Friday, October 16, 2009

Kuuza rasilimali watu nje yahitaji tahadhari

Siku chache zilizopita Waziri wa Afrika Mashariki Didorus Kamala alinukuliwa na vyombo vya habari kuwa Tanzania iko mbioni kuwa na mkakati wa kuuza wataalamu nje ya nchi. Hili ni wazo zuri, kwani wakati wote kuna imani kwamba wale walio nje wataleta walu sehemu ya 'mafao' yao nyumbani ambayo kwa namna moja au nyingine yatainua hali za tulio nyumbani ambako umasikini wa kipato unatumaliza. Pili uzoefu wao katika shughuli za maendeleo tunaweza kuamishia nyumbani(Back Home Era) nasi tukabadili hali zetu pia kwa kuongeza ajira kama vile wakianzisha kampuni.

Ulimwengu unashuhudia mapinduzi ya kisayansi yanayotokea India kwa sasa katika teknolojia ya kompyuta na mawasilinao kwa ujumla, haya yote ni kwa ajili ya vijana waliokuwa uhamishoni na hasa nchi za magharibi kuamua kurudi nyumbani(Back Home Era). Sina hakika kama hili linawezekana kwa watanzania!! Ni suala la kusubiri muda.

Kwa sasa watanzania waliopo nje wanaleta kama dola milioni 14,mafao haya ambayo yakiwekwa katika takwimu za kipesa ni madogo ukilinganisha na jirani zetu kama Uganda dola wanaorudisha milioni 896 takwimu hizi ni za mwaka 2007.Pia yatupasa kushukuru. Yatupasa kufahamu pia kurudisha riziki nyumbani ni hali ya ‘moyo wa mtu’ na fadhila aliyonayo na wala tusiiwekee asilimia mia moja katika hili kuwa hali itabadilika endapo watanzania wengi watakuwa nje ya nchi.
Makala haya inatoa tahadhari ya wazi kuwa haikubaliani na Mheshimiwa Waziri na wazo lake kuwa na mkakati wenye tija na kupigiwa ‘chapuo’ kwa nguvu kwa hali ya sasa ya nchi yetu ilipo. Si kila jambo linalotokea kuwa na faida kwa wenzetu nasi yatupasa kulikimbilia. Hapana, na hasa chapuo katika kuuza madaktari wa tiba.
Nadharia rahisi ya mtu anayeweza 'kuuza'(Seeling) ni yule aliye na ‘ziada’ ( You cannot sell if you don’t have surplus). Swali la kujiuliza Tanzania yetu ya leo ina ziada ya wasomi kiasi nasi kujinasibu kuwa tunataka kuingia katika soko la kuuza rasilimaliwatu nje?

Tukijilinganisha na Uganda tunaweza kutafuta sababu za juu tu bila kupata kiini cha kwa nini hatuna wataalamu wengi nje ya Tanzania. Jibu ni kwamba hatuna watu walio na ujuzi stahili. Uganda leo hii wana tawi la chuo kikuu cha KIU (Kampala International University-Dar Campus). UDSM wakongwe kuliko KIU hawana tawi,Mzumbe wameweka tawi Mbeya. Lakini matawi haya ni ya shahada za kijamii si ya sayansi na hasa Udaktari.

Vyuo vya tiba bado haviajwa na udahili wa wanfunzi wengi nchini ingawa idadi yake kwa sasa ni vitano na hili ni kwa sababu ya gharama, na miundo mbinu hafifu kukizi mahitaji ya vyuo hivyo kuanzishwa nchini.
Tena maeneo ambayo Mheshimiwa anayapigia chapuo ni udaktari wa binadamu na uhandisi!Haya ni maeneo nyeti sana na uhaba wake unatisha. Hatumaanishi kuwa watanzania wasiende nje kutafuta kazi na kujiongezea uzoefu, la hasha ila yatupasa kuwa makini katika kuhakikisha tunaweka nguvu katika maeneo kweli ambayo ‘tunafaida ya kiushindani’.
Gazeti la serikali la Habari Leo la tarehe 16 Oktoba lina habari ya uhaba wa madaktari na wauguzi katika hospitali ya Mirembe iliyopo Dodoma, pia hospitali hiyo inahitaji wauguzi 150! Hospitali hii inapokea watanzania zaidi 6000 ikiwa na uwezo mdogo mno wa kutoa huduma. Napata kigugumizi hivi kweli linalozungumzwa na Mheshimiwa ni hoja iliyo katika wakati muafaka kwa Tanzania ya leo.
Kuna maeneo Tanzania inahitaji kwa hakika kuuza wataalamu wake nje,lakini unauza wakatika unadahili asilimia 2 tu ya watu wenye sifa ya kuingia chuo kikuuu. Natumaini hoja ilipaswa kuwa tunahitaji kuongeza nguvu katika elimu ya juu ili tuweze kuuza wataalamu nje.
Kuna maeneo watanzania yatupasa kuyaangalia kwa ‘jicho la tai’ kwani huko tunauwezo wa kufanya vizuri na si vibaya tukajaribu, kwa mfano walimu wa lugha ya Kiswahili. Tusipoongeza udahili na kujipanga sawasawa tutakuwa wachekeshaji, kwani wale tuliowafunza lugha hii adhimu, sasa ndiyo watang’ara kama wakufunzi. Simaanishi hakuna waswahili wanaowafunza waingereza ‘kiingereza’ ila lazima uwiano uwepo kati ya mwenye ‘chake’ na mdandiaji.
Hali ilivyo sasa wakenya wengi wanasoma Kiswahili na wanahitimu wengi chuo kikuu kuliko watanzania tunavyosoma katika ngazi ya shahada Kiswahili chetu! Hapa kuna tatizo nyumbani lazima tulitatue.
Libya imeweka wazi kuwa lugha ya Kiswahili ni kati ya lugha zinazopaswa kutumika nchini humo lakini hakuna walimu, sasa haya ndiyo maeneo tunayopaswa kuweka nguvu kwani tunafaida mlinganisho nayo na hayatatuathiri kimsingi.
Lakini hili la kuuza madaktari wa binadamu nje ni hatari hasa katika nchi kama yetu ambayo watu bado tunakufa kwa magonjwa yanayotibika kama malaria, tumbo, kifua kikuu.Bado wakina mama wanakufa kwa kukosa huduma nzuri wakati wa kujifungua,MIMBA sasa imekuwa ni kuchungulia kaburi!Mimba si ugonjwa lakini kwa vile hakuna wataalamu ndiyo haya yote, ya 108 katika ya akina mama 10000 Iringa wanakufa kila mwaka. Kila dakika kuna mtoto mchanga wa kitanzania anafariki, kisa yuko mbali na kituo cha afya.
Lindi bado inaongoza kwa vifo vya akina mama wajawazito, bado tushabikie kuuza wataalamu wetu nje si sawa . Sina nia ya kupinga wazo hili yatupasa kuweka nguvu katika maeneo yenye tija kwanza, pili yatupasa kuweka nguvu katika kudahili pia na si kama hali ilivyo sasa kisa dola milioni 14 zinapswa kuongezeka!
Bodi ya mikopo ilikuwa na nia ya kutoa mikopo kwa wanafunzi zaidi ya 60,000, sasa idadi imeshuka hadi 24,000! Ni wazi kuwa mambo si mazuri kwani maelfu wamekosa udhamini si kama hawana sifa la hasha ni uhaba wa fedha. Katika hali kama hii kuna maeneo yatakosa wataalamu, Hivyo kupigia chapuo kuuza wataalamu nje tena wa afya au wahandisi ni hatari.Tena katika nchi ambayo vijana hawapendi tena kusoma masomo ya sayansi licha ya kuwepo udhamini wa asilimia mia moja.
Tusiwe kama wamalawi ambao wataalamu wake wa tiba ilio wasomesha kwa shida na gharama kubwa wapo wengi katika Uingereza kuliko walivyo katika MALAWI nzima, kisa pesa kurudisha nyumbani.
Kimsingi kurudisha hela nyumbani ni moyo wa mtu si kwa vile amewaacha watu nyumbani ndiyo atawapatia chochote kitu.
Mifano mizuri tunayo hapa hapa Tanzania,kuna watu wengi tumesahau wapi tulikotoka mara tu baada ya kuingia katika ofisi zenye kiyoyozi na kuendesha magari ya mikopo ya mitumba kutoka Japan, hatuna fadhila na watu waliotulea na hasa wazazi tunawaacha wakihenyeka katika siku za uzeeni!
Msimamo wetu ni kwamba yatupasa kupima mara mbili zaidi faida ya kipato na madhara ya kushabikia mchakato huu na kuweka nguvu ya kuuza wataalamu wetu nje. Yatupasa kuongeza kwanza nguvu katika udahili kwa elimu ya juu, kisha tuanze na walimu wa kishwahili na si kila sekta ni hatari.

No comments: