Friday, October 23, 2009

Ukosefu wa soko la uhakika ni kitanzi kwa ukuaji wa sanaa ya uchongaji

"Tumelalamika katika vikao mbalimbali vya kimkoa kuhusu ukosefu wa soko la vinyago nakuiomba serikali ya mkoa itusaidie;lakini kilio chetu kimekuwa hakisikiki"hayo ni maneno ya Mzee Joseph Rashid Adrea wa kikundi cha Jikwamue;kilichopo katika manispaa ya Mtwara eneo la Magomeni karibu na Kanisa Katoliki la Kristu Mfalme.

Mzee Rashid yupo katika sanaa ya uchongaji wavinyago kwa miaka 40 sasa.Anabainisha kuwa sanaa hii aliyoirithi toka kwa baba yake kwa sasa haina nafasi yakuvutia vijana katika mkoa wa Mtwara;kwa vile watu wengi wanaona hakuna sababu ya kuwapeleka watoto wao kujifunza kitu ambacho hakitaweza kumpatia riziki.

Vinyago vyao vipo katika mitindo tofauti kama 'ujamaa' ambacho ni muunganiko wa watu wengi walio pamoja wakiwawameshikana kwa urefu,'mawingu' huu hauna sura isipokuwa ni maumbo tu ya kitu husika,'nandenga' kwa kiswahili ni shetani,kitashwira inafanana hasa na michoro ya Tinga Tinga,pia huwa wanachonga vinyago vya dini kama misalaba,Yesu na Maria na mingine mingi kutegemeana na matakwa ya mteja.

Mtwara ni miongoni mwa mikoa ambayo inakabiriwa na tatizo la ajira hasa kwa kufahamu kwamba sanaa hii ya uchongaji ingeweza kuondoa kundi kubwa la vijana ambao wapo 'vijiweni' kwa kuwapa ajira lakini ukweli wa mambo haupo hivyo.Mtwara haina viwanda,kilimo ni cha msimu basi soko la uhakika kwa vinyago lingeweza kukomboa wanamtwara toka katika umasikini.

Hali ya kukosekana kwa soko la uhakika haikuwepo katika siku za nyuma kwa wachongaji wa vinyago katika Mtwara. Mzee Rashid aliyeanza sanaa hii mwaka 1966,anasema historia ya ununuzi wa vinyago Mkoani Mtwara ilianzishwa na kasisi wa kikatoliki wa Kijerumani anayemtaja kwa jina moja kuwa aliitwa 'Keki'.

Mjerumani huyu ndiye aliyewafumbua macho kuwa vinyago ni mali katika mkoa wa Mtwara kwenye miaka ya 1968. Keki alipofariki wahindi walichukua nafasi,lakini walilegalega na hatimaye walishindwa. Katika miaka ya 1976 walianzisha chama chao;Makonde Carving; kilichokuwa kikinunua vinyago katika maeneo mbalimbali ya mkoa huu.Nacho kikafa kibudu!

Hali ilibadilika katika miaka ya 1990 pale kasisi wa kanisa la katoliki la mtakatifu Paulo;Padri Edelfonse (Marehemu) alipojitokeza kununua vinyago kwa kila siku ya alhamisi.Vinyago hivi vilikuwa vikisafirishwa Ulaya na hasa Ujerumani.Lakini Tangu kifo cha kasisi huyu mambo yamekuwa magumu kwao na hali yao ya kipato tangu kifo cha kasisi huyu hali imekuwa ikizorota siku hadi siku.

Ukiacha wanunuzi wa nje wateja wandani wanakuja kununua vinyago lakini si kwa kasi kubwa na wala si wakutegemea. Viongozi mbalimbali hununua vinyago kwao wakitembelea Mtwara.Mzee Rashid anamtaja Jaji Mkuu Mstaafu Banabars Samatta aliwahi kununua vinyagovyake mwaka 2004,pia aliwahi kuweka nakshi katika sebule nyumba ya Waziri wa Usamala wa Raia wa zamani Mzee Bakari Harith Mwapachu.

Mzee Yustin James wa kikundi cha sabasaba katika manispaa ya Mtwara naye anatoa kilio kile kile cha kukosekana kwa soko la vinyago ndiko kunakozidi kuwadidimiza kimaisha. Ujuzi huu wa Mzee Yustin 'amerithi' kwa baba yake mwaka 1968,hali ambayo anasema sasa hivi ni ngumu kumrithisha kijana wake kwani fani hii sasa hivi ni majuto matupu.

Kijana anaona wazi kuwa hakuna unafuu wowote wa maisha atakaoupata kutokana na yeye kuwana ujuzi wa uchongaji hasa akiangalia Mzee wake anavyoteseka kwa kukosa soko la vinyago la uhakika.

Hili la kukosekana kwasoko linaoonekana kufanya kuwa ndiyo mwanzo wa mwisho wa sanaa ya uchongaji wa vinyago vya mpingo mkoani Mtwara na hasa kwa kufahamu wazi kuwa hakuna damu changa inayojifunza sanaa hii kwa sasa tofauti na zamani.

Mzee Rashid anasema umaarufu wa vinyago wa Mtwara haupo Mwenge Dar-Es-Salaam,ila hii ni sanaa ya 'makonde' na utambulisho wa kabila hili nje na ndani ya nchi,basi serkali inapaswa kubuni mbinu bora katika kuhakikisha inaendelezwa.

Msanii Danieli Mkalunde wa kikundi cha saba saba anasema hali ya soko si nzuri kwa sasa huku akitolea mfano wa kuwa walinunua mti wa mpingo mwaka 2004,lakini hadi leo hawajamaliza kuchonga kwa vile hakuna wateja wa sanaa zao.Hili linaonesha wazi kuwa soko la vinyago linazidi kuporomoka kila siku katika Mtwara.

Kilio kingine cha wasanii hawa wa vinyago ni bei ya mti wa mpingo kuwa ni ghali na wao hawaimudu bei ya shilingi 75,000.Nikiwauliza kuwa serikali imeongeza bei ya mpingo,wanasema hawana taarifa lakini lililowazi ni kuwa bei ya zamani ilikuwa inawashinda basi hata hiyo mpya wataweza wageni na kampuni kubwa na si wachongaji wadogo kama wao.

Akiliongelea suala hilo kwa uchungu Mzee Rashid anasema maofisa wa maliasili siku hizi wala hawajali katika kiwanda chake cha Jinasue,kwani walikuwa wanachukua kodi ya shilingi 100,000 kwa mwaka.Anadai aliwahi kuwauliza maofisa hao kuwa wanafanya juhudi za kumkamua ng'ombe ambaye hawafanyi juhudi zozote za kumlisha kwa kumtafutia soko la sanaa zake.

Kwa ujumla wao hawana kipingamiza na kupanda kwa kodi ya mpingo lakini serikali ilipaswa kwanza kuwatafutia soko la uhakika kwa bidhaa zao.Na si kupandisha kodi,kwani kama wao wasanii watashindwa kununua mti wa mpingo huku soko la kazi zao halipo.

Mapendekezo yao ni kuwepo kwa kijiji cha sanaa ya vinyago katika Manispaa ya Mtwara;pia kjiji hicho kiwe na wasanii wengine kama wachoraji;ili kupunguza adha kwa wateja wanaotembelea Mtwara kuweza kununua sanaa zao kwa urahisi kama vile ilivyo kijiji cha makonde Mwenge.

Kwa sasa wasanii hawapo pamoja katika manispaa ya Mtwara hivyo kuwa kero kwa wateja wao kwani hulazimaka kutembea bila uhakika wa kuwakuta wachongaji.

Pia wanatoa changamoto kwa serikali kupitia wizara ya maliasili na utalii kukuza na kuhifadhi sanaa hii ya uchongaji wa vinyago kwa kuwatafutia masoko ya uhakika wachongaji hawa wa mkoa wa Mtwara. Hili lisipopatiwa suluhu sanaa hii iliyolipatia taifa sifa na umaarufu mkubwa Duniani itapotea na wala wasindanganyike na wachongaji wachache wa Mwenge kwani wale wanaowaona Mwenge walifunzwa Mtwara ndipo wakaja huko.

Sasa kama hakuna 'kuni' katika jiko la wasanii hawa litazimika.Na 'kuni' ni kupatikana kwa soko la uhakika kwa wachongaji waliopo Mtwara.Vinyago ni utambulisho wa Mtanzania na kila mgeni mkubwa wa kitaifa nayeingia au kuondoka zawadi ya sanaa ya vinyago imekuwa ikitolewa na Rais, Makamu wa Rais au Waziri Mkuu. Hii ni ishara ya wazi kuwa inaheshima, basi yatupasa kuheshimu pia kazi hii kwa kuwatafutia soko la uhakika wasanii hawa wa Mtwara.

1 comment:

Unknown said...

I would like to be in touch with up coming artists from Jikwamue group. Thanks Omary (omagambo@yahoo.com)