliouziwa viwanda wamegeuza ‘maghala’ ya kukusanyia mazao na kuuza nje ya kiwa ghafi, mazao kama korosho bado asilimia 90 inasafirishwa ‘ghafi’ katika masoko ya ASIA na kubanguliwa kisah kuuzwa katika Ulaya, kwa faida nono!
Rais Mstaafu wa awamu ya tatu Mzee Benjamini William Mkapa aliwahi kuwapa changamoto wadau wa korosho wakatika fulani katika kongamano la Kibaha Pwani pale alipokuja na korosho toka Uingereza ambayo haifiki hata robo kilo lakini ikiuzwa kwa zaidi ya dola 4 za Marekani. Hata kama ukisema kwamba katika kila kilo moja ya korosho kuna asilimia 70 ya ‘makapi’ na asilimia 30 ndiyo inayobaki safi kwa kuliwa, niwazi kuwa bei ya kilo 350/= wanayolipwa wakulima wa Newala Tanzania ni ndogo mno!
Hakuna njia nyingine ya kuwakomboa wakulima wetu zaidi ya kuhimiza uwekezaji katika viwanda, vidogo, vya kati na vikubwa, lakini mashaka yakuja na hasa suala la uhaba wa nishati tulio nao!
Hata maoni yako yawe nini, hakuna haja ya kulaumiana tunahitaji mawazo ya pamoja katika kutatua uhaba wa nishati nchini! Gazeti la Mtanzania Daima la tarehe 20.10.2009 linahabari juu ya ‘kukosekan kwa soko la chai’ kwa wakulima wa Milima ya Usambara baada ya kuibuka mgogoro wa ‘msitu’ ambao unatoa kuni kwa ajili ya nishati.
Wakulima ambao wanategemea kiwanda cha Mponde wanapata 6,000, hivyo kufungwa kwa kiwanda hiki ni mashaka kwa familia hizi. Niwazi kuwa ‘steam’ ndiyo teknolojia inayotumika kwa viwanda vingi vya chai vilivyopo mbali na miundo mbinu ya gridi ya Taifa, na si Tanzania tu , Malaysia pia wanatumia kuni, lakini wapo mbioni kubadili na kutumia umeme wa maji.
Chai siyo sawa na ‘tikiti maji’ ambalo linaweza kukaa zaidi ya masaa 24. Chai inahitaji kuvunwa na kufikishwa kiwandani katika kipindi kifupi ndani ya masaa 24 yakizidi tunaongea lugha nyingine.
Tatizo la nishati limeanza tangu 1983 katika Tanzania kwa upande wa viwanda vya Chai, na tangu wakati huo tumeshuhudia viwanda vingi vikigeuka ‘mahame’
Familia ya MULA ndiyo wamiliki wa kiwanda hiki cha Mponde Tanga, lakini pia wanamilki kiwanda cha chai cha Lumbele, kilichopo Iringa ambacho nacho pia kipo katika mgogoro wa kugombea msitu wa nishati ya kuni kwa ajili ya kuendesha mitambo ya chai. Tanga wanagombea na wanakijiji msitu wa ‘SAKARE’ na Iringa ni msitu wa ‘Lyembela’ kwa mujibu wa gazeti la Mtanzania Daima, la 23. Mei, 2008.
Ingawa katika mgogoro wa Iringa kiwanda kilishinda mahakamani katika kesi iliyoendeshwa mahakama ya biashara na kuwa wamiliki halali, mgogoro wa Tanga bado unafukuta na Waziri Mkuu Mizengo Kayanza Pinda, mtoto wa mkulima anaufahamu!
Huu ni mgogoro wa nishati kati ya wakazi na viwanda na safari hii ni kugombea ‘kuni’. Kuni ni mgogoro katika viwanda vingi , hata MeTL kupitia kiwanda chao cha nguo cha Morogoro kilishaingia katika mgogoro huu wa nishati ya kuni, na kutishia uzalishai wake.
Tanzania inazalisha 1% ya chai ya ulimwengu na ni ya nne barani Afrika kwa kuzalisha chai.Nchi kwa sasa ina mkakati wa kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani 55,000 kufikia 2013. Chai kwa sasa inaonekana kupanda katika kuingiiza fedha za kigeni Taifa, katika msimu wa 2006-07, dola milioni 39.4 zilikusanywa zikipanda kutoka dola milioni 27 kwa msimu wa 2005-06.
Hili la nishati linaonekana kuwa ‘mwiba’ mkali kwa sekta ndogo ya chai, lazima tujipange kutafuta suluhu kwa wakulima wadogo wapatao 32,000 wanaolima chai nchini na hasa wale walioonesha njia na nia ya kuenda mbele kupitia ushirika.
Basi yatupasa kufahamu kuwa nishati ni changamoto kubwa kwa ‘KILIMO KWANZA’ yatupasa kujipanga kutatua tatizo hili la nishati si kwa chai tu bali viwanda vingine pia. Tuache ‘malumbano’ katika nishati tujipange kama nchi, nani alifanya kosa wapi haina maana kwa sasa, tufikirie kupata nishati kwanza.
Tusipokuwa waangalifu tunaweza kujikuta tumetumia muda mrefu katika kujadili watu na kusahahu kuwa bado tuna tatizo nalo ni nishati.

No comments: