Friday, October 23, 2009

Kuelekea usawa tunahitaji tahadhari

Siku za karibuni katika mikutano,makongamano,semina na warsha mbalimbali watu mashuhuri wamesikika wakiweka wazi ya kuwa nafasi za ushiriki wa wanawake katika bunge zinahitajika kuongezeka hadi kufikia asilimia 50.

Taasisi moja ya wanaharakati wanaojihusisha na mabadiliko katika jamii ya kitanzania wakati wa maandamano yaliyokuwa yameaandaliwa kwa kumpongeza Dk. Asha Rose Migiro ambaye kwa sasa ni Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa iliweka wazi juu ya kuhimiza kuongezwa kwa nafasi za wanawake hadi kufikia 50% katika nyumba za maamuzi.

Gazeti la Mtanzania la siku ya ijumaa tarehe 9 machi mwaka 2008 likimnukuu Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia na Watoto; Mheshimiwa Sophia Simba liliandika kuwa nyongeza ya nafasi za wanawake bungeni ni lazima kufikia hamsini asilimia.

Hili la nyongeza ya wanawake katika bunge ni suala ambalo halina ubishi na ni la kupigiwa chapuo katika jamii ya watanzania katika kuona wanawake walioachwa nyuma kwa muda mrefu katika mchakato wa kupigania maendeleo ya nchi hii wanashiriki vilivyo katika kila harakati.

Jamii ya watanzania wanaona na kusikia ndugu zetu wa kike wakionewa,wakinyanyaswa na kudharauliwa kwa vile tu ni wanawake. Kwa ujumla wanawake ni wa watu wanaataabika katika kila jambo linaloihusu jamii yetu hii.

Hivyo kufanya nia yoyote itakayo pelekea mabadiliko yatakayo lipa nafasi kundi hili kubwa la watu katika idadi ya watanzania ambao wanakisiwa kuwa zaidi ya nusu ya watanzania wote kuwa ni jambo la lazima. Hili ni kwa mantiki ya ujenzi wa Tanzania yenye neema.

Hakuna anayeweza kulipa gharama za mateso na manyanyaso wanayokutana nayo wanawake katika juhudi zao za kila siku kwa leo hii katika Tanzania.Ingawa ni wazi kuwa hali hii ya kuwaweka nyuma wanawake katika kila jambo ni suala lililo na asili toka enzi za ukoloni. Kutokana na ukweli huoa 'affirmative action' kuelekea usawa katika jamii yetu kuwa ni jambo la maana na kuhimizwa kwa nguvu zote.

Ila katika kitimiza nia hii itakayosaidia katika kupunguza makosa yaliyotokea muda mrefu katika jamii yetu nilaizma tahadhari kuchukuliwa hasa kwa kufahamu ukweli kuwa kundi lililonyuma katika Tanzania ya leo si wanawake tu.

Kuna walemavu,vijana na masikini,Hivyo basi katika kutimiza lengo hili la nafasi za upendeleo ni lazima tujiridhishe kwa kuangalia pia hao wanawake wanaoingia katika nafasi hizo za upendeleo wasiwe tu toka katika kundi lilelile la jamii iliyokwisha 'nufaika'.

Ukweli lazima uwekwe wazi katika hii asilimia 50% wanawake vijana watakuwa asilimia ngapi? Uwakilishi wa wanawake walemavu utakuwa wa asilimia ngapi?

Pia hili nalo ni la kujiuliza pia katika wanawake hao,wanawake wa 'KIISLAMU' watakuwa wangapi? Hili ni jambo la wazi na wala si kwa ushabiki tu. Uwakilishi huu lazima uwe unaochukua watu wa kutoka makundi yote katika jamii.

Basi nia hii lazima iweke wazi juu ya ushiriki wa makundi yaliyo achwa nyuma kwa kipindi kirefu miongoni mwa wanawake. Na wala isije ikawa mwisho wa safari tunaona sura zile zile katika,uongozi huo. Huu hautakuwa 'usawa' kwa maana pana ya usawa ni lazima tuweke wazi hili mapema. kwani leo pia tunapigia chapuo lakini wakati ukifika utaona majina yale yale yanapita.

Kwani tusipokuwa wakweli unaweza kuona nafasi hizi zikiongezeka wakipata wake wa wakubwa na watoto wao.Tena walio nz umri mkubwa huku ushiriki wa vijana ukiachwa kando.

Pia tahadhzri inahitajika kwani 'affirmative action' katika kuelekea usawa si kufikia 'idadi' fulani la hasha; bali kujiridhisha kuwa watu hao walio nje ya mfumo kwa muda mrefu wana sifa na kweli wameandaliwa kuchukua majukumu hayo.

Kwa mfano hauwezi kupigia kelele kwamba itungwe sheria inayohitaji ofisi ziwe za serikali au binafsi ziwe zinaajiri wanawake kwa asilimia fulani bila kwanza kuhakikisha kuwa wanawake wenyewewe wana ujuzi huo.Au kusema tu kila ofisi inakuwa inaajiri walemavu kwa idadi fulani bila kwanzn kuwa na maandalizi ya kuwapa ujuzi hao wanaotakiwa kuchukua nafasi hizo hivyo basi kufanya kila linalo amriwa kuwa halina maana.

Mchungaji Jesse Jackson katika waraka wake kwa vyombo vya habari wa mwaka 1995; alioupa jina 'Affirming Affrimative Action', anasema hatua za upendeleo katika jamii siyo 'quotas'- Kwa kuzingatia ukweli; utakuwa uvunjaji wa sheria kumpendelea asiye na sifa dhidi ya aliye na sifa. Kile 'affirmative action' inatupatia ni kutumia kwa malengo na dira ili kushirikisha nguvu kubwa zaidi ya jeshi katika kufanya kazi ( Tafsiri ni yangu)

Nchini kwa sasa juhudi zozote za kuelekea usawa hasa katika kupata kazi na nafasi za uwakilishi katika mabaraza mbalimbali ya kutoa maamuzi hayaweki wazi ni asilimia ngapi ya watu wanao wakilisha makundi ya kijamii ambayo yalinyanyasika na wanaendelea na mataabilko wanahitajika.

Yatupasa kuwa wakeli kuwa nasafi za upendeleo ziwe kwa wale waliokosa nafasi na si waliokwwisha 'neemeka' kutumia njia hii kuendeleza, unyonyaji wao usio na tija. Basi tahadhari inahitajika katika kuwaandaa wale walio nyuma kama wanawake kielimu, Chuo Kikuu Mzumbe kimeonesha njia kwa kudahili 50 kwa 5o ya wasichana na wavulana, huu ni mwanzo mwema kuelekea usawa kwa vitendo, na wengine waige!

No comments: