Sunday, October 25, 2009

Mwangwi wa jina batili 'mafua ya nguruwe' na biashara ya minofu ya nguruwe

‘Makosa yamekwishafanyika , na hakuna anayeweza kurudisha imani ya wateja kwa haraka minofu ya nguruwe na hasa ya dola 20 kwa nguruwe….sijui ni nani alileta uzushi huu wa ‘mafua ya nguruwe’, wanalalamika wakulima wa jimbo la Minesota,Marekani jimbo linaloshika nafasi ya tatu katika biashara ya nyama ya nguruwe na bidhaa zake.
Tangu kuibuka kwa ugonjwa huu, vyombo vya habari na wataalamu wa afya duniani wamejikuta wakiuita kwa jina ambalo wakulima na wataalamu wa magonjwa ya wanyama hawakubaliani nalo, nalo ni ‘mafua ya nguruwe’ (Swine Flu).
Lililowazi ni kwamba imani ya walaji hasa wa Ulaya imepungua tangu kutokea kwa kosa la kuuita ugonjwa huu ‘mafua ya nguruwe’.
Watu wengi wamepoteza maisha katika zaidi ya nchi 24 duniani. Ikiwa inakadiriwa watu 1000 wamefariki katika Marekani pekee, na kumfanya Rais Barack Obama kutangaza hali ya hatari, nia ikiwa kupunguza urasimu wa kisheria katika kutoa tiba kwa wagonjwa.
Mexico ni nchi ya kwanza kukumbwa na ugonjwa huu, ikiwa siku tatu kabla ya ujio wa Rais Barack Obama aliyetembelea nchi hiyo kwa nusu siku 16,April,2009, mtu ambaye alishikana naye mikono na kumuongoza katika maeneo ya makumbusho, mkurugenzi wa mambo ya kale na makumbusho (National Anthropology Museum) Felipe Solis, alifariki wiki moja baada ya tukio hilo, linaandika gazeti la Daily Mail la Uingereza.
Ingawa White House iliwahi kubainisha kuwa afya ya Rais i salama na hilo walilizangatia kabla hajafanya ziara hiyo, nayo serikali ya Mexico kukanusha kuwa Felipe Solis hajafariki kwa mafua ya nguruwe, lakini vyombo vya habari na jamii ya Mexico inaamini dalili zote zilikuwa wazi hadi kifo chake kuwa ni AH1N1.
Pamoja na vifo vingi vinavyotokana na ugonjwa huu duniani malalamiko ya wakulima wa nguruwe ni dhidi ya jina hili na hasa kuhusianisha moja moja kwa na nguruwe.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema litaacha kuuita ugonjwa huu ‘mafua ya nguruwe’ ili kukwepa madhila ya makosa ya jina kwa biashara ya nguruwe duniani.
Nchini Tanzania taarifa ya karibuni ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya iliyosambazwa kwa vyombo vya habari na Mheshimwa Blandina Nyoni, iliendeleza kutumia jina ‘mafua ya nguruwe’.
Ingwa katika taarifa ile iliyopatatikana kulikuwa na maneno yenye kutia moyo kuwa ugonjwa huu hautokani na ‘kula nyama’ ya nguruwe. Lakini maneno haya hayakupewa uzito na vyombo vya habari.
Waatalamu wa biashara wanasema ‘mpe mbwa jina baya’ (Give a dog bad name) wakimaanisha katika ‘branding’ kosa likifanyika na jamii ikaamini katika hilo, lazima kazi ya ziada ifanyike ili kurudisha imani ya walaji.Hivyo umakini unahitajika sana katika kutoa jina.Nyama ya nguruwe sasa imepewa jina baya, tena ambalo hata haliusiki nalo kisayansi.
Watanzania ni mashahidi na bado tunakumbuka jinsi Mzee Yusuph Makamba alivyokauka koo kujaribu kurudisha imani ya wavaaji wa ndala zilizopewa jina masihala la ‘yebo yebo’ wakati akiwa Mkuu wa Mkoa wa Daresalaam. Kuna waliopigana na kujeruhiwa na wengine kuripotiwa kupoteza uhai kisa jina baya la ‘yebo yebo’
Hakuna anayejua madhala ya ndala zile za kwa kiwanda husika, lakini zile ndala ni zinazopendwa katika Ulaya na Uchina na hasa kwa maeneo ya baharini. Lakini katika Tanzania si mali kitu, na ni fedheha kwa mavaaji. Hii yote inaonesha uhusiano wa jina baya na imani ya mlaji.
Nguruwe ni nyama nyeupe ambayo katika soko la Ulaya na Marekani ni nyama pendwa kwa sababu za kiafaya ukilinganisha na nyama nyekundu.Ni wazi kuwa imani ya walaji nyama nyeupe katika soko la Ulaya, Amerika ambako walaji nyama wameonesha kuacha kula nyama nyekundu (ng’ombe na kondoo) sasa wataanza kula nyama nyeupe nyingine tofauti na nguruwe, yaaani kuku ambayo ilipigwa mweleka na ‘mafua ya ndege’!
Hili si sana kwa walaji wa Afrika, kwani walaji wa nyama wa ulaya hawataki kula nyama nyekundu kwa sababu za kiafya, na ni wazi kuwa mauzo ya mboaga za asilia (organic vegetable) zitapata nafasi kubwa kutokana na makosa haya ya ‘jina baya’ kwa nguruwe.
Profesa Marie Grammer wa Chuo Kikuu cha Minnesota, nchini Marekani ambaye pia mtaalamu wa magonjwa ya nguruwe anasema kitaalamu hakuna uhusiano wa wazi kati ya minofu ya nguruwe na bidhaa zake na H1N1. Isipokuwa ugonjwa unaotokana na muingiliano kati ya binadamu na wanyama.
Na wala ugonjwa hauwezi kuambukizwa kwa kula nyama ‘iliyoandaliwa vizuri’ au mazao mengine ya nguruwe.
Maneno vizuri yanabainisha hali ya usalama, hivyo pasi na usafi kuzingatiwa ni wazi kuwa nyama ya nguruwe inaweza kuwa hatari!
Kituo cha kupambana na magonjwa ya kuambukiza cha Marekani kinasema virusi vinavyoleta magonjwa kwa nguruwe ni ,A influenza, na wala hakuna uhusiano na H1N1 na nguruwe hivyo kutaka makosa ya jina yasahihishwe.
Tangu rai ya kuomba kubadilishwa makosa haya mara tu ugonjwa huu ulipojitokeza mwezi Aprili nchini Mexico, bado jina hili limeendelea kutumika na vyobmo vya habari nchini Tanzania na Dunia kwa ujumla.
Ingawa takwimu hazipo wazi ni kwa kiasi gani biashara ya nyama ya nguruwe ilivyo na manufaa lakini ukweli ni kwamba, kuna jamii nyingi katika mikoa ya Mbeya, Morogoro,Arusha,Iringa,Sumbawanga,Kilimanjaro, Morogoro na Daresalaam wameathirika na wanaendelea kuathirka kutokana na hofu hii kwa walaji.
Daresalaam ni soko kuu la nyama ya nguruwe maarufu kama ‘kitimoto’ambayo sasa katika miji na vitongoji vingi vya kibiashara nchini ni rahisi kukuta mabanda ya kuchoma nyama ya nguruwe. Basi yatupasa kurekebisha kuita ‘jina sahihi’ maana hofu tunayoijenga haina mwisho mwema kwa jamii ya wafugaji wa nguruwe.

No comments: